SERIKALI, TAASISI ZAOMBWA KUISAIDIA U20 WANAWAKE

October 04, 2013
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeiomba Serikali, taasisi na kampuni mbalimbali kuisaidia timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya wanawake kwa vijana wenye umri chini ya miaka 20 inayojiwinda kwa mechi ya Kombe la Dunia dhidi ya Msumbiji.

Timu hiyo hivi sasa iko kambini Mlandizi mkoani Pwani chini ya Kocha Rogasian Kaijage kujiandaa kwa mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza itakayochezwa Oktoba 26 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mpira wa Miguu ya Wanawake ya TFF, Lina Kessy amesema hiki ndio kipindi muafaka cha kuisaidia timu hiyo ili iweze kufanya vizuri katika mashindano hayo.

Ameitaka jamii kujitokeza kuisaidia timu hiyo ambayo haina mdhamini wala mfadhili, kwani timu za Taifa ni za Watanzania badala ya kusubiri ifanye vibaya na kusema ni kichwa cha mwendawazimu.

Kessy ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA), ameishukuru kambi ya JKT Ruvu kwa kutoa fursa ya kambi kwani timu hiyo hailipii malazi badala yake inalipia huduma nyingine inazopata hapo.

Vilevile amewashukuru wadau mbalimbali ambao wamekuwa wakijitolea kutokana na ukweli kuwa tangu kuanza mashindano ya mpira wa miguu wa wanawake kumekuwepo uungwaji mkono mkubwa.

“Shukrani za kipekee kwa wazazi kukubali watoto wao wachezee timu ya Taifa, kwani wengi bado wanasoma na wapo chini ya uangalizi wa wazazi. Pia tunawaomba wazazi wajitokeze mazoezini ili kuwajenga kisaikolojia wachezaji wetu,” amesema.

Fainali za Dunia za U 20 kwa wanawake zitafanyika mwakani nchini Canada. Iwapo Tanzania itaitoa Msumbiji katika raundi hiyo, raundi inayofuata itacheza na mshindi kati ya Botswana na Zimbabwe

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »