Mkazi wa Ngungwa,kata ya Kongowe
wilayani Kibaha ,Mkoani Pwani,Bahati Semwe akimuonyesha mbunge wa jimbo
la Kibaha Mjini ,Silvestry Koka,maji ya kisima ambayo wanatumia ,hivyo
amemuomba kusimamia kero hiyo ili wapate maji safi na salama
Mbunge wa jimbo la Kibaha Mjini
Silvestry Koka,akizungumza katika mkutano wa hadhara ,huko Miembesaba
‘A’ kata ya Kongowe wakati wa muendelezo wa ziara yake ya jimbo,ambapo
hadi sasa ameshatembelea kata ya Visiga,Misugusugu na Kongowe.
Picha na Mwamvua Mwinyi
……………
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
MBUNGE wa jimbo la
Kibaha Mjini , Silvestry Koka,ametoa kiasi cha sh.milioni mbili
zitakazosaidia kutumika kuezeka madarasa yaliyojengwa baada ya kuungua
katika shule ya msingi Kongowe.
Mwaka 2016 vyumba vitatu vya madarasa na ofisi ,shuleni hapo viliungua kutokana na kutokea shoti ya umeme .
Koka alitoa mchango
huo ,wakati alipokuwa kwenye mkutano wa hadhara ,Miembesaba ‘A’kata ya
Kongowe katika muendelezo wa ziara yake ya jimbo.
Aliomba fedha
zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo pamoja na kukamilisha
ujenzi wa shule hiyo zisimamiwe na kutumika kwa matumizi lengwa.
Akizungumzia
changamoto za kielimu kijumla ,alisema kwasasa maeneo mengi yanakabiliwa
na tatizo la upungufu na uchakavu wa miundombinu .
Koka aliitaka jamii
,wadau ,kamati za shule na viongozi mbalimbali kushiririkiana kuongeza
vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo mashuleni .
“Kulikuwa na kero
kubwa ya uhaba wa madawati na kusababisha watoto wetu kusoma huku wakiwa
wamekaa chini na kupata vifua kutokana na vumbi”
“Lakini tumejitahidi
tumemaliza kero hiyo ,kilichobaki kwasasa ni tatizo la
miundombinu,ambapo tushikamane kumaliza ama kulipunguza ili watoto
waondokane na mlundikano wa kusoma kwenye darasa moja ama kusoma kwa
awamu” alifafanua Koka.
Koka aliwaasa wazazi
na walezi ambao watoto wao wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza
na darasa la kwanza kuwapeleka shule .
Alisema elimu ndio nguzo na hazina ya watoto ,hivyo ni jukumu la wazazi kuona umuhimu wa kuwapa haki hiyo watoto hao.
Kuhusu tatizo la
kutumia maji ya visima badala ya maji safi na salama kutoka Dawasco huko
eneo la Ngungwa kata ya Kongowe ,alisema linashughulikiwa .
Alisema tatizo la
maji lililokuwepo awali Kibaha ,sivyo ilivyo sasa kwani wamepiga hatua
,mradi wa Ruvu Juu na Ruvu Chini imekamilika hivyo kazi iliyobakia ni
kusambaza .
Katika afya ,Koka
alielezea anaendelea kusimamia changamoto wanazokabiliana nazo ikiwemo
uhaba wa watumishi,vifaa tiba na madawa.
Alisema kutokana na
hilo ,mwezi June mwaka jana ,alileta kontena la vifaa tiba mbalimbali
lililogharimu mil.400 na vifaa hivyo vilisambazwa kituo cha afya mkoani
na zahanati zilizopo jimboni hapo.
Alieleza ataendelea
kusimamia asilimia 10 ya vijana ,wazee,wanawake,walemavu kwenye mapato
ya ndani ya halmashauri ya Mji wa Kibaha ,ili inufaishe makundi hayo.
Koka alisema kwasasa
,asilimia 10 inatakiwa igawanywe asilimia 4 akinamama,asilimia 4
vijana,wazee na walemavu asilimia moja ,moja.
Nae afisa elimu kata
ya Kongowe,Aziza Matekenya alisema wakati baadhi ya majengo ya shule ya
msingi Kongowe yakiungua shule hiyo ilikuwa na wanafunzi 1,840.
Alisema halmashauri
ilitoa milioni kumi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa hayo na imeahidi
kuongeza milioni 20 kwa ajili ya umaliziaji.
Aziza
alieleza,kwasasa shule ina jumla ya vyumba 12 vya madarasa vinavyotumika
,vitatu vichakavu ambapo inahitaji vyumba vya madarasa 40 ili kukidhi
mahitaji.
Shule hiyo ilijengwa miaka ya 70 ,kwasasa ina wanafunzi 2,820 na walimu 35 .