SERIKALI YASIKIA KILIO CHA MBUNGE MPINA UKOSEFU WA HUDUMA KWENYE ZAHANATI JIMBO LA KISESA

June 27, 2022

 
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Innocent Bashungwa



WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais- TAMISEMI, Innocent Bashungwa amesikia kilio cha Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina aliyehoji sababu ya Serikali kutozifungua Zahanati 10 zilizojengwa na kukamilika kwa miaka mingi sasa huku wananchi wa vijiji hivyo wakilazimika kutembea umbali mrefu kutafuta huduma.

Akichangia bajeti ya Wizara ya Afya bungeni Dodoma Mei,2022, Mpina alisema upungufu wa watumishi wa kada ya Afya ngazi ya Zahanati ni tatizo ambalo halijapata suluhu kwa muda mrefu na wananchi wakiendelea kukosa huduma hitajika katika vijiji vingi vya Jimbo la Kisesa.

Mpina alisema Serikali ilipaswa kuweka utaratibu mzuri wa ajira na kutumia njia mbadala ya kuingia 4 mkataba na vijana waliohitimu mafunzo mbalimbali ya Afya ambao hawaja ajiriwa ili kusaidia utoaji wa huduma kwa wananchi.

“Mheshimiwa Spika, Kwenye Jimbo langu la Kisesa nina Zahanati 10 zilizokamilika muda mrefu lakini huduma hazitolewi, Mfano Zahanati ya Kijiji cha Semu, Mwandu Kisesa, Makomangwa, Mwageni, Mwagayi, Isangijo, Ikigijo, Mwakisandu, Malwilo na Tindabuligi, lakini pia tuna maboma ya muda mrefu 10 ya Kijiji cha Inonelwa, Mwamhongo, Nzanza, Matale, Masanga, Mwakipugila, Ntobo, Ng’hanga, Mwakasumbi na Lubiga” alisema Mpina.

Hata hivyo kwa mujibu wa orodha ya majina ya watumishi wapya wa sekta ya Afya iliyotangazwa na Waziri Bashungwa Juni 26, 2022 kwa Jimbo la Kisesa zitafunguliwa Zanahati 6 kati ya 10 zilizokamilika ujenzi wake.

Waziri Bashungwa amezitaja Zahanati hizo mpya zilitakazofunguliwa rasmi kwa Jimbo la Kisesa na idadi ya watumishi wapya kwenye mabano kuwa ni Zahanati ya Kijiji cha Isangijo Kata ya Lubiga (3), Zahanati ya Kijiji cha Makomangwa Kata ya Mwandoya (3), Zahanati ya Kijiji cha Mwagayi Kata ya Itinje (3).

Pia Waziri Bashungwa amezitaja zahanati nyingine zitakazofunguliwa Jimbo la Kisesa kuwa ni Zahanati ya Mwageni Kata ya Isengwa (3), Zahanati ya Kijiji cha Mwasungura Mwageni B (2), Zahanati ya Kijiji cha Malwilo Mnadani Kata ya Tindabuligi (3), Zahanati ya Mwandu Kisesa Kata ya Kisesa (3).

Waziri Bashungwa amewataja watumishi hao na majina ya vituo vyao kwenye mabano kuwa kuwa ni Teodora Kalistus Chodota Muuguzi Daraja la II, Ayubu Gladwell Mwaibosi Muuguzi Daraja la II na Ramadhani Shabani Mrutu, Tabibu Daraja la II (Co) (Zahanati ya Isangijo).

Wengine ni Joseph Rashid Ghake, Muuguzi Daraja la II, Edomu Anania Mwakingwe, Muuguzi Daraja La II, Frank John Mandala Tabibu Daraja la II (Zahanati ya Makomangwa).

Bashungwa amewataja wengine kuwa ni Nuru Daud Mwala , Muuguzi Daraja la II na Ernest Joseph Kachwele, Muuguzi Daraja la II (Zahanati ya Malwilo). Wengine ni Samwel Gelewa Simon, Muuguzi Daraja la II, Maryam Baraka Omar Female, Tabibu Daraja la II (CO) na Yohana Magori Magori, Muuguzi Daraja la II (Zahanati ya Mwagayi).

Wengine ni Azizi Poul Mgoboleni, Tabibu Daraja La II (Co), Johnson Joseph Kayombo, Muuguzi Daraja la II na Damian Emanuel Lyimo, Muuguzi Daraja la II (Zahanati ya Mwageni). Bertha Juvenary Nyamwiula, Muuguzi Daraja la II na Nkeshimana Jumanne Kasonga, Muuguzi Daraja la II (Zahanati ya Mwageni B- Mwasungura).

Wengine ni Kissile Nelson Mwakabago, Muuguzi Daraja la II, Eufransia Zacharia Mjuanga, Muuguzi Daraja la II na Ezekiel Christopher Mantyotyo, Tabibu Daraja la II (Co) (Zahanati ya Mwalilo Mnadani). Watumishi wengine ni Thereza Revocatus Lweyemaho, Muuguzi Daraja la II, Kasilda Gervas Nkembo, Tabibu Daraja la II (CO) (Zahanati ya Mwandu Kisesa).

RAIS SAMIA AZINDUA MIF,AIPONGEZA KWA KAZI NZURI KWA WATOTO WA KIKE

June 19, 2022

 


 Na John Mapepele



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Samia Suluhu Hassan leo Juni 19, 2022 amezindua taasisi ya Mwanamke Initiative Foundation (MIF) iliyopo Zanzibar inayojishughulisha na kumkwamua mtoto wa kike katika elimu ili kutimiza ndoto zake yenye kauli  mbiu inayosema “lea mwana tung’are”.


 Kabla ya kuzindua taasisi hiyo, Mhe. Rais Samia ameupongeza uongozi wa MIF kwa mkakati kabambe wa taasisi hiyo wa kuleta chachu ya kuunganisha Serikali na MIF na taasisi nyingine katika kumkomboa mtoto wa kike kielimu huku akielekeza serikali inavyofanya maboresho izingatie masuala ya mitaala,ukaguzi wa elimu,utungaji wa mitihani na sifa za walimu.   


Aidha, Mhe. Rais ametoa wito kwa wadau mbalimbali nchini kuunga mkono jitihada zinazofanywa na MIF huku akisisitiza kuwa suala la kuwakomboa Watoto wa kike ni suala la kila mtu. “Hilo ni jukumu letu sote, tunatakiwa wote tushirikiane.” Ameongeza Mhe. Rais


Amezielekeza Wizara zinahusika na elimu kwa pande zote mbili za muungano kuhakikisha zinashirikiana ili kuhakikisha kuwa watoto wote wakiume na wakike wanatimiza  ndoto zao kwa faida ya taifa zima.Kwa upande wake, Mwenyekiti na Mwanzilishi wa Mfuko huo, Mhe. Wanu Hafidh Ameir ambaye pia ni Mbunge wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar amemshukuru Rais kwa kuja kuzindua taasisi  hiyo  huku akielezea kuwa  kwa kuja kuzindua  amewapa heshima  kubwa wadau wote wa elimu nchini.


Amesema MIF inatambua kuwa kumekuwa na  changamoto katika jamii inayowazunguka  lakini wao wameamua kujikita katika elimu hususan  kubadili  mtazamo na fikra ya kuwa mtoto wa kike hana uwezo na badala yake ni kumkomboa ili hatimaye ayaishi malengo na ndoto za maisha yake huku akiiomba jamii iwaunge mkono.


Amewashukuru wadau mbalimbali waliojitokeza ambapo amewaomba kuendelea  kuchangia ili kuwasaidia watoto wa kike  waweze kutimiza ndoto zao.


 Afisa Mtendaji Mkuu wa MIF, Fatuma Mwasa ameyaelezea malengo makubwa ya taasisi hiyo  kuwa ni pamoja na kusaidia jamii huru iliyo na maendeleo isiyosumbuliwa na  ujinga, umasikini na maradhi kwa kumwinua mtoto wa kike kielimu, kuwawezesha vijana kiuchumi, kuongeza uelewa katika afya ya akili na kushughulika  na afya ya uzazi, afya ya mama na mtoto. 


Ameitaja baadhi ya mipango inayofanywa na MIF kuwa ni pamoja na kujenga kituo cha  cha kisasa cha mafunzo maalum kama vile ushonaji, umeme kinatakachogharimu takriban  bilioni 15 kwa ufadhili wa nchi za Falme za Kiarabu.


Pia kuendelea kuongeza mafunzo kwa walimu wa shule za msingi na kuwachukua wanafunzi ambao hawajafanikiwa kwenye masomo na kuwa vhyuo  vya ufundi ambapo amesisitiza kuwa wamekuwa wakifanya vizuri. 


Ameongeza kuwa MIF inafundisha kilimo cha mbogamboga  lengo ni kutaka kurudisha fedha  mapema, pia inajenga vyoo katika shule, kutoa ufadhili wa kusomesha  nje ya nchi wanafunzi wanaofaulu vizuri na kuwatafutia, masoko na mitaji. 


Katika uzinduzi huo mawaziri anayesimamia elimu, Profesa Adolf Mkenda, anayesimamia Michezo. Mhe. Mohamed Mchengerwa na anayesimamia Utumishi, Mhe. Jenista Mhagama wameungana na mawaziri kutoka  SMZ kushiriki uzinduzi huo.

WADAU WAPONGEZA MIF KWA KUSAIDIA MTOTO WA KIKE ZANZIBAR, WAJITOKEZA KUCHANGIA

June 18, 2022

 


Na John Mapepele. 

Wadau mbalimbali wa kupigania maendeleo ya mtoto wa kike nchini wamejitokeza  kuchangia takribani  shilingi  bilioni moja  kwenye  taasisi ya Mwanamke Initiative Foundation (MIF) iliyopo Zanzibar inayojishughulisha na kumkwamua mtoto wa kike katika elimu ili kutimiza ndoto zake. 

 Wadau hao wametoa michango  hiyo katika  halfa maalum ya chakula cha usiku iliyoandaliwa na taasisi ya (MIF) usiku wa kuamkia leo Juni 19, 2022 Zanzibar  kutokana na kazi kubwa na nzuri inayofanywa na mfuko huo  katika suala zima la  kuwasaidia Watoto wa kike kufikia malengo  yao hivyo kuendesha maisha yao.


Mwenyekiti na Mwanzilishi wa Mfuko huo, Mhe. Wanu Hafidh Ameir ambaye pia ni Mbunge wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na mtetezi wa haki  za vijana na wanawake amewashukuru wadau mbalimbali waliojitokeza ambapo amewaomba kuendelea  kuchangia ili kuwasaidia Watoto wa kike  waweze kutimiza ndoto zao.


 “Naomba kuchukua  fursa hii kushukuru sana isiwe mwanzo wala mwisho naomba iwe mwanzo na tuendelee kuchangia  mfuko wetu wa Mwanamke Initiative ili kuona kwamba mtoto wa kike anasimama  na anaweza kushindana katika ulimwengu” amefafanua,  Mhe Wanu.


Wakitoa maoni yao kwa nyakati tofauti tofauti kuhusu kuanzishwa kwa mfuko huo, wamepongeza jitihada kubwa zinazofanywa na MIF kwa kuwasaidia watoto wa kike Zanzibar huku wakitoa rai kwa wadau wengi zaidi  kushiriki kwenye jitihada hizo za kuwakomboa Watoto wa kike kwa kuchangia kwa hali na mali katika mfuko huo ili lengo liweze kutimia. 


“Tumefarijika sana na kazi kubwa na nzuri zinazofanywa na mfuko huu, tunaomba na wadau wengine waendelee kujitokeza kuchangia kwa  kuwa ukimsaidia mtoto wa kike aweze kujikwamua umesaidia taifa”aliongeza Tuli Mwambapa ambaye ni Mkurugenzi wa Benki ya CRDB nchini.

Benki ya CRDB imechangia shilingi milioni mia tatu ambapo wadau wengine pia waliweza kuchangia kwenye hafla hiyo.

Katika hafla hiyo mbali na wageni mbalimbali waliohudhuria   pia Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Omary Mchengerwa ambaye ni mume wa Wanu alishiriki.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Samia Suluhu Hassan. leo,  Juni 19, 2022 anatarajiwa kuuzindua rasmi mfuko huo.

WAZIRI MCHENGERWA AIPONGEZA TIMU YA KRIKETI KUTWAA UBINGWA RWANDA, AMSHUKURU RAIS SAMIA

June 18, 2022

 

 

Na John Mapepele


Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa ametoa pongezi kwa  Timu ya Tanzania ya  Wanawake ya Kriketi kwa  kutwaa Ubingwa leo Juni 18, 2022 kwenye mashindano ya Kwibuka Cup nchini Rwanda, yaliyoshirikisha nchi nane ( Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Botswana , Nigeria, Brazil na Ujerumani) bila kufungwa na timu yoyote. 

Aidha, amempongeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake mkubwa anaoutoa katika michezo.

Amesema hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha michezo kwa kuweka mikakati  kabambe chini ya uongozi wa Samia imeleta matokeo chanya kwenye sekta za michezo na sanaa hapa nchini.

Amesema taarifa ya hali ya uchumi wa nchi iliyosomwa bungeni hivi karibuni imeonesha kuwa sanaa na burudani zimechangia kwa asilimia 19.4 katika kipindi cha mwaka 2021 na kuziacha kwa  mbali sekta mbalimbali.

Amesema dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuifanya michezo kuwa uchumi badala mazoe ya kuifanya michezo kama  kitu cha burudani pekee.

Aidha, amesema Serikali tayari inazigharimia timu zote za taifa zinazojiandaa kwa ajili ya mashindano ya kimataifa kwa kuziweka kambini kuanzia mwanzo wa mwaka huu.

Hivi karibuni Mhe. Mchengerwa amekaririwa vyombo vya habari akisisitiza kuwa michezo na sanaa ni uchumi  hivyo wanamichezo na wasanii wanapaswa kutambua kuwa vipaji walivyonavyo ni mtaji wa maisha yao.

Ujumbe wa Klabu ya Southampton uliokutana na Mhe. Waziri Mchengerwa na kufanya mazungumzo ya kuinua michezo ulioongozwa na Mkuu wa Idara ya Biashara ya klabu hiyo David Thomas pia ulimpongeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya kwenye michezo na kumzawadia jezi ambayo ilipokelewa kwa niaba yake na Mhe. Mchengerwa.

UWEKEZAJI MKUBWA KUFANYWA NA SERIKALI KATIKA SEKTA YA KILIMO CHA UMWAGILIAJI– MNDOLWA

June 18, 2022

 

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Raymond Mndolwa akiongea na waandishi wa Habari baada ya mkutano na watumishi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na wahandisi wa Umwagiliaji wa Mikoa, uliofanyika Jijini Dodoma mapema leo.

Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Raymond Mndolwa na Baadhi ya watumishi wa Tume hiyo pamoja na wahandisi wa Umwagiliaji wa mikoa



Baadhi ya watumishi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji wakifuatilia kikao kilichofanyika jijini Dodoma mapema leo.






Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw, Raymond Mndolwa amesema, kutakuwa na kilimo cha umwagiliaji cha uhakika kutokana na uwekezaji mkubwa wakihistoria unaofanywa na serikali ya awamu ya sita katika sekta ya kilimo cha umwagiliaji.

Bw,Mndolwa ameyasema hayo mbele ya Waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari jijini Dodoma mara baada ya kufungua kikao kazi kilichowahusisha watumishi wote wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na kuongeza kuwa, kutokana na majukumu makubwa iliyopewa na serikali Tume ya Taifa ya Umwagiliaji “niliona ni muhimu sana tukutane watumishi wote ili tujipange,tuweze kutekeleza majukumu hayo”.

“Tume tuna juku la kuwasaidia wakulima waweze kulima kutokana na kilimo wanacholima ili waweze kupata maji katika mazao wanayolima hili ni sehemu ya majukumu yetu, kutokana na hali yakuwa na upungufu wa mvua serikali imeweka msisitizo mkubwa katika kilimo cha umwagiliaji kwa matarajio yajayo”.

Tunataka Wananchi na Wakulima waliokata tamaa ya kulima warudi shambani, kwasababu tume ya Taifa ya Umwagiliaji imewezeshwa na inakuja kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo cha Umwagiliaji.

Akizungumzia suala la Bajeti kubwa iliyoelekezwa na Serikali ya awamu ya sita katika Sekta ya Kilimo cha Umwagiliaji, Mkurugenzi Mndolwa ameongeza kusema kuwa, Tume imeelekeza nguvu katika miradi iliyokwisha buniwa na miradi hiyo ndiyo ya kipaumbele, baada ya miradi hiyo ya mwaka huu hatua itakayofuata ni kujenga miradi mingine ya umwagiliaji nchini katika maana ya mikoa yote itakayotekeleza kilimo cha umwagiliaji na aina gani ya miradi ifanyike katika kuhakikisha kila Mkoa na Wilaya inapata miradi ya Kilimo cha Umwagiliaji.

Alisema wana panga upya kuhakikisha kwamba mwaka wa fedha unaofuata yaani 23/24 watakuwa na mkakati ambao utaenea nchinzima.

Mwaka wa fedha huu 22/23 watarekebisha Skimu thelathini (30) za kilimo cha umwagiliaji lakini Wahandisi wa umwagiliaji wa mikoa watafanya mapitio ya miradi iliyokwisha kwa lengo la maboresho kulinga na na bajeti yetu.

“Nina ahidi kwamba maboresho yatakuwa makubwa ili kila mwananchi anayetaka kulima aweze kulima.”Alisisita Kikao cha leo ni majumuisho ya siku yapili ya kikao kilichohusisha watumishiwa Tume Makao makuu na Wahandisi wa Umwagiliaji wa mikoa kilichojadili, Mpango mkakati wa miaka mitano wa utekelezaji wa shughuli zaTume.

TANZANIA NA INDIA KUJA NA MAPINDUZI MAKUBWA KWENYE UTAMADUNI

June 17, 2022

 


Na John Mapepele.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema  kuwa Tanzania na India zinakwenda kupitia na kuboresha mikataba ya mashirikiano ya awali  kwenye eneo la Utamaduni na Sanaa iliyojiwekea  mwaka 1984 ili  kuiboresha iweze kuleta mapinduzi makubwa na ya haraka kwa faida ya pande zote.

Mhe, Mchengerwa ameyasema haya leo Juni 17, 2022 akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk. Hassan Abbasi wakati alipotembelewa ofisini kwake na Balozi wa India nchini Mhe.  Binaya Srikanta Pradhan na kufanya mazungumzo ya kuendeleza mashirikiano kwenye sekta hizo.

Aidha, amesema mambo mengi yalikubalika   baina ya nchi zote mbili hususan  kuendelea kwa tamaduni  pia  kumekuwa na mambo mengi ambayo yameandikwa ambayo kuna haja ya kufanya mapitio.


Ameongeza  kuwa katika maongezi hao  wamekubaliana kuwa  na kituo maalum cha kuandaa filamu ambacho kitatumika kwa nchi za Afrika mashariki ambapo  baadhi ya wasanii kutoka India  watashiriki moja kwa moja kwenye eneo hili.


Pia amesema eneo jingine  kubwa ambalo wamejadili  ni kuhusu umuhimu wa  wa kufanya mkutano mkubwa kuhusu bahari ya Hindi ambao utajumuisha nchi hizo  mbili.

Amesema tamasha hilo litasaidia kuonyesha historia za nchi zote zilikotoka zilipo na zinakoelekea

Aidha, amesema  bahari ya Hindi imebeba historia kubwa ambayo tayari watafiti kutokana  India na Tanzania wamefanya utafiti hivyo ni muhimu  kuutumia utafiti huo kwa faida ya nchi zote.

Naye  Mtaalam  na Mtafiti  Arindam Mukherjee ambaye ameambatana  na Mhe. Balozi amefafanua kuwa tafiti zinaonesha kuwa  Bahari ya Hindi ilikuws ikitumika kwa miaka mingi kufanya biashara  ambapo yapo baadhi ya maeneo ambayo yamethibitika yamekuwa yakikaliwa na waswahili na pia kumekuwa na mfanano wa maneno ya kiswahili.

SOUTHAMPTON KUWANOA MAKOCHA WA TANZANIA -WAZIRI MCHENGERWA

June 17, 2022

Na John Mapepele.


Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema  Tanzania inakwenda  kushirikiana na klabu ya Soka ya Southampton  kuwandaa makocha wa soka ili wawe kwenye kiwango cha kimataifa.

Mhe. Mchengerwa amesema haya leo juni 17, 2022 ofisini kwake akiambatana na Katibu Mkuu wa Wizara yake, Dk. Hassan Abbasi wakati alipokutana na ujumbe wa Klabu hiyo ulioongozwa na Afisa Biashara  Mkuu wa Klabu hiyo David Thomas. 


Amesema dhamira ya Serikali ni kuona kuwa michezo mbalimbali inasimamiwa  kisayansi ili kuleta tija ikiwa ni pamoja na kuwa na makocha ambao watasaidia kufundisha  timu za micherzo ili kufuka kwenye kiwango cha kimataifa.


Katika kikao hicho  wamekubalina kuwa Timu ya soka  ya ya Wanawake chini ya Miaka 17 (Serengeti Girls)  itakwenda kupatiwa mafunzo maalum   kwenye Klabu hiyo ikiwa ni maandalizi ya kwenda kwenye  mashindano ya kombe la dunia nchini India.

Katika tukio hilo ujumbe wa timu hiyo ulimzawadia jezi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe Samia Suluhu Hassan ikiwa ni kuthamini mchango wake mkubwa anaoutoa kuendeleza michezo nchini.

MNDOLWA AONGOZA MAPITIO YA MPANGO MKAKATI WA MIAKA MITANO WA TUME YA TAIFAYA UMWAGILIAJI

June 17, 2022

 

MkurugenziMkuu, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Raymond Mndolwa akifungua kikao kazi cha mapitio ya mpango mkakati wa miaka mitano wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Jijini Dodoma.

Mhandisi wa Umwagiliaji wa Mkoa wa Singida William Kadinda akielezea namna mpango mkakati utakavyorahisisha utekelezaji kiutendaji katika maeneo husika.


Baadhi ya Wataalam wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji wakijadiliana kwa lengo la kuboresha Mpango Mkakati wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.

Picha ya pamoja kati ya Menejimenti ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji na Wahandisi wa Umwagiliaji wa Mikoa.




Na; MwandishiWetu - Dodoma

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw. Raymond Mndolwa, ameongoza kikao kazi cha mapitio ya mpango mkakati wa miaka mitano wa Tume ya Taifa ya umwagiliaji, uliohusisha wataalam na wahandisi wa Umwagiliaji nchini, mapema leo Jijini Dodoma.

Bw. Mndolwa alisema kuwa,kuna umuhimu wakufanya mapitio ya mpango mkakati huo kwa pamoja tofauti kwa kuwa Mpango mkakati huo ni Dira ya Taasisi hivyo ni muhimu kila mtumishi katika taasisi anatakiwa kuifahamu kwani ndiyo zana inayotumika katika utekelezaji wa kazi za kila siku.

“Nimeona kuna Umuhimu wa kupitia kwa pamoja ili pale ambapo patakuwa na marekebisho turekebishe kwa pamoja, na kuwe na ushiriki kwa hoja katika kazi hii.” AlifafanuaMndolwa.

Kwa upande wake Mhandisi wa Umwagiliaji wa Mkoa wa Singida William Kadinda amesema, kikao kazi hiki kinatoa fursa ya mpango wa miaka mitano ambao unajumuisha shughuli zinazofanyika, pia kinaangalia maslahi ya watumishi katika upande wa mafunzo na kuona mahitaji yao, nakuweza kuwaongezea uwezo kiutendaji.

Kukamilika kwa mpango mkakati huo ni hatua muhimu kwa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji wakati huu,ikiwa na jukumu kubwa la ukarabati na ujenzi wa Skimu za umwagiliaji pamoja na Mabwawa kwa ajili ya umwagiliaji. Lengola serikalini kufikia Hekta 1,200,000 za umwagiliaji mwaka 2025.

KIONGOZI WA MABOHORA DUNIANI ATUA NCHINI KUFANYA ROYAL TOUR TANZANIA

June 16, 2022

 




 
 

 Na John Mapepele,
 
Kiongozi Mkuu wa madhehebu ya Kiislamu ya Mabohora (Dawoodi Bohoras); Sheikh Syedna Mufaddal Saifuddin, ametua nchini leo Alhamisi Juni 16, 2022, tayari kufanya ziara ya kiimani na mapumziko mafupi. 

Saydna Mufaddal, atakuwa nchini kwa takribani wiki mbili ambapo pamoja na shughuli za kiimani amekuja kuunga mkono azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuitangaza na kuifungua nchi hasa kupitia filamu ya Royal Tour.

“Akiwa nchini amekuja kuunga mkono malengo ya Royal Tour na yeye mwenyewe na wafuasi wake watakwenda mapumziko hapa nchini na msafara wake wote katika maeneo mbalimbali na pia iwapo taratibu zitakamilika na akaridhia anaweza kufanya mhadhara wake mkubwa wa kidini Julai hapa nchini ambapo wafuasi wake kati ya 30,000 hadi 40,000 kutoka sehemu mbalimbali duniani humfuata na tunajipanga ikitokea hivyo tutawaonesha watu hao na mabohora wengine duniani filamu ya Royal Tour,” alisema mmoja wa viongozi wa dhehebu hilo nchini Bw. Zainuldeen Adamjee. 

Akimpokea Kiongozi huyo, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema amewasilisha kwa kiongozi huyo salaam za Mhe Rais Samia ikiwemo utayari wa Tanzania kuwa mwenyeji wa mhadhara mkubwa wa mwaka wa kiongozi huyo utakaoleta maelfu ya watu hapa nchini.

“Hii ni sehemu ya muendelezo wa Royal Tour (post royal tour) ambapo Mhe Rais wetu amefanya kazi kubwa ya kuitangaza nchi yetu na sasa wawekezaji na watalii wakiwemo viongozi wa kimataifa wa kiimani na wa kijamii nao wanazidi kuja Tanzania. Kwa eneo letu sisi la utamaduni tumemhakikishia Sheikh kuwa Tanzania ni salama na aendelee kutuombea amani lakini pia alete wafuasi wake wengi zaidi kuja kutembelea na kuwekeza Tanzania,” alisema Waziri Mchengerwa.

Katika mapokezi hayo, Waziri Mchengerwa, aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi, ambaye pia anasimamia Kamati ya Rais iliyoratibu Royal Tour.

