Polisi: Wagombea Urais marufuku kuambatana na wapambe.

August 13, 2015


Kaniki
Na Lorietha Laurence –Maelezo
Jeshi la Polisi nchini limesitisha maandamano ya wafuasi wa vyama vya siasa wakati wa kuchukua ,kutafuta  wadhamini, na kurejesha fomu za kugombea nafasi ya Urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Naibu Inspekta Jenerali wa jeshi la Polisi Abdulrahman  Kaniki amesema kuwa jeshi limechukua hatua hiyo kutokana na ukiaukwaji wa sheria za usalama barabarani uliojitokeza wakati wagombea wa vyama vya CHADEMA na CCM walipochukua fomu za kugombea Urais makao makuu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
 “Kwa sababu za kiusalama   Jeshi la Polisi linasitisha maandamano ya aina yoyote wakati wote wa zoezi la kuchukua fomu, kutafuta wadhamini  mikoani pamoja na zoezi la kurejesha fomu “ alisema Kaniki.
Aidha aliongeza kuwa jeshi la Polisi nchini linafanya utaratibu wa kuwakutanisha wadau wote wa siasa ikiwemo viongozi wa vyama vya siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi Mkuu ili kuona namna bora ya kufanya uchaguzi katika hali ya amani na utulivu.
“Jeshi la Polisi halitasita kumchukulia hatua za kisheria mgombea, kiongozi, mfuasi au chama chochote cha siasa kitakachokiuka agizo hili,” alisema.
Hatua hiyo ya jeshi la Polisi nchini inatokana na baadhi ya wagombea wa nafasi za Urais kufuatana na kundi kubwa la wanachama, na wapambe wao wakati wa kuchukua fomu za kuomba kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi hivi karibuni na kuatarisha usalama ikiwemo kufungwa kwa barabara na kusababisha baadhi ya shughuli za kijamii kusimama.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »