Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano, Mhe. Elias John Kwandikwa (kushoto) akisisitiza jambo
kwa watendaji wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) Mkoa wa Tanga
mara baada ya kukagua barabara ya Turiani- Mziha- Handeni yenye urefu wa
kilomita 108 jumatatu Februari 12, 2018. Kulia ni Meneja wa TANROADS
Mkoa wa Tanga, Mhandisi Alfred Ndumbaro.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano, Mhe. Elias John Kwandikwa (kushoto) akisisitiza jambo
kwa Viongozi wa Wilaya ya Handeni wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo,
Godwin Gondwe (wa pili kushoto) mara baada ya kukagua barabara ya
Handeni- Manyara yenye urefu wa kilomita 88 jumatatu Februari 12, 2018.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano, Mhe. Elias John Kwandikwa (kushoto) akijadiliana jambo
na Mkuu wa Wilaya ya Handeni Godwin Gondwe (katikati) na Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, William Makufye wakati wa
ziara yake ya kukagua miradi ya ujenzi wa barabara Wilayani humo
jumatatu Februari 12, 2018.
(NA MPIGAPICHA WETU)
…………………………………………………………………….
Na Ismail Ngayonga- MAELEZO- Handeni
SERIKALI imesema ipo mbioni
kuanzisha mfumo wa utambuzi na usajili wa barabara zote nchini, hatua
inayolenga kuziwezesha barabara zote kujengwa katika viwango
vinavyofafana na ubora wa huduma ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa
wananchi hususani wa maeneo ya vijijini.
Hayo yamesemwa leo Wilayani
Handeni Mkoani Tanga na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,
Elias Kwandikwa wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya ujenzi wa
barabara katika Wilaya za Handeni, Kilindi na Korogwe.
Kwandikwa alisema ili kutekeleza
adhma hiyo, Serikali imekusudia kuiwezesha Wakala wa Barabara za Mijini
na Vijijini (TARURA) kwa kuiongezea uwezo wa vitendea kazi na waatalamu
wa kutosha ili kuhakikisha kuwa miradi ya barabara iliyopo katika
Halmashauri zote nchini inakuwa na chombo maalum cha usimamizi.
“Ni wajibu wa Watendaji wote
kushirikiana katika kusimamia miradi ya barabara, kwa kutoa ushirikiano
wa kutosha kwa TARURA ikiwemo kuipata fedha pale inapokwama katika
kutekeleza wajibu wake hususani katika maeneo korofi yanayohitaji fedha
maalum” alisema Kwandikwa.
Alisema kukamilika kwa miradi ya
barabara katika maeneo mengi ya vijijini kutawezesha wananchi kushiriki
kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kiuchumi ikiwemo uzalishaji na
usafirishaji wa mazao na pembejeo na hivyo kuvutia uwekezaji katika
miradi mikubwa ya maendeleo.
Aidha Kwandikwa alisema ili
kutekeleza vyema majukumu yake, ni wajibu pia wa TARURA kujisogeza
karibu zaidi kwa jamii ikiwemo kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wananchi
na Viongozi mbalimbali katika Mamlaka ya Serikali za mitaa, hatua
inayolenga kujenga uelewa wa mamlaka, wajibu na majukumu ya taasisi
hiyo.
Aliongeza kuwa asilimia 80 ya
uwezeshaji wa uchumi katika maeneo ya vijijini unategemea upatikanaji wa
miundombinu ya barabara za uhakika, hivyo ni wajibu wa TARURA
kuhakikisha kuwa wananchi wanashiriki kikamilifu katika shughuli za
kuinua uchumi pasipo kukabiliwa na changamoto zisizo na ulazima.
Akifafanua zaidi Kwandikwa
alisema Serikali ipo tayari wakati wowote kutoa ushirikiano unaohitajika
ikiwemo kupokea ushauri, mapendekezo na maoni kuhusu hatua mbalimbali
zinazopaswa katika kuboresha na kusimamia miundombinu ya barabara
inayosimamiwa na taasisi hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya
ya Handeni, Godwin Gondwe alisema Wilaya yake imejipanga kikamilifu
katika kuhakikisha kuwa sheria, kanuni na taratibu mbalimbali zinafuatwa
katika usimamizi wa miundombinu ya barabara kwa kuwa hatua itasaidia
kuleta maendeleo ya haraka kwa wananchi.
“Wilaya imejipanga kikamilifu
katika kusimamia sheria ikiwemo kudhibiti mifugo inayovuka kutoka upande
mmoja wa barabara kwenda mwingine, kwa kuwa mara nyingi imekuwa
ikichangia uharibifu wa miundombinu ya barabara zetu” alisema Gondwe.