Afya ya Maranda sasa yatetereka, alazwa Moi

March 04, 2014
Dar es Salaam. Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rajabu Maranda, anayetumikia kifungo cha miaka 18 gerezani kwa wizi wa fedha katika Akaunti ya Madeni ya Nje (Epa) katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), amelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili akisumbuliwa na tatizo la mgongo.
Msemaji wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu (MOI), Jumaa Almasi aliliambia gazeti hili jana kuwa Maranda alifikishwa hospitalini hapo Februari 16, mwaka huu.
“Ni kweli Maranda yupo hapa tangu Februari 16 na alifanyiwa upasuaji kutokana na matatizo ya mgongo wiki tatu zilizopita na hali yake inaendelea vizuri ingawa hawezi kuamka kitandani,” alisema Almasi.
Kuhusu ugonjwa unaomsumbua, Almasi alisema: “Ugonjwa ni siri kati ya mgonjwa na daktari wake na binafsi siwezi kuuelezea ila kama nilivyosema alifanyiwa upasuaji wiki tatu zilizopita.”
Alisema Maranda yuko chini ya uangalizi wa askari Magereza kutokana na kuendelea kutumikia adhabu ya kifungo gerezani.
Maranda aliyewahi kuwa Mweka Hazina wa CCM mkoani Kigoma na binamu yake, Farijala Hussein, ambao kwa pamoja walipatikana na makosa sita kati ya saba waliyokuwa wanakabiliwa nayo ya kujipatia Sh2.2 bilioni za Epa.
Maranda na wenzake pia wanatumikia kifungo cha miaka mitatu jela ambayo itakwenda sanjari na kifungo cha awali cha miaka mitano kutokana na kifungo cha miaka mitatu kwa kila kosa, ambayo ni kula njama, kughushi nyaraka, kuwasilisha hati bandia na kujipatia kiasi hicho cha fedha.
Novemba 2012, Maranda kwa mara ya tatu alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela na kuamriwa kurejesha Sh616.4 milioni.
chanzo:mwananchi

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »