SALAMU
ZA MWAKA MPYA ZA MHE. NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,
WAZEE NA WATOTO ZIKISISITIZA JUU YA WAJIBU WA WATOA HUDUMA ZA AFYA NA
MABARAZA YA KITAALUMA PAMOJA NA HAKI ZA WANANCHI KUPATA HUDUMA BORA ZA
AFYA.
Ndugu Wananchi,
Nachukua
fursa hii kuungana nanyi nyote kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa
kutufikisha salama siku hii ya leo tunapoanza mwaka mpya 2018. Hii ni
neema pekee ambayo Mwenyezi Mungu ametujaalia kwani kuna wengi
walitamani kuifikia siku hii lakini hawakubahatika. Hivyo, nawatakieni
nyote kheri na fanaka katika mwaka huu mpya.
Napenda
kutumia fursa hii pia kuwashukuru na kuwapongeza Wanataaluma na Watoa
huduma za afya wote kwa kuendelea kutoa huduma kwa ari, juhudi, uaminifu
na uadilifu licha ya changamoto mbalimbali wanazokutana nazo katika
utendaji kazi wa kila siku. Nami nawatia shime na hamasa ili muendelee
na moyo huo wa kuwahudumia na kuwatumikia Wananchi.
Natambua
kuwa Sera yetu ya Afya inataka tuijenge jamii yenye afya bora na
ustawi ambayo itachangia kikamilifu katika maendeleo ya mtu binafsi
pamoja na yale ya Taifa. Aidha, Sera na Sheria zetu mbali mbali
zinatambua umuhimu na nafasi ya Mabaraza ya kitaaluma katika kuboresha
na kusimamia viwango vya maadili ya wanataaluma walio chini ya Wizara
yangu. Jambo hili ni muhimu sana hususan tukizingatia ongezeko la
minong’ono, manung’uniko na hata malalamiko kutoka kwa wananchi dhidi ya
baadhi ya watoa huduma ambao wanakiuka taratibu au miiko ya kazi zao
na hivyo kuathiri ubora wa utoaji huduma.
Nimeona
kama sehemu ya salamu zangu za mwaka mpya wa 2018, nitoe maelekezo
yatakayoweza kutusaidia kuboresha utoaji huduma katika sekta ya afya
kupitia Watoa Huduma za Afya na Mabaraza ya Kitaaluma na pia
kuwakumbusha wananchi juu ya haki yao ya msingi ya kupata huduma bora za
afya na wajibu wao wa kuhakikisha hilo linatokea.
- Wanataaluma wa Afya:
Nawakumbusha
Wanataaluma wote katika Sekta ya afya, yaani Madaktari, Wauguzi,
Wakunga, Wafamasia, Wataalam wa Maabara, Madaktari na Wataalam wa Afya
ya Kinywa na Meno, Wataalam wa Mionzi, Wataalam wa viungo bandia na
Wafiziotherapia, kwamba taaluma hizi ni za Kuheshimika sana (Noble), na
hivyo kazi na majukumu mnayoyatekeleza yamejengwa katika misingi ya
kuaminiwa (Trust) na Jamii, na kwamba kuaminiwa huko ndio kiini cha
heshima ya taaluma hizi. Hivyo, ni wajibu wa kila mwanataaluma
kutekeleza majukumu yake akiongozwa na msingi huu mkuu, pamoja na
misingi mingine ya kimaadili ambayo ni: HURUMA, UKWELI, FARAGHA, USIRI,
UAMINIFU, USAWA, HAKI, UTU na MAHUSIANO MEMA.
Aidha,
naendelea kuwakumbusha kuwa, utekelezaji wa majukumu yenu siku zote ni
lazima uzingatie matakwa ya Katiba ya Nchi ambayo ndiyo Sheria Mama.
Mkumbuke kuwa Dira Kuu katika utekelezaji wa wajibu wenu kama
wanataaluma ni uzingatiaji wa haki, heshima, usawa na utu kwa wote
wanaokuja mbele yenu kupata huduma za kitaaluma. Vile vile mkumbuke kuwa
siku zote mnao wajibu wa kutekeleza majukumu yenu ya kitaaluma kwa
kuzingatia Sheria nyingine za nchi, Kanuni, Sera, pamoja na Miongozo
iliyowekwa kwa mujibu wa Sheria za Nchi, pamoja na Miongozo na Matamko
ya Kimataifa ambayo tumeridhia kuyatekeleza na kuyazingatia.
Aidha,
nawakumbusha Wanataaluma wote Waandamizi na Viongozi katika Sekta ya
Afya kwamba ni wajibu wao kuhakikisha kuwa Wanataaluma na watoa huduma
wote walio chini yao wanazingatia na kufuata Sheria, Kanuni, Weledi
(Professionalism) pamoja na Maadili (Ethics) ya taaluma au kazi zao na
kuchukua hatua stahiki za nidhamu, kwa mujibu wa Sheria, kunapotokea
ukiukwaji. Pia kila Mwanataaluma ana wajibu wa kuhakikisha kuwa
Wanataaluma wanaomzunguka wanatekeleza majukumu yao kwa misingi hii
iliyotajwa na ana wajibu wa kutoa taarifa kwa Mamlaka husika pindi
panapotokea ukiukwaji au kuonekana viashiria vyake. Jambo hili ni muhimu
sana ili kama Wanataaluma msikubali kazi nzuri inayofanywa na wengi
iharibiwe na wakorofi wachache miongoni mwenu.
- Mabaraza ya Taaluma
Natumia
fursa hii pia kuyakumbusha Mabaraza yote ya Kitaaluma yaliyo chini ya
Wizara yangu kuhakikisha kuwa wanasimamia kikamilifu Sheria
zinazosimamia Wanataaluma wao. Hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa
mtu yeyoye anayetaka kutoa huduma za kitaaluma ni lazima awe na elimu
na ujuzi unaokubalika, na atambulike kwa kupewa usajili na leseni ya
kufanya kazi za kitaaluma. Dhima ya Wizara ni kuona kuwa jamii inapata
huduma zilizo sahihi, salama na zenye ubora unaokubalika. Hivyo,
Mabaraza yana wajibu wa kuchukua hatua stahiki kwa yeyote atakayebainika
kukiuka Sheria na taratibu zilizowekwa.
- Wanajamii
Napenda
kuwajulisha wanajamii wote kuwa mnayo haki ya kupata huduma za afya
zilizo salama, bora na ambazo zinazingatia misingi ya usawa, haki na
zinazozingatia heshima na utu wa binadamu. Pia, mnayo haki ya kupata
taarifa sahihi kuhusu hali ya afya au ugonjwa, na kupata ushauri au tiba
kwa wakati na kwa gharama zinazokubalika. Hivyo, wanajamii mnao wajibu
wa kutoa taarifa wakati wowote mnapobaini kuwepo kwa viashiria au
vitendo vya ukiukwaji wa maadili, sheria na taratibu zilizowekwa kwa
misingi ya Sheria za Nchi. Kati ya vitendo visivyo kubalika ni pamoja
na rushwa, ubadhirifu wa mali za umma, wizi, lugha chafu, matusi,
dharau, mavazi yasiyo na heshima, ulevi, matumizi ya madawa ya kulevya,
uropokaji wa siri za wagonjwa, unyanyasaji wa kijinsia, matumizi mabaya
ya simu za mkononi na tabia nyingine zote zinazofanana na hizi.
Hitimisho na Maagizo,
Nahitimisha salamu zangu kwa kutoa maagizo yafuatayo:
- Wanataaluma na Watoa Huduma,
- Kila Mwanataaluma na mtoa huduma anapaswa kuvaa kitambulisho chenye jina lake kamili wakati wote awapo eneo la kazi. Hii ni pamoja na uvaaji wa sare nadhifu za kazi.
- Viongozi wa kila kituo cha kutolea huduma za afya wahakikishe kuwa kuna Masanduku ya kutolea maoni yanayoonekana kwa uwazi na urahisi, na kwamba maoni yanayotolewa yanafanyiwa kazi ipasavyo.
- Viongozi wa kila kituo cha kutolea huduma za afya wahakikishe kuwa kuna Ofisi za kuwasilisha malalamiko zilizo karibu ili kufikiwa na wateja wote wenye uhitaji.
- Viongozi wa vituo vya kutolea huduma za afya wanapaswa kuweka wazi namba zao rasmi za simu kwenye mbao za matangazo ambazo mwananchi atazitumia kutoa taarifa au kuwasilisha maoni au malalamiko.
- Mganga Mkuu wa Kituo, Mganga Mkuu wa Wilaya, Mganga Mkuu wa Mkoa au Kiongozi mwenye mamlaka katika utoaji wa huduma za afya ana wajibu wa kuwasilisha malalamiko dhidi ya mwanataaluma anayetuhumiwa katika Baraza la Taaluma husika pindi panapotokea vitendo vya ukiukwaji wa weledi (Professionalism) na maadili (Ethics).
- Mabaraza ya Taaluma
Kila
Baraza la taaluma pamoja na Wawakilishi wao waliopo katika Wilaya,
Mikoa na ngazi ya Taifa waweke wazi utaratibu wa kisheria wa
uwasilishwaji wa malalamiko na taratibu za Uchunguzi wa vitendo viovu
dhidi ya wanataaluma. Hii ni pamoja na kuweka wazi namba za simu na
anuani za barua pepe (e-mails).
- Wanajamii kwa ujumla:
- Nawasihi Wanajamii kuwaheshimu na kuwathamini Watoa huduma za Afya nchini
- Nawasihi wanajamii wote kutoa taarifa, maoni au malalamiko dhidi ya wanataaluma au watoa huduma wanaokiuka misingi ya Taaluma zao, au wanaotoa huduma kinyume na Taratibu zilizopo kwa:
- Uongozi wa kituo husika,
- Mganga Mkuu wa Wilaya,
- Mganga Mkuu wa Mkoa,
- Ofisa wa TAKUKURU,
- Baraza la Taaluma Husika,
- Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, au
- Katibu Mkuu OR-TAMISEMI, au kwa
- Kiongozi yeyote wa Serikali, ili awasilishe taarifa hizo kunakostahili.
Aidha ni vema taarifa itolewe kwa kumtaja mhusika ili kurahishisha ufuatiliaji.
Nawatakieni nyote Kheri na Afya Njema kwa mwaka mpya wa 2018.
Ahsanteni sana.
Dkt. Faustine Ndugulile (Mb)
NAIBU WAZIRI WIZARA YA AFYA,
MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,WAZEE NA WATOTO.
31/12/2017.