TUME YA TAIFA YA UMWAGILIAJI KUJENGA MABWAWA 14 NA HEKTA ELFU 10 ZA UMWAGILIAJI KWAAJILI YA UZALISHAJI WA MBEGU, SHILLINGI BILIONI 420 KUTUMIKA.

June 16, 2022


Mheshimiwa Hussein Bashe Waziri waKilimo akizungumza wakati akifungua semina ya siku mbili iliyowahusisha wadau wa Sekta ya Umwagiliaji mjini Morogoro

Mheshimiwa Hussein Bashe Waziri waKilimo akizungumza wakati akifungua semina ya siku mbili iliyowahusisha wadau wa Sekta ya Umwagiliaji mjini Morogoro


Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji,Bw, Raymond Mndolwa akizungumza wakati wa semina hiyo

Picha ya Pamoja ya Wajumbe mbalimbali walioudhuria Semina hiyo Walioketi. Katikati ni Waziri waKilimo Mheshimiwa Hussein Bashe.






NA MWANDISHI WETU,MOROGORO

Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Hussein Bashe, amesema kwa Mwaka wafedha ujao Wizara yake itatumia Shilingi Bilioni 420 katika ujenzi wa Miundo mbinu ya Skimu za umwagiliaji ikiwemo Hekta elfu kumi kwa ajili ya uzalishaji wa Mbegu ambapo wadau wa sekta binafsi watapewa kipaumbele kwa ajili ya kuzalisha Mbegu, ujenzi wa mabwawa 14 yatakayokuwa na miundombinu ya umwagiliaji kwa matumizi ya kilimo na mifugo.
 

Aliyasema hayo leo Mjini Morogoro wakati akifungua semina ya siku mbili iliyowahusisha wadau wa Sekta ya Umwagiliaji mjini Morogoro, Waziri Bashe ameendelea kusema kuwa utekelezaji wa kazi hiyo utakwenda sambamba na kuanzishwa kwa Ofisi za Umwagiliaji za Wilaya nchi nzima pamoja nakuajiri wasimamizi wa Skimu za umwagiliaji watakaohusika kusimamia zoezi la ukusanyaji wa ada na tozo za umwagiliaji kwa uhakika.

Eneo lingine la kipaumbele kwa Waziri Bashe ni pamoja na kuwasaidia Wakulima Wadogowadogo kupataTeknolojia bora za kilimo cha umwagiliaji kwa bei nafuu ili waweze kupata tija na kuchangia ongezeko la mavuno katika sekta ya umwagiliaji, zoezi hilo litawahusu pia Vijana wanaojishughulisha na kilimo cha umwagiliaji.

Kwaupande wake Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Bw,Raymond Mndolwa amewataka watumishi wote wa tume ya Taifa ya Umwagiliaji kufanya kazi kwa bidi na ubunifu ili kutimiza matarajio yaliyowekwa na serikali, akiamini taasisi yake inauwezo wakutekeleza majukumu yaliyopangwa na serikali kwa wakati, ufanisi na ubora unaotakiwa katika kuhudumia wananchi.

“ Nitamsapoti kila mtumishi aweze kutimi za wajibu wake, tumejipanga na lililopo mbele yetu tunaweza kulitekeleza”

Semina hiyo ya siku mbili imewashirikisha wadau mbalimbali ikiwemo sekta binafsi, Wakulima wadogo, Wataalam waBenki, Vyama vya Ushirika, Wahandisi na Maafisa kilimo wa Wilaya ikiangazia namna ya kuboresha maeneo matatu muhimu katika kilimo cha umwagiliaji ,uzalishaji, huduma za u mwagiliaji na njia bora yakukusanya Ada naTozozaUmwagiliaji.

 

MTUME BONIFACE MWAMPOSA AFIKA NYUMBANI KWA MBUNGE WA KISESA, LUHAGA MPINA KUHANI MSIBA MAMA YAKE NA KUMBUKUMBU YA MZEE MPINA

June 16, 2022

 

 

Mtume Boniface Mwamposa Bulldoza  akiendesha maombi maalum  kwa wazazi wa Mbunge wa Kisesa, Mhe. Luhaga Joelson Mpina, Marehemu Mpina Gabisi Samweli Luchemba na Marehemu Kephrine Kabula Masaga alipofika katika Kijiji cha Isangijo Wilaya ya Meatu Mkoa wa Simiyu Juni 15, 2022. Marehemu Mzee Mpina alifariki Juni 14, 2021 na Mama alifariki Juni 1, 2022.
Mtume Boniface Mwamposa Bulldoza akiendesha maombi ya kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kufariki kwa Baba mzazi wa Mbunge wa Kisesa, Mhe. Luhaga Joelson Mpina, Marehemu Mzee Mpina Gabisi Samweli Luchemba na kuhani msiba wa Mama yake Mpina, Marehemu Kephrine Kabula Masaga aliyezikwa Juni 8, 2022. Hafla hii imefanyika Kijiji cha Isangijo Wilaya ya Meatu Mkoa wa Simiyu Juni 15, 2022.

