Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF),
Jamal Emil Malinzi amewazawadia makocha wapya 27 waliofuzu kozi ya ukocha
kwamba kila mmoja mmoja atampa koni 20 na vizibao 22 kwa ajili ya mazoezi.
Rais Malinzi alitoa ahadi hiyo wakati wa hafla ya kufunga kozi ya ukocha ngazi
ya ‘Intermidiate’ kwa makocha waliohitimu. Rais Malinzi alialikwa
na waratibu kuwa mgeni rasmi ambaye awali, alishangazwa kwa namna ilivyoratibiwa
kwa kufuata miongozi ya TFF na CAF.
Katika hotuba yake, Rais Malinzi
aliwataka waamuzi hao kuzingatia weledi wakiwa ni mabalozi wa kupinga
matumizi ya dawa za kulevya lakini zaidi wajiepushe kwa njia yoyote
ile kupanga matokeo.
Rais Malinzi alifurahishwa na idadi
kubwa ya makocha waliohitimu kwani kabla walikuwa ni wachezaji wa timu
kubwa na kongwe mbalimbali, “Hilo sasa linanisukuma kuwapa kila mmoja
wenu koni 20 na bips (vizibao) 22,” alisema Rais Malinzi.
Alitumia nafasi hiyo kuwataka Watanzania
kuwaombea dunia Rais wa Heshima wa TFF, Leodegar Chilla Tenga ambaye
anawania Ujumbe wa Kamati ya Utendaji wa FIFA kwa nchi zinazozungumza
Kiingereza ambako anapambana na Kwesi wa Ghana.
Pia katika mkutano huo Mkuu wa CAF
utakaofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia ukihusisha nchi 53 kati ya
54 wanachama wa CAF, pia watapiga kura kuichagua Zanzibar kuwa mwanachama
kamili wa shirikisho hilo.
Kozi hiyo iliendeshwa na Wilfred
Kidao - Mkufunzi anayetambuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika
(CAF), akisaidiwa na Manyika Peter aliyefundisha programu au mtaala
kwa makocha wa makipa; Dk. Nassoro Ally Matunzya aliyewanoa makocha
hao kuhusu tiba za wanamichezo/wanasoka na Mkufunzi wa muda mrefu wa
soka, Hemed Mteza.
Wahitimu wa kozi hiyo walikuwa Doris
Malyaga ambaye ni Mwanamke pekee kati ya wanafunzi 27 walisoma kozi
hiyo kwa kipindi cha siku 14 cha mwanzo wa mwaka. Doris ni mwanahabari
za michezo aliyehudhuria kozi hiyo. Anaandikia gazeti la MwanaSPOTI
linalotolewa na Kampuni ya Magazeti ya Mwananchi (MCL).
Wengine ni nyota wa zamani wa timu
ya mpira wa miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ waliopata kuchezea klabu
kongwe na kubwa nchini. Wanafunzi hao ni Boniface Pawasa, Fred Mbuna,
Innocent Haule, Herry Morris, Ivo Mapunda, Nizar Khalfan na Mussa Hassan
Mgosi.
Wengine ni Omar Kapilima, Amosi Mgisa,
Uhuru Mwambungu, Yussuf Macho, George Minja, Haruna Adolf, Selemani
Omari, Ally Ruvu, Masoud Selemani, Haji Mustapha, Mhasham Khatib, Issa
Ndunje, Salum Kapilima, Said Salum, Julio Elieza, Hassan Mwakami, Rajab
Mponda, Ally Mbonde na Evod Mchemba.
EmoticonEmoticon