Baada ya kupita miaka miwili bila kuchezwa kwa mashindano ya kuwania
Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki, michuano hiyo imerejea
tena msimu huu na Tanzania imethibitisha kushiriki.
Nchi wanachama Tanzania Bara, Zanzibar, Uganda, Kenya, Burundi, Rwanda, Somalia, Sudan, Sudan Kusini, Eritrea na Ethiopia.
Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),
Kidao Wilfred amethibitisha kikosi cha kwanza cha ‘Taifa Stars’
kushiriki na matarajio ya kufanya vema michuano hiyo itakayofanyika
kuanzia Novemba 25, 2017 hadi Desemba 9, mwaka huu.
Kidao amesema kwamba uteuzi wa timu za kwanza kwa kila nchi
mwanachama wa Baraza la Mpira wa Miguu la Afrika Mashariki ni
makubaliano ya viongozi wa CECAFA waliokutana kwa pamoja huko Sudan,
Septemba, mwaka huu.
Kutokana na makubaliano hayo ya kuita timu za kwanza, michuano hiyo
itaathiri kidogot ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwa
kuwa wachezaji wengi wanaounda kikosi hicho, wanatoka timu za VPL.
Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi (TPLB), Boniface Wambura amesema:
“Tutakaa kama kamati na kuangalia siku ya Jumatano na Alhamisi baada ya
michuano hiyo na kupanga ratiba ya mechi ambazo zitapanguliwa wakati wa
michuano ya Chalenji.”
Mbali ya michuano hiyo, Tanzania imethibitisha kushiriki michuano ya
Chalenji ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 itakayofanyika
Bujumbura nchini Burundi kuanzia Desemba 12, 2017 hadi Desemba 22, mwaka
huu.
Kadhalika, Tanzania imethibitisha kushiriki michuano ya Chalenji kwa
wanawake ikienda kutetea taji katika michuano itakayofanyika Rwanda
mwezi Desemba, mwaka huu. Tarehe rasmi itatajwa baadaye.
CECAFA imeamua kurejesha hadhi yake kwani mara baada ya michuano ya
Chalenji ya vijana huko Burundi, mwakani itakuwa ni zamu ya Tanzania
ambako michuano hiyo inatarajiwa kuanza Agosti 11, 2018 hadi Agosti 25,
mwakani.
Wakati huo huo Kidao amethibitisha Tanzania kuwa wenyeji wa
mashindano ya Vijana ya Chalenji ya CECAFA/CAF kwa vijana chini ya miaka
17 mwakani na mashindano hayo yatatumika kama sehemu ya kufanya
maandalizi Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri
wa chini ya miaka 17 (AFCON – U17).
Michuano ya mwakani ina baraka za Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa
sababu shirikisho hilo linataka kutumia michuano hiyo ya vijana ya
Kanda mbalimbali za Afrika kupata timu saba katika michuano AFCON – U17
ya mwaka 2019.
Kanda hizo ni CECAFA (Afrika Mashariki), COSAFA (Nchi za Kusini mwa
Afrika), WAFU – UFOA (Afrika Magharibi); UNAF (Afrika Kaskazini) na
UNIFFAC (Afrika ya Kati).
EmoticonEmoticon