Mtume Boniface Mwamposa Bulldoza akimbariki Diwani wa Kata ya Lubiga, Mhe. Juma Isack Mpina ambaye ni Kaka wa Mbunge wa Kisesa, Mhe. Luhaga Joelson Mpina wakati wa ibada maalum ya kumbukumbu ya mwaka mmoja wa kifo cha Mzee Mpina Gabisi Samweli Luchemba na kuhani msiba wa Mama yake Mpina, Marehemu Kephrine Kabula Masaga Kijiji cha Isangijo Wilaya ya Meatu Mkoa wa Simiyu, Juni 15,2022
Mtume Boniface Mwamposa Bulldoza akiwapaka mafuta ya upako wananchi wa Jimbo la Kisesa walifika nyumbani kwa Mbunge wa Kisesa Mhe. Luhaga Joelson Mpina wakati wa ibada maalum ya kumbukumbu ya mwaka mmoja wa kifo cha Mzee Mpina Gabisi Samweli Luchemba na kuhani msiba wa Mama yake Mpina, Marehemu Kephrine Kabula Masaga katika Kijiji cha Isangijo Wilaya ya Meatu Mkoa wa Simiyu Juni 15,2022
Mtume Boniface Mwamposa akiwa katika picha ya pamoja na watoto wa Marehemu Kabula Kephrine Masaga baada ya ibada ya kumbukumbu ya mwaka mmoja wa kifo cha Mzee Mpina Gabisi Samweli Luchemba na kuhani msiba wa Mama mzazi wa Mpina aliyefariki  Juni 1, 2022. Hafla hii imefanyika katika Kijiji cha Isangijo Wilaya ya Meatu Mkoa wa Simiyu Juni 15, 2022.
Mtume Boniface Mwamposa akiiombea Baraka ardhi ya nyumbani kwa Mzee Mpina baada ya ibada ya kumbukumbu ya mwaka mmoja wa kifo cha Mzee Mpina Gabisi Samweli Luchemba na kuhani msiba wa mama yake Mzazi Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, Kephrine Kabula Masaga leo Juni 15, 2022 katika Kijiji cha Isangijo Wilaya ya Meatu Mkoa wa Simiyu.
Mtume Boniface Mwamposa Bulldoza akimpaka mafuta ya Baraka Mbunge wa Kisesa, Mhe. Luhaga Joelson Mpina wakati wa ibada maalum ya kumbukumbu ya mwaka mmoja wa kifo cha Mzee Mpina Gabisi Samweli Luchemba na kuhani msiba wa Mama yake Mpina, Marehemu Kephrine Kabula Masaga katika Kijiji cha Isangijo Wilaya ya Meatu Mkoa wa Simiyu Juni 15,2022


Mtume Boniface Mwamposa akiweka shada la maua katika Kaburi la Mama yake Mzazi, Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, Marehemu Kephrine Kabula Masaga aliyefariki Juni 1, 2022. Hafla hii imefanyika Kijiji cha Isangijo Wilaya ya Meatu Mkoa wa Simiyu leo Juni 15, 2022.

Mtume Boniface Mwamposa Bulldoza akiendesha maombi kwenye Kaburi la Mama yake mzazi Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, Marehemu Kephrine Kabula Masaga aliyezikwa Juni 8, 2022 pamoja na kumuombea Baba Mzazi wa Mpina Marehemu Mzee Mpina Gabisi Samweli Luchemba Hafla hii imefanyika Kijiji cha Isangijo Wilaya ya Meatu Mkoa wa Simiyu Juni 15, 2022.
Mtume Boniface Mwamposa Bulldoza (kulia) akiendesha maombi maalum ya kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kufariki kwa Baba mzazi wa Mbunge wa Kisesa, Mhe. Luhaga Mpina (kushoto), Marehemu Mpina Gabisi Samweli Luchemba na kuhani msiba wa Mama yake, Marehemu Kephrine Kabula Masaga katika Kijiji cha Isangijo Wilaya ya Meatu Mkoa wa Simiyu leo Juni 15, 2022