March 09, 2014

TANZANIA YAENDELEA KUWA KINARA WA UWATAWALA BORA

Katibu Mtendaji wa Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) Tanzania Rehema Twalib (wa kwanza kushoto) akiongea na waandishi wa habari leo jijijni Dar es salaam ambapo Tanzania inaungana na nchi nyingine za Afrika wanachama wa mpango huo kuadhimisha siku APRM na kutoa  taarifa ya tathmini ya utawala bora nchini. Katikati ni Afisa Habari Idara ya Habari MAELEZO Frank Mvungi na wa kwanza kulia ni Mratibu wa APRM Tanzania Dkt. Cuthbert Ngalepeka.
Baadhi ya waandishi wa habari wakitekeleza majukumu yao leo jijini Dar es salaam ambapo Tanzania inaungana na nchi nyingine za Afrika wanachama wa Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM) katika kuadhimisha siku ya APRM na kutoa  taarifa ya tathmini ya utawala bora nchini. Picha zote na Eleuteri Mangi -MAELEZO
**************************************
Na Frank Mvungi-MAELEZO
MPANGO wa Afrika wa kujitathmini kiutawala bora (APRM) umebainisha kuwa Tanzania ni moja ya Nchi zinazofanya vizuri katika  utawala bora.

Hayo yamesemwa na Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania Rehema Twalib wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam alipokuwa akieleza mafanikio yaliyofikiwa hadi sasa ikiwa ni sehehmu ya maadhimisho ya siku mchako huo ambayo huadhimishwa Machi 9 kila mwaka.

Bi Rehema alibainisha kuwa Tanzania imepata mafanikio katika Nyanja za Demokrasia na Utawala Bora, Siasa, Usimamizi wa uchumi, uendeshaji wa makampuni,Maendeleo ya uchumi-Jamii na Masuala mtambuka kama afya.

Akifafanua zaidi Bi. Rehema alisema Tanzania kupitia APRM imefanya tathmini yake katika maeneo hayo na kuwasilisha ripoti yake mbele ya wakuu wa nchi wanachama na kujadiliwa.

Wakati huo huo alizitaja hatua zinazochukuliwa na Serikali kuwa ni kuanza kufanyia kazi mpango kazi wa kitaifa (NPoA) wa kuondoa changamoto zilizobainishwa katika ripoti ya APRM kuhusu hali ya utawala bora nchini. 

  Pia Bi Rehema alizitaja hatua nyingine ambazo Tanzania imefikia katikakutekeleza  mchakato wa APRM kuwa ni kuwashirikisha wananchi kutoa maoni yao kuhusu hali ya utawala bora nchini na Serikali kuruhusu wataalamu wa utawala bora kutoka nchi wanachama kuja nchini kuhakiki mchakato huo.

Aidha, Bi Rehema alibainisha kuwa lengo kuu la mpango huu ni kuwashirikisha wananchi ili kushirikiana na Serikali zao kubaini changamoto za utawala bora ili zifanyiwe kazi na kuhimiza nchi kutekeleza viwango vinavyokubalika kimataifa na kikanda.

APRM ni mpango ulioasisiwa machi 9, 2013 na wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (AU) ambapo Tanzania kwa sasa ni miongoni mwa nchi 34 kati ya 54 za AU zilizokwisha jiunga na mpango huu ambapo ilijiunga mwaka 2004.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »