KIWANDA CHA UTENGENEZAJI WA BERI ZA MAGAIRI,BETRI ZA SIMU KUFUNGULIWA HANDENI.

January 08, 2014
UJENZI wa mradi wa kiwanda cha kwanza Nchini Tanzania Kilichopo katika kijiji cha Mkalamo Kata ya Kwamsisi Wilayani Handeni Mkoani Tanga kinachojishugulisha na maswala ya utengenezaji wa betri za magari, betri za simu pamoja na bidhaa mbalimbali kupitia madini ya Grafait (KINYWE) kipo mbioni kufunguliwa na kuanza shuguli za uzalishaji mwanzoni mwa mwaka ujao hali ambayo itakuza uchumi wa Nchi yetu na Taifa kwa ujumla.

 Mmoja wa wamiliki wa kiwanda hicho kijulikanacho kwa jina la SinoTan Minning Industry ltd Mussa Luhezi huku akishirikiana na wachina alisema kuwa wapo kwenye hatua za mwisho za kufunga mashine kubwa za uzalishaji na baada ya hapo wananchi wa eneo hilo watapewa kipaumbele ya kufanya kazi katika kiwanda hicho. 

Akifafanua juu ya mradi huo Mussa alisema kuwa kupitia madini hayo watatumia teknolojia ya kutumia betri hizo katika gari bila kutumia disel au petrol lakini kwa sasa hivi wameanza na kutengeneza tofali za kuzuia moto kwenye nyumba za makazi huku wakiendelea na juhudi za kuomba kibali serikalini cha kuzalisha betri hizo.


''Tulipofanya  upembuzi yakinifu tulivutiwa kuwekeza katika eneo hilo baada ya kuona malighafi ya kutosha ambayo pamoja na kuwa na
faida kwa mwekezaji lakini pia utawasaidia kiuchumi wananchi wa eneo hilo na licha ya wananchi hao kupata ajira lakini pia watanufaika na nishati ya umeme itakayofika kiwandani hapo ,''alisema Mussa.

Meneja wa mradi huo Amiry Mainde alisema mpaka sasa wamekusanya tani 350 za kuanzia shuguli za uzalishaji  na kwa awamu ya pili wanatarajia kuongeza zaidi ya tani 1000, huku akielezea kuwa kupitia mradi huo watachimba visima vya maji ambavyo vitawasaidia wananchi kutatua kero ya ukosefu wa maji tatizo ambalo limekuwa likiwafanya wananchi wa eneo hilo kushindwa kujikita kwenye shuguli za uzalishaji  kwa kufuata maji katika visima vilivyopo mbali na makazi yao.

Baadhi ya Wananchi wa Kijiji hicho akiwemo Mgaza Hassan alionyeshwa  kufurahishwa na mradi huo na kuahidi kuwa bega kwa bega na wawekezaji hao kijijini hapo katika kuhakikisha kiwanda hicho kinaanza kazi na wakazi kutoka maeneo mbalimbali kufaidika na ajira kiwandani hapo.

Mradi huo unamiliki hekta 50 na mpaka sasa kimetumia zaidi ya Tsh billioni 22 za ujenzi wa kiwanda hicho katika kuhakikisha kinaleta maendeleo kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »