*MANGULA AWASILI KUONGEZA NGUVU IRINGA
MANGULA ATUA RASMI KALENGA
*Asema Chadema wanalia kilio cha mamba
*Ni kwa kukimbiwa na wananchi kwa kudhuru watu.
*Asema hatapanda jukwaani, ataratibu tu kampeni
*Asisitiza anayegombea Kalenga si Mgimwa ni CCM
NA BASHIR NKOROMO, IRINGA
MRATIBU wa Kampeni za CCM
katika uchaguzi mdogo jimbo la Kalenga, Iringa Vijijini, Makamu
Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula amesema, madai ya Chadema
kwamba CCM imepeleka mamluki katika jimbo hilo ni kilio cha mamba, baada
ya chama hicho kukimbiwa kutokana na vitendo vyake vya kudhuru watu
ikiwemo kuwatoboa macho kwa bisibisi na kuwamwagia tindikali.
Mangula amesema mbali na
vitendo vya kutoboa macho na kumwagia watu tindikali, ambavyo Chadema
inadaiwa kufanya, pia chama hicho kimeogofya wananchi kwenda kwenye
mikutano yake, kutokana na kujiwekea histoa mbaya ya watu kuuawa katika
mikutano yake kadhaa ambapo sasa wamefikia watu zaidi ya wanane tangu
chama hicho kuanzishwa.
Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM
Bara, ametoa ufafanuzi huo baada ya mwandishi mmoja wa habari kutaka
kujua CCM ilikuwa na maoni gani kuhusu tuhuma ambazo zimetolewa na
Chadema, kwenye mkutano wake na waandishi, leo, Machi 3, 2013 ikisema
kwamba CCM imeingiza watatu iliowaita majambazi, kutoka mikoani kwa nia
ya kufanya fujo jimboni Kalenga nyakati za kampeni.
Mangula ambaye amewasili mjini
Iringa, leo, Machi 3, 2013, akiwa tayari kuingia katika jimbo la
Kalenga, ambako alisema atapiga kambi hadi Machi 16, mwaka huu uchaguzi
ukapofanyika na CCM kuibuka Kidededea, alisema, CCM haina sababu ya
kuingiza waovu jimboni kwa kuwa siyo jadi yake na inatambua thamani ya
amani kuwepo katika eneo lolote.
"CCM inatambua umuhimu wa
amani mahala popote, na kwa bahati nzuri mimi binafsi ninao uzoefu na
mifano mingi kuhusu madhara ya kutoweka amani hivyo kama kiongozi na
mratibu wa kampeni za CCM katika jimbo hili la Kalenga siwezi kuruhusu
CCM kufanya mambo ya kijinga kiasi hicho", alisema Mangula na kuongeza;
"Wakati Chadema wanajaribu
kujikosha kwa wananchi kwa kulia machozi ya mamba, sisi tumeshajua
kwamba chama hicho kimeingiza mamluki kumi kutoka nje ya Iringa ikiwemo
Tarime na Temeke, na kuwatawanya katika kata
mbalimbali. Na hili sisi
tunalisema kwa ushahidi wa kutosha, tunawajua mamluki hao na hata majina
yao tunayo...tunasubiri kuchukua hatua za kisheria kabla ya kuwataja".
Katika hatua nyingine, Mangula
alilaani hatua ya Chadema kutumia ufukara wa mtoto mmoja na familia
yake, kuombea kura kwa wananchi katika kampeni zake zinazoendelea za
kumnadi mgombea wa chama hicho katika jimbo la Kalenga, akisema kwamba
hatua hiyo, mbali na kwamba siyo sahihi katika siasa lakini ni
kumfadhililisha mtoto huyo umasikini wake.
"Hawa Chadema hawana utu
kabisa, inawezekanaje Meneja wa kampeni wa chama hicho anambeba mtoto wa
mtu na kumnadi kwa wananchi kwamba amevaa sare chakavu za shule na
kwamba ni kiongozi wa CCM. Hili jambo limetusikitisha sana kwa sababu ni
kuivunjia heshima CCM na pia kumdhalililisha mtoto huyu kwa umasikini
wake", alisema Mangula alionyesha picha iliyochapishwa kwenye gazeti la
Tanzania Daima, Meneja wa kampeni za Chadema akiwa amembeba mtoto
aliyevaa nguo chakavu za shule.
Mangula aliwataka wana-CCM
katika jimbo la Kalenga kutokuwa na hofu yoyote, wakati wa kampeni na
siku ya kupiga kura kwa sababu anaamini ulinzi wa serikali upo wa
kutosha.
Akizungumza na baadhi ya
viongozi wa CCM mkoa wa Iringa, Mangula aliwataka kutumia muda wa
kampeni kuwajulisha wana-CCM na wananchi kwa jumla kwamba wanayemnadi
kushinga ubunge si Godfrey Mgimwa, bali ni CCM ndiyo inayowania kiti
hicho.