Na Rashid Nchimbi wa Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi la Polisi mkoani Arusha limeweza
kudhibiti matukio ya uhalifu kwa 17.9% mwaka jana 2017 tofauti na mwaka
2016 ambapo kulikuwa na matukio 2,817 wakati mwaka 2017 kulikuwa na
matukio 1,963 pungufu ya matukio 854, huku matukio ya uvunjaji
yakipungua toka 604 hadi 294 ikiwa ni zaidi ya mara mbili ya mwaka 2016.
Akitoa
taarifa hiyo Kamanda Polisi wa mkoa wa Arusha, Naibu Kamishna (DCP)
Charles Mkumbo alisema kwamba, matukio hayo ya uhalifu yamezidi kupungua
mwaka hadi mwaka ambapo mwaka 2016 matukio yalipungua kwa 6.8%
ikilinganishwa na mwaka juzi 2015, na kuongeza kwamba hayo yote
yanatokana na ushirikiano mzuri kati ya wananchi na Jeshi hilo.
Makosa
mengine ambayo yamepungua ni pamoja na Unyang’anyi wa kutumia nguvu
ambayo mwaka 2016 yalikuwa 86 na mwaka jana 2017 yameshuka hadi 40 huku
makosa ya kutupa watoto yalikuwa 38 lakini mwaka 2017 yameshuka hadi
kufikia 13.
“Matukio
ya Mauaji nayo yalipungua kutoka 65 hadi 58 kwa mwaka 2017, wizi wa
Watoto yalikuwa 20 na yamepungua hadi matukio mawili, na yalioongezeka
ni Ubakaji na Ulawiti ambapo mwaka 2016 matukio ya Ubakaji yalikuwa 144
na mwaka jana yameongezeka matukio matano wakati makosa ya Kulawiti
yalikuwa 58 yameongeza kufikia 62”. Alisema Kamanda Mkumbo.
Aidha
katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya Jeshi hilo liliweza kukamata
Cocaine gramu 480, Bhangi kilogramu 211 na gramu 760 na Mirungi
kilogramu 317 na gramu 710 pamoja na watuhumiwa 554.
Kwa
upande wa Usalama Barabarani Jeshi hilo limeweza kukusanya jumla ya
shilingi 3,825,180,000 kutokana na makosa mbalimbali ambapo kwa mwaka
2016 Jeshi hilo lilikusanya jumla ya shilingi 4,708,680,000 kutokana na
makosa hayo.
Hata
hivyo Kamanda Mkumbo alisema kwamba kushuka kwa makosa ya Usalama
Barabrani kumetokana na watumiaji wengi wa barabara hususani madereva
wa vyombo vya usafiri kufuata vyema sheria za Usalama Barabarani hali
hiyo imetokana na elimu iliyokuwa inatolewa na Jeshi hilo kitengo
Usalama Barabarani kupitia Radio mbalimbali za hapa jijini Arusha, elimu
kwa wanafunzi lakini pia elimu ya kituo hadi kituo kwa wadereva wa
Pikipiki za abiria.
Pamoja
na mafanikio yaliyopatikana katika kupunguza uhalifu, Kamanda Mkumbo
ameendelea kutoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Arusha kuendelea
kushirikiana na Jeshi hilo katika kutoa taarifa za uhalifu na wao
kuzifanyia kazi mara moja lakini pia ametoa onyo kwa yoyote
atakayedhubutu kushiriki kutenda uhalifu, atakamatwa na kufikishwa
kwenye vyombo vya sheria.