**********
Wiki moja baada ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyalandu kupangua wakurugenzi wizarani hupo, baadhi ya askari wa
wanyamapori wameibuka na kupinga uamuzi huo, huku wakitishia kufanya
mgomo.
Askari hao zaidi ya 10 walioomba kutotajwa majina
gazetini kwa usalama wa ajira zao, wamepinga kuondolewa kwa Prof
Alexander Songorwa kwenye nafasi ya Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori
na badala yake kuteuliwa kwa Paul Sarakikya kukaimu nafasi hiyo.
Mmoja wa askari hao, akizungumza kwa niaba ya
wenzake, alisema kwa ujumla wao wanashangazwa na jinsi Nyalandu
alivyomwondoa kazini Prof Songorwa licha ya kuwa alikuwa mtendaji mzuri
aliyejali wafanyakazi na kuweka uzalendo mbele.
“Profesa Songorwa alikuwa Pori la Selous kufanya
doria siku tatu kabla ya kuondolewa kazini, alishirikiana na askari,
hatua ambayo ni nadra sana kufanywa na viongozi,” alisema mmoja wa
askari hao.
Alisema endapo Rais Jakaya Kikwete hatatengua uamuzi uliofanywa na Nyalandu, watafanya mgomo ambao utasababisha tembo kuuawa.
“Huyu mtu amekaa wizarani kwa mwaka mmoja tu,
amejitahidi kudhibiti matumizi mabaya ya fedha, anajituma kiasi cha
kulala porini, lakini leo anaondolewa katika kazi bila sababu za
kueleweka. Sisi tunahisi kuna jambo hapa,” alisema askari huyo huku
akichagizwa na wenzake.
“Sisi tupo nyuma yake na hatutasita katika hilo. Kama anataka afukuze wizara nzima lakini siyo kumwondoa Songorwa.”
Walisema wana wasiwasi kuwa kuondolewa kwa Profesa
Songorwa kumesababishwa na utendaji wake mzuri hasa kudhibiti Mfuko wa
Hifadhi ya Wanyamapori (TWPF) ambao pengine umesababisha baadhi ya
watendaji ndani ya wizara waliokosa masilahi kupeleka taarifa za uongo
kumchongea Profesa Songorwa.
Askari hao walisema utendaji wa Profesa Songorwa
ulikuwa wa pekee kwa aina yake na aliweza kuendesha kitengo cha
kiintelijensia kilichogundua baadhi ya wafanyakazi wa maliasili
kujihusisha na ujangili.
“Aliweza kuwagundua wafanyakazi wa wizara ambao ni
majangili na majina anayo kwa nini asiachwe amalize kazi yake, badala
yake anafukuzwa bila kosa.” Alisema mmoja wao.
Nyalandu akanusha:
Hata hivyo, Nyalandu alikanusha tuhuma na lawama
zilizorushwa kwake kuwa amewapangua wakurugenzi kinyume na taratibu,
akisisitiza kuwa alichukua uamuzi huo kwa sababu ya kushindwa kutekeleza
majukumu yao.
chanzo:MWANANCHI