PANAFRICAN ENERGY YATOA YAFADHILI UJENZI WA WODI YA ‘MAMA NGONJEA’ HOSPITALI YA WILAYA KINYONGA KILWA KIVINJE NA KUKARABATI WODI ZA UZAZI NA CHUMBA MAALUM CHA UANGALIZI WA AKINA MAMA

December 08, 2015


Meneja Uwajibikaji kwa jamii kutoka Kampuni ya PanAfrican Energy Andrew  Kangashaki  (kushoto ) na Mkurugenzi wa Wilaya ya Kilwa Twalib Mbasha wakikabidhiana mkataba wa miradi  ya ujenzi wa nyumba ya mama ngojea  katika hospital ya Kinyonga  na ukarabati wa wodi  ya uzazi  mara baada ya kumaliza kusaini mikataba hiyo katika hafla fupi iliyofanyika jana Kilwa Kivinje.
Meneja Uwajibikaji kwa jamii kutoka Kampuni ya PanAfrican Energy Andrew  Kangashaki(wa tatu kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Wilaya ya Kilwa Twalib Mbasha (wa tatu kulia) wakisaini makubaliano ya miradi miwili ya ujenzi wa mama ngojea ‘maternity waiting home’ yaani nyumba maalum kwa kina mama wajawazito watakaokua wakisubiri kujifungua itakayojengwa katika hospitali ya Kinyonga – Kilwa Kivinje na kukarabati wodi ya uzazi na chumba maalum cha uangalizi wa akina mama mara tu baada ya kujifungua katika kituo cha afya cha Kilwa Masoko. 

Huku wakishuhudiwa na Mwanasheria wa Wilaya Mh. Godfrey Makary (wapili kutoka kulia), Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Juma Abdalah Njwayo(wa pili kushoto), Mbunge wa jimbo la Kilwa Kaskazini kupitia chama cha CUF Mh. Vedasto Edgar Ngombale(wakwanza kushoto) pamoja na Mbunge wa Kilwa Kusini kupitia chama cha CUF Selemani Bungawa a.k.a Bwege(wakwanza kulia).

Mbunge wa Kilwa Kusini kupitia chama cha CUF Selemani Bungawa a.k.a Bwege(wapili kulia) akitoa neno la shukrani kwa Kampuni ya PanAfrican Energy kwa niaba ya wananchi wa Kilwa Kusini mara baada ya makabidhiano ya mkataba wa miradi itakayowanufaisha wananchi wa kilwa.
Wafadhili wa mradi wa ujenzi wa wodi ya wazazi Kampuni ya PanAfrican Energy pamoja wakiwaonesha wanahabari chumba cha uzazi katika kituo cha afya cha Kilwa Masoko ambacho kipo katika mradi uliosainiwa kati ya wilaya ya Kilwa na kampuni hiyo. Hii ni katika kuunga jitihada za serikali za kuboresha huduma za afya.
Hali halisi ya mazingira ya wodi ya wagonjwa katika kituo cha afya cha Kilwa Masoko, hii ni wodi ya wanaume. Kiyuo hichi cha afya  kilijengwa mwaka 1952 enzi za ukoloni mpaka sasa hakijawahi kukarabatiwa.
Wakisaini makubaliano ya miradi ya ujenzi wa mama ngojea na ukarabati wa chumba cha uzazi na wodi maalum ya uangalizi wa kina mama mara tu baada ya kujifungua wilayani Kilwa ni Meneja Uwajibikaji kwa jamii kutoka Kampuni ya PanAfrican Energy Andrew Kangashaki(wa pili kushoto) pamoja na Mkurugenzi wa Wilaya ya Kilwa Twalib Mbasha (wa pili kulia) wanaowashuhudiwa ni Mwanasheria wa Wilaya ya Kilwa Mh. Godfrey Makary ( kulia), Mkuu wa Wilaya ya hiyo Juma Abdalah Njwayo (kushoto) jana katika hafla fupi iliyofanyika jana katika hospitali ya Kinyonga Kilwa Kivinje.

Wanahabari wakihakikisha wanapata habari sahihi kutoka kwa wahusika.

Wauguzi wa Hospitali ya Kinyonga Kilwa Kivinje wakishuhudia makabidhiano ya mkataba wa miradi ya ujenzi wa mama ngojea ‘maternity waiting home’ utakaofanyika katika hospitali yao na mradi mwingine wa ukarabati wa wodi ya uzazi utakaofanyika katika kituo cha afya cha Kilwa Masoko. Hafla hiyo ilifanyika hospitalini hapo jana.PICHA NA MICHUZI  JR-MICHUZI MEDIA GROUP.

=========  =======  ======   ==========
PANAFRICAN ENERGY KUTOA TSH .335,142,142 KUFADHILI UJENZI WA WODI ZA AKINA MAMA WAJAWAZITO WANAOSUBIRI KUJIFUNGUA ‘MAMA NGONJEA’ YAANI MATERNITY WAITIING HOME, HOSPITALI YA  WILAYA ,KINYONGA KILWA KIVINJE NA KUKARABATI WODI ZA UZAZI NA CHUMBA MAALUM CHA UANGALIZI WA AKINA MAMA MARA TU BAADA YA KUJIFUNGUA KITUO CHA AFYA CHA KILWA MASOKO.

