SIMBA KUIVAA RUVU SHOOTING VPL

October 04, 2013
NA BONIFACE WAMBURA,DAR ES SALAM.
Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inaingia raundi ya saba kesho (Oktoba 5 mwaka huu)  kwa mechi nne ambapo Ruvu Shooting itakuwa mwenyeji wa vinara Simba kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 

Viingilio katika mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Mohamed Theofil kutoka Morogoro kuanzia saa 10 kamili jioni vitakuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000. Tiketi zitauzwa uwanjani kuanzia saa 4 asubuhi.

Mechi nyingine za kesho ni JKT Ruvu itakayoumana na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam huku Coastal Union ikiwa mwenyeji wa Azam kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha ndiyo utakaotoa fursa kwa timu za Oljoro JKT na Mbeya City kuoneshana ujuzi katika kusaka pointi tatu.

Ligi hiyo itaendelea Jumapili (Oktoba 6 mwaka huu) kwa mechi kati ya Yanga na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Mgambo Shooting itaialika Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »