MAKAMU
Mwenyekiti wa UWT Taifa Bi.Thuwaiba Kisasi akizungumza na wanawake wa
Umoja huo katika Mikoa ya Mjini na Magharibi Unguja katika mwendelezo wa
ziara yake visiwani Zanzibar.
PICHA NA ABEID MACHANO
………………..
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
VIONGOZI na watendaji mbali mbali
wa Umoja wa Wanawake Tanzania(UWT) wametakiwa kukusanya taarifa na
takwimu sahihi za wanachama wa Chama cha Mapinduzi na Umoja huo kwa
lengo la kupata wanachama wa uhakika watakaoleta ushindi wa CCM katika
Uchaguzi Mkuu wa Dola wa mwaka 2020.
Agizo hilo limetolewa na Makamu
Mwenyekiti wa UWT Taifa Bi.Thuwaiba Kisasi wakati akizungumza na
wanawake wa umoja huo wa Mikoa ya Mjini na Magharibi Zanzibar huko
katika ukumbi wa Mkoa Mjini uliopo Amani, amesema ili CCM ishinde kwa
kishindo katika Chaguzi mbali mbali za dola ni lazima kuwepo na mfumo
rasmi wenye takwimu sahihi za wanachama hai.
Alisema kuwa Chama cha Mapinduzi
kinakabiliwa na changamoto zisizokuwa za lazima kwa baadhi ya uchaguzi
mbali mbali uliopita kutokana na kuwepo kwa tabia chafu za baadhi ya
watendaji kupotosha takwimu,hali inayopelekea kuwepo kwa wanachama ambao
sio halisi.
“Hatutowavumilia baadhi ya
watendaji ambao wanapotosha takwimu za wanachama wetu kwa kusudi ama
kutumiwa na baadhi ya watu wengine kwa maslahi yao binafsi lazima tuwe
waadilifu na wenye kuipenda jumuiya na Chama chetu kwa ujumla.
Kitendo cha kupotosha takwimu ni
sawa na kukisaliti chama chetu na kupelekea kitumie nguvu nyingi wakati
wa uchaguzi hali ya kuwa tuna rasilimali kubwa ya wanachama wanaokipenda
na kukiunga mkono chama chetu”, amesema Makamu Mwenyekiti huyo na
kuwasisitiza viongozi na watendaji wa UWT kuanzia ngazi za mashina hadi
taifa kuhakikisha wanaratibu takwimu sahihi za wanachama hai hasa wapya
wanaojiunga na chama hicho.
Pia alieleza kuwa Chama cha
Mapinduzi kwa sasa kipo katika utaratibu mzuri wa kuanzisha mfumo wa
kisasa wa kadi za wanachama za Kielectoniki zitakazokuwa na taarifa zote
za mwanachama kwa lengo la kurahisisha masuala mbali mbali ya
kiutendaji ndani taasisi hiyo.
Alifafanua kwamba kupitia kadi
hizo itakuwa rahisi kupata taarifa za wanachama hasa wa UWT ili iwe
rahisi kuwapatia mikopo mbali mbali kupitia vikundi vyao vya
ujasiriamali na fursa zingine zitakazowawezesha kujiajiri wenyewe.
Kupitia mkutano huo ambo ni
mwendelezo wa ziara ya kikazi ya Makamu Mwenyekiti huyo yenye lengo la
kuwashukru wanawake wa Umoja huo kwa busara zao za kumchagua kwa kura
nyingi katika uchaguzi wa UWT ngazi ya taifa pamoja na kukumbushana
utekelezaji wa mikakati mbali mbali ya kiutendaji ndani ya umoja huo.
Pia liwambia Akina Mama hao kuwa
uchaguzi umekwisha hivyo makundi yaliyoundwa wakati wa vuguvugu la
uchaguzi yavunjwe na badala yake washikamane kwa mustakabali wa
maendeleo ya umoja huo na CCM kwa ujumla.
“ Tunashukru katika uchaguzi wa
jumuiya zetu hazikutokea figisufigisu kama zilizotokea kwa baadhi ya
uchaguzi wa jumuiya za wenzetu hivyo tusirudi nyuma bali tupendane,
tushirikiane na kushauriana mambo mema yatakayoimarisha UWT kwa maslahi
ya wanawake wote wa Tanzania.”, alieleza Thuiwaba.
Akizungumzia mikakati ya
kiutendaji ya umoja huo kuwa ni pamoja na kuwapatia viongozi, watendaji
na wanachama wa ngazi mbali mbali mafunzo ya kuwajengea uwezo ili waweze
kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Naye Kaimu Naibu Katibu Mkuu
Zanzibar Bi. Tunu Kondo amesema UWT kwa Zanzibar imejipanga vizuri
katika kwenda sambamba na mabadiliko mbali mbali ya kiutendaji
yanayotokea katika chama na umoja huo.
Aliahidi kuwa maagizo mbali mbali
yaliyotolewa na Makamu Mwenyekiti kwa upande wa Umoja huo yatatekelezwa
kwa wakati mwafaka huku wakiendelea kufanya kazi kwa kasi,uadilifu na
ufanisi wa hali ya juu.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu
wa UWT anayefanyia kazi zake Tanzania bara, Eva Kiwele Mwingizi ameeleza
kufurahishwa kwake na ari na hamasa za kiutendaji za wanawake wa Umoja
huo katika Mikoa mbali mbali Zanzibar na kueleza kuwa hiyo ni ishara ya
mafanikio.
Amesema huu ndio wakati wa
wanawake wa Chama cha Mapinduzi Tanzania nzima kushirikiana katika
masuala mbali mbali ya kiamendeleo, kijamii na kisiasa kwa lengo la
kuidhibitishia dunia kuwa wanawake ni wachapakazi na sio watu wa kukaa
ndani tu bila kufanya kazi.
Katika mwendelezo wa ziara hiyo
Makamu Mwenyekiti huyo anamalizia ziara yake hiyo Mkoa wa Kaskazini
Unguja kwa upande wa Kisiwa cha Unguja.