Wakazi wa Kilwa wana haki ya kuendelea na kuwa na matumani baada ya kushuhudia makubaliano ya miradi mingine mikubwa  katika eneo lao kati ya Kampuni ya PanAfrican Energy na Wilaya ya Kilwa. Moja ya miradi hiyo ni ujenzi wa wodi ya kupumnzikia wakina mama wakisubiri kujifungua katika Hospitali ya Kinyonga iliyopo Kilwa Kivinje, na mradi mwingine ni ujenzi wa wodi ya wazazi na chumba maalum cha uangalizi wa akina mama mara baada ya kujifungua katika Kituo cha afya cha Kilwa Masoko. 

Katika hospitali ya wilaya , PANAfrican Energy watafadhili ujenzi wa wodi ya kusubiria akina mama, yaani mama ngonjea (maternity waiting home,) ambayo ni sehemu wanaposubiri  akina mama ambao wanaweza kuwa kwenye uzazi hatarishi.  Hii ni njia  kuu ya kuondoa tatizo la umbali mrefu kama kikwazo cha akina mama kujifungua salama ambapo hivi sasa wakina mama hushindwa kufika mapema hospitalini kutokana na kutokuwa na chumba maalum kwa ajili ya kusubiria huduma ya kujifungua. 

Kuwepo kwa wodi ya kupumnzikia akina mama hawa hapa Kinyonga ni manufaa tosha ukiangalia hali halisi ya mazingira na miundombinu ya Kilwa.  Pamoja na  na kupunguza vifo vya akina mama wajawazito kwani watakuwa karibu na hospitali, pia itapunguza gharama  kwani mama huyu anaweza kuchukua usafiri wa kawaida na kwa utaratibu wake na kwenda kusubiria.

Miradi hii miwili inaunga  mkono jitihada za serikali za kuboresha huduma za afya nchini na imekuja muda muafaka ambapo serikali inachukua hatua kupunguza na kutokomeza kabisa vifo vya akina mama wajawazito na matatizo yanayotokana na ujauzito.  Kutokana na utafiti uliofanywa mwaka 2009/10 nchini inaonesha kuwa wanawake 454 hufariki kwa kila 100,000, kila mwaka kutokana na matatizo yanayotokana na ujauzito.

 Vifo vya akina mama wajawazito vinatokana na  kutokwa damu nyingi wakati na baada ya kujifungua, utoaji mimba usio salama, shinikizo la damu, na kukosa uchungu wa kutosha au kukosa kabisa wakati muda wa kujifugua umefika .Uwepo mdogo wa sehemu za dharura na huduma kwa mtoto aliyezaliwa, ukosefu mkubwa wa watoa huduma za afya wenye ujuzi pamoja na mfumo duni wa rufaa, yote haya yanachangia kwa kiasi kikubwa vifo vya kina mama wajawazito.

Akiongea katika hafla ya kusaini makubaliano ya miradi hiyo leo kwa niaba ya Kampuni ya PanAfrican Energy, Meneja Uwajibikaji kwa jamii wa Kampuni ya PanAfrican Energy Bwana Andrew Kangashaki alisema, “Idadi ya vifo vya kina mama wajawazito imekua kubwa ya kutisha na tunataka kuwahakikishia wakazi wa kilwa kwamba ni kupitia miradi kama hii  mabpo tunaweza kuwa sehemu ya kumaliza tatizo hili kwa pamoja.

 Leo tena tunasaini makubaliano mengine na wilaya ya kilwa katika masuala ya afya; Tutafadhili miradi hii miwili yenye gharama ya Tshs 335,142,142. Moja ni nyumba ya kupumzikia kina mama wajawazito wanaosubiri kujifungua katika hospitali ya Kinyonga, Kilwa,  ambayo itagharimu Tsh 220,292,430.00 huku wodi za wazazi katika kituo cha afya cha kilwa masoko kitagharimu Tsh 114,849,636.00. 

Huu ni muendelezo wa kusapoti Nyanja za afya katika wilaya ya kilwa.  Mwanzoni mwa mwaka huu kampuni ya PanAfrican Energy ilikamilisha ujenzi wa nyumba za wauguzi  wa kituo cha affya cha Nangurukuru, ambacho hapo awali walikikarabati.  Nyumba za wauguzi zilikabidhiwa mwezi Juni kwa mkuu wa wilaya ya Kilwa. 

“Lengo letu kuu ni kuchangia mafanikio ya kiuchumi na ya kijamii katika wilaya ambapo Kampuni inafanya kazi, kutambua na kuimarisha uhusiano usiotengeka kati ya ustawi wa biashara na ustawi wa jamii kwa kutimiza mahitaji yao. Tunawasikiliza wananchi wa Kilwa na kuyazingatia mahitaji yao kwa umaakini. “aliongeza, Bw.Andrew.


Naye Mkurugenzi wa wilaya ya kilwa Bw.Twalib Mbasha aliishukuru Kampuni ya PanAfrican Energy kwa jitihada kubwa wanazoendelea kuzifanya katika kuwawezesha wakazi wa kilwa. “Mmetuhakikishia kuwa mpo nasi, nyie ni washirika tunaweza kuwategemea katika Nyanja zinazogusa na kuhusu maisha yetu. 

Tunapenda kuwahakikishia kuwa tutakuwa pamoja katika kukamilisha miradi hii kuanzia mwanzo mpaka mwisho.” Alisema.  Pamoja na wauguzi na wafanyakazi wa sekta ya afya wilaya ya Kilwa, pia walioshuhudia usainishaji wa makubaliano hayo ni Mkuu wa wilaya ya Kilwa, Mhe. Juma Njwayo pamoja na wabunge wa Kilwa Mh.Vedasto Edgar Ngombale and Selemani Bungawa.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »