KONGAMANO LA VIJANA JIMBO LA MAGOMENI KUHUSU UDHALILISHAJI

January 01, 2018

01
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Wanawake na Watoto Zanzibar Nasima Haji Chum azungumza na Vijana wa Jimbo la Magomeni Zanzibar katika Kongamano la Wazi lilozungumzia udhalilishaji wa Kijinsia huko uwanja wa Magae ulioko katika Jimbo hilo.
 …………….
Na Maryam Kidiko /Mwashungi Tahir- Maelezo Zanzibar.        
MKURUGENZI wa Idara ya Maendeleo ya Wanawake na Watoto Zanzibar Nasima Haji Chum amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaumizwa sana na suala la udhalilishaji wa Kijinsia na inaendelea kupanga mipango madhubuti juu ya wanaofanya vitendo hivyo.
Hayo aliyasema katika Kongamano la Vijana wa Jimbo la Magomeni lililofanyika katika uwanja wa Magae mjini Unguja kuhusu suala la  udhalilishaji wa kijinsia unaoendelea kukithiri katika Jamii nini kifanyike ili suala hili liweze kupunguwa.
Alisema suala la udhalilishaji linaendelea kuzungumziwa kwa upana katika taasisi mbali mbali Unguja na Pemba hivyo  lengo na adhma   iliyokusudiwa na Serikali ya Zanzibar ni kulitokomeza suala hilo na kumalizika kabisa.
Nasima aliwataka wazazi kuwa karibu sana na vijana kuhusu kusimamia malezi ya watoto ili kujuwa tabia zao za kila siku katika maisha yao wanayoishi kwani kufanya hivyo kutapelekea kujuwa vikitokea kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji wanavyofanyiwa itajulikana kwa haraka.
“ili suala hili tuweze kulipatia taarifa za uhakika inatubidi sisi wazazi na walezi tuwe karibu sana na watoto wetu na wao watakuwa wawazi kusema suala hili la udhalilishaji litapowafikia”alisema Mkurugenzi huyo.
Aidha alisema Wananchi wote washirikiane kwa pamoja na Wizara husika katika jambo hili kufanya hivyo kutapelekea kutokomeza kabisa suala la udhalilishaji katika Visiwa vyetu.
“Nawaomba Vijana muweze kuacha muhemko ambao unasababisha kuongeza suala hili la udhalilishaji “alitowa msisitizo Mkurugenzi huyo.
Nae Mwenyekiti wa Vijana Jimbo la Magomeni Ussi Jecha Haji alisema lengo la kongamano hilo ni kuisaidia Serikali ya Zanzibar kuweza kupambana na suala la udhalilishaji wa kijinsia kwa nguvu zote.
Mwenyekiti huyo aliwataka Vijana kutoka Majimbo mengine mbali mbali kuweza kuiga mfano wao ili kushirikiana pamoja na Serikali kupinga vitendo  vya udhalilishaji uliokithiri katika Jamii.

Kwa upande wa risala ya Vijana Jimbo la Magomeni walieleza kuwa Jamii yetu katika Nchi imekubwa na janga kubwa la ukatili wa udhalilishaji wa kijinsia kwa kukithiri vitendo vya udhalilishaji na ulawiti kwa watoto wadogo wa kike na wa kiume ambavyo vinafaywa na watu wasio na hofu.
Hivyo Jumuiya ya Vijana (UVCCM) jimbo la Magomeni inaiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Baraza la Wawakilishi kutunga Sheria mpya itakayozuwia uingizaji wa picha za ngono, Dawa za kuongeza nguvu za kiume imeonekanwa ndio sababu kubwa ya kuongezeka vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia katika jamii.
Wakati huo huo Muwasilishaji wa Zafela huduma na sheria Siti Abasi Ali aliweza kutowa mada ya masuala ya udhalilishaji alisema suala la simu kwa Vijana linapelekea kuongezeka kwa masuala ya udhalilishaji kwa kuangalia mambo yanayochochea vitendo hivyo.
Vile vile alisema kuwa wazazi wawe makini sana na watoto wao wakati wa kuwafanyia usafi wa mwili na wa nguo zao ili wakifanyiwa udhalilishaji waweze kujuwa haraka.
“Nawaomba Wazazi na Walezi wa watoto wetu tuwache tabia ya kuwabebesha kila kitu wadada wa kazi kwa kuwafanyia kila kitu watoto bila sisi kuwashuhulikia hivyo tujenge tabia ya kuwashuhulikia watoto wetu sisi wenyewe “alisema Mwanasheria wa Zafela.
Kauli mbiu ya kongamano hilo ilibeba ujumbe muhimu unaosema (USIKUBALI, ZUNGUMZA, TOA TAARIFA) kwa pamoja tushirikiane kuzuwia aina zote za udhalilishaji.
Kongamano hilo la wazi limeandaliwa na Vijana wa Jimbo la Magomeni lililozungumzia mada za udhalilishaji ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra ya kuazimisha miaka 54 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
     
             IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO ZANZIBAR.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »