Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amesema
kuwa Tanzania na Rwanda zimekubaliana kuunganisha Reli ya Kisasa
(Standard Gauge) kutoka Isaka mkoani Shinyanga mpaka Kigali nchini
Rwanda, ili kukuza biashara na uchumi wa nchi hizi mbili.
Rais
Magufuli ameeleza hayo leo Ikulu Jijini Daar es Salaam muda mfupi baada
ya kufanya mazungumzo na Rais wa Rwanda, Mhe. Paul Kagame aliyekuja
nchini kwa ziara ya kikazi ya siku moja.“Mimi na Rais Kagame kumeongea
mambo mengi ya ushirikiano na kwa pamoja tumekubaliana kuanza ujenzi wa
Reli ya Standard Gauge kutoka Isaka mpaka Kigali,” ameeleza Rais
Magufuli.
Ameeleza
kuwa ili kuharakisha ujenzi wa reli hiyo, kwa pamoja wamewaagiza
Mawaziri wanaohusika na sekta ya ujenzi na wale wale wa Mambo ya Nje wa
nchi hizi mbili kukutana haraka wiki ijayo kusughulikia masuala kadhaa
yanayohusu ujenzi wa reli hiyo ikiwa ni pamoja na kujadili namna ya
upatikanaji wa fedha za ujenzi.
Akielezea
umuhimu wa kukuza uchumi na biashara baina nchi hizi mbili, Rais
Magufuli amesema mpaka sasa mwenendo wa biashara kati ya nchi hizi
umekuwa wa kusuasua na kwamba reli hiyo itasaidia kuimarisha biashara na
ushirikiano wa Tanzania na Rwanda.
“Tunataka
ikifika mwezi Desemba mwaka huu, mimi na Rais Kagame tuwe tayari
tumeweka mawe ya msingi kwa ajili ya kuanza ujenzi wa reli hii,”
alisisitiza Rais Magufuli.
Amesisitiza
kuwa mbali na kuimarisha uchumi, ujenzi wa reli hiyo yenye urefu wa
takribani kilometa 400 pia utatoa ajira kwa vijana wengi na kusaidia
usafirishaji wa madini ya Nickel kutoka nchi za Rwanda, Burundi na
Tanzania ambapo madini hayo yanashindwa kuchimbwa kutokana na kukosekana
usafiri madhubuti wa reli.
Katika
hatua nyingine, Rais Magufuli amesema kwamba Tanzania inamuunga mkono
Rais Kagame kwa asilimia mia moja katika kuchukua Uenyekiti wa Umoja wa
Afrika na kwamba itafanya kila linalowezekana kuzishawishi nchi marafiki
pia zimuunge mkono Rais huyo wa Rwanda.
Kwa
upande wake, Rais Paul Kagame amemshukuru Rais Magufuli na Watanzania
kwa kumuunga mkono katika nafasi ya Uenyekiti wa Umoja wa Afrika na
kwamba atafanya kila linalowezekana kuzishawishi nchi za Afrika kuongeza
uwekezaji na kila nchi kuweka kikakati ya kuongeza ajira ili kuwafanya
vijana waachane na dhana ya kukimbili nchi za Ulaya kutafuta maisha
bora.
“Tatizo
la vijaqna kukimbilia nchi za Ulaya linaweza kumalizika iwapo sisi
Waafrika kwa umoja wetu tutashirikiana na kutafuta ufumbuzi, ikiwa ni
pamoja na nchi moja moja kuweka mikakati madhubuti ya kuwapa elimu na
ujuzi sahihi ili vijana hawa waweze kumudu mazingira yao na
kujiendeleza.” Ameeleza Rais Kagame.
Aidha,
Rais Kagame amesifu utendaji kazi wa Rais Magufuli na kuahidi kuja mara
kwa mara nchini Tanzania kwa ajili ya ushauri na kujifunza zaidi.
“Naahidi kuwa nitakuwa nakujamara kwa mara kuomba ushauri kutoka kwa
Rais Magufuli ili kuweza kusaidia nchi zetu na Bara la Afrika kwa
ujumla. Alimalizia Kagame
Hii
ni ziara ya tatu kwa Rais Kagame kuzuru Tanzania tangu Rais Magufuli
aingie Madarakani mwaka 2015. Mara ya kwanza alikuja kuhudhuria sherehe
za kuapishwa John Pombe Magufuli kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.