HII HAPA LIGI KUU YA VODACOM TANZANIA BARA

November 02, 2017
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), hii hapa tena wikiendi hii.
Mechi moja inachezwa kesho Ijumaa Novemba 3, 2017 kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea ambako mwenyeji Majimaji FC itacheza na Stand United ya Shinyanga.
Mchezo huo wa Songea utaanza saa 10.00 jioni (1600h).
Jumamosi kutakuwa na michezo mitano ambako minne itaanza saa 10.00 jioni (1600h) wakati mwingine utakuwa saa 1.00 usiku (1900h).
Michezo hiyo ya Jumamosi itakuwa ni kati ya Singida United itakayocheza na Young Africans kwenye Uwanja wa Namfua mkoani Singida wakati Tanzania Prisons itakuwa wageni wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba  mjini Bukoba, Kagera.
Njombe Mji kwa upande wake watakuwa wenyeji wa Mbao FC ya Mwanza kwenye Uwanja wa Sabasaba mkoani Njombe huku Mtibwa Sugar ikisafiri kutoka Morogoro kwenda Mtwara kucheza na Ndanda FC kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona. Hizo ni mechi zitakazochezwa saa 10.00 jioni.
Mchezo pekee utakaofanyika saa 1.00 usiku utakuwa ni kati ya Azam FC na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Azam.
Jumapili kutakuwa na michezo miwili ya Ligi Kuu ambako Lipuli ya Iringa itakuwa mwenyeji wa Mwadui FC ya Shinyanga kwenye Uwanja wa Samora wakati Simba itakuwa mgeni wa Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya. Mechi hizo zitaanza saa 10.00 jioni.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »