*Ahimiza wakazi wa Ruangwa wajiunge na bima hiyo
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa wilaya ya Ruangwa wajiunge na
Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili waweze kumudu gharama za matibabu bila
kulazimika kuwa fedha taslimu.
Ametoa
wito huo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa mji
wa Ruangwa na vijiji vya jirani katika mkutano wa hadhara uliofanyika
kwenye viwanja vya CWT, mjini Ruangwa, mkoani Lindi.
“Leo
hii nimetoa kadi za CHF kwa wazee 4,000 wa wilaya hii. Ninaishukuru
Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kwa kutenga fedha na kuwalipia wazee
hawa ili wanufaike na bima hii ya afya kama ambavyo imeelekezwa kwenye
Ilani ya Chama cha Mapinduzi.”
“Ninatoa
wito kwa wananchi wengine walipie sh. 15,000 kwa mwaka ili wapatiwe
kadi kwa ajili ya watu sita wa familia zao; yaani mhusika, mwenza wake
na watoto wanne. Bima hii inasaidia kwa vile unapata matibabu hata kama
huna fedha taslimu,” alisema.
Waziri
Mkuu alikabidhi kadi kwa Mzee Issa Juma Ngalapa, mkazi wa kata ya
Nachingwea pamoja na Mzee Suleiman Stola Lihepa wa kijiji cha
Kilimahewa, kata ya Nachingwea kwa niaba ya wazee wote waliotakiwa
kupatiwa kadi hizo.
Akitoa
ufafanuzi juu ya mpango huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Ruangwa Bw. Andrea Chezue alisema mpango wa kutoa kadi za bima ya afya
kwa wazee wameuita ‘CHF Endelevu’ kwa sababu walifanya tathmini na
kubaini kuwa matibabu yao yana gharama, na yasipolipiwa, dawa zitaisha
au wazee hao hawataweza kupatiwa huduma.
“Katika
Halmashauri tulifanya utambuzi wa wazee wa kuanzia miaka 60 na
kuendelea kwenye vijiji vyote na kubaini kuwa kuna wazee 4,000. Tukaamua
Halmashauri iwalipie sh. 15,000 kwa kila wazee sita kama ilivyo katika
kaya ili tuweze kuchangia gharama za matibabu yao,” alisema.
“Mzee
akipatiwa kadi hii, inakuwa ni ya kudumu, anaitumia miaka yote. Si ya
kulipia kila mwaka kama zilivyo zile nyingine. Hadi sasa tumeshatoa kadi
kwa wazee 2,700 na tunaendelea kutengeza kadi hadi tukamilishe zote.
Tumepanga kuwa kila mwaka, tutafanya utambuzi wa wazee katika vijiji
vyote ili wale wanaofikisha umri huo, nao pia waingizwe kwenye mpango
huu,” alisema.