MWALALA:NILIWEKA HISTORIA YA MIAKA SABA YANGA KUIFUNGA SIMBA.

January 08, 2014
NAKUMBUKA bao ambalo nililifunga wakati nimesajiliwa na Yanga liliweka rekodi ya kufuta uteja wa timu hiyo kwa wapinzani wao Simba kwa kipindi cha miaka saba iliyopita kwa kufunga bao na hivyo kupelekea shangwe na nderemo katika mitaa ya Jangwani.

Kauli hii aliitoa mshambuliaji wa zamani wa Yanga,Benard Mwalala ambaye kwa sasa ni kocha mkuu wa timu ya Halmashauri FC ya Muheza anasema baada ya kufunga bao hilo alishangaa kuona uwanja mzima ukilipuka kwa kelele kitendo ambacho kilimfanya kuhisi upinzani wa timu hizo mbili ni mkubwa sana.


Akizungumzia histori yake binafsi kuhusu maisha ya soka ,Mwalala anasema alianza kucheza mpira ya miguu mwaka 2000 akiwa na timu ya Nzoia Sugar ya Kenya ambapo aliichezea kwa kipindi cha miaka mitatu na kuhamia timu ya Villa SC ya Uganda kuanzia mwaka 2003 mpaka 2006.

Anasema baada ya kumaliza mkataba wake na Villa SC ya Uganda aliamua kuja nchini Tanzania kujiunga na Mabingwa wa Ligi kuu Tanzania bara Yanga mwaka 2006 ambapo aliweza kudumu na timu hiyo kwa kipindi cha miaka miwili.

Mwalala anasema mwaka 2009 aliamua kuondoka hapa nchini kuelekea nchini Malaysia kujiunga na timu ya PDRM ambapo alifanikiwa kuichezea kwa kipindi cha mwaka mmoja kabla ya kurejea Yanga mwaka 2010 kuendeleza harakati zake za kisoka.

Kama unavyojua maisha ya mpira ya miguu ni kutafuta maslahi mwaka huo huo,Mwalala aliiacha timu hiyo na kutimkia nchini Omani kujiunga na timu ya Sur ambapo aliingia mkataba wa mwaka mmoja na baada ya hapo akarejea nchini kujiunga na mabingwa wa soka Tanzania bara 1988 Coastal Union “Wagosi wa Kaya”

Anaeleza kuwa aliweza kuichezea Coastal Union ya Tanga kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2011 mpaka 2012 alipoamua ondoka kwa kukosa nafasi ya kuichezea baada ya kumalizika msimu wa ligi kuu Tanzania bara.

Baada ya kuondoka kuacha kucheza Coastal Union,Mwalala alikwenda kusomea mafunzo ya Ukocha wa mpira wa miguu na kupata mafunzo hayo ngazi ya juu kutokana na umahiri wake na kupenda kazi yake aliweza kupata timu ya soka Halmashauri FC ya Muheza inayoshiriki Ligi ya Mkoa wa Tanga.

Akizungumzia sababu zilizompelekea yeye kupenda kuwa mwalimu wa mpira wa miguu,Mwalala anasema kilichomvutia ni kutokana na majukumu aliyowahi kupewa wakati akichezea Coastal Union ambapo yeye alikabidhiwa jukumu la kuifundisha timu hiyo wakati Kocha wao Mkuu,Jamhuri Kiwelu alipokwenda Dubai kusoma.

Anaeleza kuwa alipoachiwa jukumu hilo aliweza kuwaongoza vema wachezaji wenzake kwa kipindi cha mwezi mmoja na nusu kwa mafanikio makubwa yaliyopelekea wao kufanya vizuri katika michezo yao ya Ligi kuu iliyokuwa ikifuatia kabla ya Juma Mgunda kukabidhiwa kuinoa timu hiyo.

Mwalala anaeleza kuwa wakati akiwa mchezaji alianza kushughulika na masuala ya ukocha mpaka alipoamua kutundika daluga rasmi mwaka 2011 na kuingia rasmi kwenye mafunzo ya ualimu wa mpira wa miguu.

Anasema kitu ambacho hatoweza kukisahau maishani kwake kuhusiana na soka ni wakati alipokuwa akichezea Yanga alikwenda mazoezini akiwa amevalia jezi ya  Kenya ambayo ni nyekundu kitendo ambacho kiliwauzi mashabiki wa Yanga.

Mwandishi wa Makala hii alimuuliza Mwalala anadhani nini kifanyike Tanzania ili soka letu liweze kupiga hatua kubwa kama zilivyo nchi nyengine duniani,Mwalala anasema Tanzania inabahati kubwa sana kwa kuwa watanzania wanapenda mpira lakini miongoni mwao waache siasa ili kuweza kupata mafanikio.

Anaongeza kuwa lazima ufike wakati wachezaji wakubaliana kwa kauli moja kwenda kutafuta maisha ya mpira nchi za nje ili kuweza kuwapa nafasi wachezaji chipukizi nao waweze kuonekane pamoja na kuwa na utamaduni wa kucheza la nje ili kuleta ushindani wao kwa wao.

Aidha analitaka shirikisho la soka hapa nchini (TFF)kuhakikisha linaweka mkakati wa kuwalinda wachezaji kwa sababu kuna mikataba mingi ya wachezaji inavunjwa bila kufuatwa kwa utaratibu bila wao kuingilia kati lengo likiwa kuweza kuwapa motisha bila kuwepo upendeleo wa aina yoyote ile.

Halikadhalika aliushauri uongozi mpya wa shirikisho la soka ulioingia madarakani chini ya Rais wake,Jamali Malinzi kuhakikisha wanaongeza idadi ya timu zinazoshiriki Ligi kuu Tanzania bara ili viweze kuwa zaidi ya kumi na nne vilivyopo hivi sasa kwa sababu hakuna mashindano mengine ya kuchezwa zaidi ya hayo.

Mwalala pia anatoa ushauri kwa vilabu vyote vinavyoshiriki Ligi kuu kuhakikisha wanaziingia kwenye mashindano mbalimbali timu zao B kabla ya timu kubwa kucheza au kuingizwa kwenye ligi za wilaya ya mikoa ili kuwa kuwa na wachezaji wazuri  imara na ambao wataleta ushindani.

Mshambuliaji huyo wa zamani hakusita kuzungumzia suala la shirikisho hilo kuwatafuta wadhamini kwa ligi daraja la kwanza na ligi kuu soka Tanzania bara hasa kwa vikosi vya B ili kuweza kuleta mabadiliko makubwa katika soka letu na Taifa kwa ujumla

Akizungumza suala la viwanja vya soka hapa nchini,Mwalala aliishauri Serikali kupitia wizara ya michezo na utamaduni kuhakikisha inalisimamia suala hilo kwa kuweka msukumu mkubwa kwa viwanja ili kuwawezesha vijana kushiriki michezo kikamilifu.

Mwisho.
Mwandishi wa Makala hii anapatikana kupitia 
anapatikana kupitia 0714543839/0754000186.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »