UMOJA WA ULAYA WAIPATIA TANZANIA MSAADA WA SHILINGI BILIONI 130 KUSAIDIA UPATIKANAJI UMEME VIJIJINI

November 02, 2017
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi Amina Shaban (kushoto) akiupokea ujumbe kutoka Umoja wa Ulaya, ukiongozwa na Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa na Maendeleo Bw. Neven Mimica (katikati) na Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania Bw. Roeland van de Geer, walipokuwa wanawasili Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kutoa msaada wa Euro milioni 50 kwa Tanzania.
 Ujumbe kutoka Umoja wa Ulaya pamoja na Maafisa wa Wizara ya Fedha na Mipango wakimsikiliza kwa makini, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James akitoa maelezo ya ujio wa ugeni huo kuwa ni neema kwa nchi ya Tanzania kwani Umoja wa Ulaya wametoa msaada wa Euro Milioni 50 utasaidia vijijini 3600 nchini kupata  umeme.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James (kulia) na akimweleza jambo Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa na Maendeleo wa Umoja wa Ulaya Mr. Neven Mimica wakati wa hafla fupi ya Umoja wa Ulaya (EU) kutiliana saini makubaliano ya msaada wa Euro milioni 50 kwa ajili ya kusaidia usambazi wa umeme vijijini kupitia Mradi Kabambe wa Kusambaza umeme Vijijini (REA).
  Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James akiwa pamoja na Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa na Maendeleo wa Umoja wa Ulaya Bw. Neven Mimica wakisaini Mkataba wa  msaada wa fedha za kusaidia usambazaji wa umeme Vijijini (EURO milioni 50) katika ukumbi wa  Wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam.
 Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James na Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa na Maendeleo wa Umoja wa Ulaya Mr. Neven Mimica, wakibadilishana hati za makubaliano ya msaada wa ruzuku ya kiasi cha EURO Milioni 50 katika ukumbi wa wizara ya Fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam.
  Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James akiwa na Ujumbe kutoka Umoja wa Ulaya pamoja na Maafisa waandamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kusaini mkataba wa msaada wa utekelezaji wa nishati ya umeme vijijini katika ukumbi wa Wizara ya fedha na Mipango, Jijini Dar es Salaam
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Doto James akiagana na Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa na Maendeleo wa Umoja wa Ulaya Bw. Neven Mimica, baada ya kusaini mkataba wa msaada wa Euro milioni 50 ambazo Umoja huo umeipatia Tanzania kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini kupitia Wakala wa Umeme Vijijini REA.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Wizara ya Fedha na Mipango)
Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
TANZANIA imezidi kupata neema kutoka Jumuiya ya Kimataifa ambapo Novemba 2, 2017, Umoja wa Ulaya (EU) umeipatia Tanzania msaada wa Euro milioni 50, takriban Shilingi bilioni 130 kwa ajili ya kufadhili Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini unaoendeshwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Mkataba wa Makubaliano hayo umetiwa saini Jijini Dar es Salaam kati ya Katibu Mkuu na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James na Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa na Maendeleo wa Umoja wa Ulaya (EU) Bw. Neven Mimica.
Msaada huo umelenga kuwasaidia raia wa Tanzania kufikiwa na huduma nafuu ya nishati ya umeme kwa kupanua uwezo wa gridi ya Taifa pamoja na mtandao wa usambazaji umeme.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James ameushukuru Umoja wa Ulaya kwa msaada huo mkubwa utakaoiwezesha nchi kuwa na umeme wa uhakika utakaochangia ukuaji wa uchumi wa nchi na maendeleo ya watu wake.
“Umoja wa ulaya ni wadau wetu muhimu wa maendeleo kutokana na misaada muhimu na mikubwa wanayotupatia, na kusadia agenda yetu ya maendeleo” alisema Bw. James
Alisema kuwa kiasi cha msaada wa Euro milioni 50 kilichotolewa na Umoja huo bila masharti yoyote si kidogo, na kwamba kitasaidia kutatua changamoto ya upatikanaji wa nishati ya umeme utakaochangia kuimarika kwa sekta ya viwanda itakayochochea ukuaji wa uchumi wa nchi.
Bw. Doto James alisema kuwa tangu Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini REA uanze miaka 9 iliyopita, idadi ya vijiji vilivyounganishiwa umeme imeongezeka kutoka vijiji 400 mwaka 2008 hadi kufikia vijiji 4395 hivi sasa.
Alisema kuwa ni matarajio ya Serikali kwamba ifikapo mwaka 2020, vijiji vyote 12,000 hapa nchini vitakuwa vimeunganishwa na nishati hiyo hivyo kuchochea shughuli za uzalishaji viwandani na kiuchumi kwa wananchi, vitaimarika.
Kwa upande wake, Kamishna wa Ushirikiano wa Kimataifa na Maendeleo wa Umoja wa Ulaya (EU) Bw. Neven Mimica, amesema kuwa msaada huo wa Euro milioni 50 wanaoutoa ni sehemu ya msaada wa Euro milioni 207 ambazo wanachama wengine wa Umoja huo, ikiwemo Sweden, Uingereza, Norway na Benki ya Dunia, watatoa kufanikisha mradi huo wa usambazaji umeme vijijini kupitia REA.

“Nguvu hizi za pamoja zitaviwezesha takriban vijiji 3,600 vilivyoko maeneo mbalimbali ya nchi ambapo watu zaidi ya milioni 1 wanatarajiwa kunufaika na mradi huo” Alisema Bw. Mimica
Alisema hatua hiyo itachangia kuimarika kwa ubora wa maisha ya wananchi wa Tanzania, kuimarika kwa sekta za afya, elimu na kuleta faida za kijamii na kiuchumi zinazoonekana kwao moja kwa moja hususan wanawake na watoto.
Misaada ya Umoja wa Ulaya kwa Tanzania imejikita katika Nyanja tatu za Utawala bora, Umeme na Kilimo endelevu ambapo Umoja huo kupitia Mfuko wake wa Maendeleo (EDF) umetenga kiasi cha Euro milioni 626 katika kipindi cha kuanzia mwaka 2014-2020

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »