Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa
Taifa wa Bima ya Afya Bwana Michael Mhando na Mkuu wa Huduma za Matibabu
Jeshini Brigedia Denis Raphale Janga wakitia saini mkataba wa
ushirikiano ambapo Mfuko utatumia vituo vya matibabu vya Jeshi kutibu
wanachama wake.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa
Taifa wa Bima ya Afya Bwana Michael Mhando na Mkuu wa Huduma za Matibabu
Jeshini Brigedia Denis Raphale Janga wakikabidhiana mkataba.
………………………………………………………….
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
(NHIF) umeingia mkataba na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ambapo
wanachama wa mfuko huo na wategemezi wao watapata huduma za matibabu
katika hospitali za jeshi nchini kote.
Mkataba huo wa miaka mitatu uliosainiwa jana unalenga kupanua
wigo wa vituo vya matibabu na kuanzisha ushirikiano wa kihistoria baina
ya pande mbili hizo.
Akizungumza wakati wa kutia saini mkataba huo Mkuu wa Huduma za
Afya Jeshini Brigedia Denis Raphael Janga, amesema amepokea kwa furaha
mkataba huo kwa kuwa utawapa nafasi ya kutoa huduma bora kwa kundi kubwa
la wanachama wa NHIF ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikosa huduma
katika vituo vya jeshi vilivyo karibu nao.
Ameahidi kushirikiana kwa karibu na uongozi wa NHIF ili
kuhakikisha wanachama na wategemezi wao wanapata vipimo na dawa wakati
wote watakapokwenda kwenye vituo hivyo.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya
Bwana Michael Mhando amesema NHIF kwa muda mrefu fursa ya kufanya kazi
na JWTZ katika sekta ya matibabu na kwamba mkataba huo unafungua
historia mpya ya ushirikiano baina ya taaisi hizo wa kujenga nchi kwa
pamoja.
Amesema ili kuhakikisha kuwa mkataba huo unakuwa na manufaa kwa
pande zote mbili Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya utaandaa mafunzo maalumu
kwa watoa huduma wa vituo vya jeshi ili kuhakikisha kuwa kunakuwa na
uelewa wa pamoja wa namna ya kuhudumia wanachana wa NHIF watakaokwenda
kupata huduma katika vituo hivyo.
Mhando ameongeza kuwa NHIF itaendelea kushirikiana na uongozi wa
JWTZ ili kukamilisha taratibu za kiutawala zitakazowawezesha wanaejeshi
na familia zao kujiunga na kunufaika na matibabu kupitia Mfuko wa Taifa
wa Bima ya Afya.
Aidha ameushauri uongozi wa JWTZ kutumia fursa ya mikopo ya
vifaa tiba, ukarabati na dawa na vitendanishi inayotolewa na Mfuko wa
Taifa wa Bima ya Afya ili kuhakikisha kuwa vituo vya matibabu
vinavyomilikiwa na JWZT vinakuwa na mazingira mazuri na vitendea kazi
vinavyotakiwa.
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lina vituo vya matibabu vya ngazi mbalimbali zaidi ya kumi na nane nchini kote.