Khadija Baragasha,Tanga.
WAMILIKI wa vyombo vya habari na Wahariri Nchini
wameombwa kuzipa kipaumbele habari
zinazohusu unyanyasaji na ukatili kwenye vyombo vyao ili
jamii iweze kuelimika na kutambua athari
na kuepuka matendo hayo mabaya
Aidha waandishi wa habari nchini wameshauriwa
kutotangaza habari za taasisi ama
vikundi ambavyo shughuli zake zinamuelekeo wa
kuifanya jamii iende kinyume
na maadili ya mtanzania.
Hayo yalielezwa na mwanaharakati maarufu Jijini hapa wa haki za binaadamu, Nuru Rajab wakati akitoa maoni yake kuhusu matukio ya
kinyama yanayotokea ndani ya jamii yanayokiuka mpaka haki za binaadamu.
Akizungumzia unyanyasaji huo aliyouelekeza hasa kwa mtoto na wanawake, Rajab alisema kuwa unyanyasaji ni kitendo kisichokubalika ndani ya jamii na taifa kwa
ujumla na kwamba elimu ya ubaya na athari zake ni vema ikatangazwa kwa upana
zaidi na kupewa kipaumbele katika vyombo vya habari.
Mwanaharakati huyo ambaye pia ni
mwenyekiti wa vijana wa Chadema Wilaya ya Tanga alieleza kuwa hali na mapambano
ilivyo katika suala la unyanyasaji,
kunatakiwa elimu ya kutosha ndani ya jamii na kwamba njia pekee ya kusambaza
uelewa kwa watu ni kupitia vyombo vya
habari pamoja na waandishi kuacha
kuripoti taarifa za baadhi ya taasisi ama vikundi zinazokinzana na maadili ya
mtanzania.
Rajab pia
alieleza umuhimu wa viongozi wa dini kuimarisha suala la maadili na uadilifu kwa waumini wao pamoja na
kuweka bayana ubora wa muumini ni uchamungu wenye uadilifu.
Hata hivyo alieleza maana ya unyanyasaji,
athari zake na jinsi ya kukabiliana na tatizo hilo ndani ya jamii ambapo alisema
kuwa maana ya unyanyasaji ni kumtoa mtu kwenye hali yake ya kawaida na
kuonekana dhariri asiye na thamani mbele ya jamii.
Athari nyingine za unyanyasaji kwa mujibu wa Rajab ni mtu
kutoishi kwa uhuru,kukosa haki ya kufikilia elimu ya juu au zote,kumkatisha mtu
kushiriki katika shughuli za kisiasa na kiutamaduni,ongezeko la watoto wa
mitaani, kupoteza maisha kwa maradhi au kujiua, mtoto kukosa malezi bora na
hata kupunguza nguvukazi.
Aliwataka
wananchi kwa ujumla kuacha woga
katika kudai haki zao za msingi na kwamba mtu mwenye hofu na hata
kukidai kilichochake atakuwa anajinyanyasa mwenyewe na kusema
ili kupambana na unyanyasaji ndani ya jamii ni lazima kila mmoja awe
shujaa wa kusimamia haki na kuondoa hofu ya kuifuatilia pale anapoona inaporwa
na mtu aidha kwa kutumia nafasi yake,nguvu au uwezo kifedha.