KOCHA Mkuu wa timu ya Coastal Union,Hemed Morroco amesema kikosi chake kipo imara kuweza kuwakabili wapinzani wao Tanzania Prison katika mchezo wa Ligi kuu Tanzania bara ambao utachezwa Septemba 14 mwaka huu katika uwanja wa Mkwakwani mkoani hapa.
Akizungumza jana,Morroco alisema maandalizi yao kuelekea mchezo huo yanaendelea vizuri kwa wachezaji wake kufanya mazoezi kila siku asubuhi na jioni ili kuweza kuwakabili maafande hao wa jeshi la magereza hapa nchini pamoja na kuchukua pointi tatu muhimu.
Morroco alisema wao msimu huu wamedhamiria kumaliza mzunguko wa kwanza wakiwa wanaongoza ligi hiyo ambayo inashirikisha timu 14 ikiwa ni malengo yao waliyojiwekea kwa muda mrefu na kueleza hilo litawezekana kutokana na uimara wao na mshikamano uliopo.
Alisema ligi kuu msimu huu sio ya kubeza kutokana na kila timu kuonekana kujipanga na kutaka kupata pointi tatu muhimu hasa zinapokuwa zikicheza mechi zao za ugenini na nyumbani hivyo nasi tumejipanga zaidi kuhakikisha hilo kwenye timu yetu linafanikiwa.
"Tunajua mechi yetu na Prison haitakuwa rahisi sana kutokana na kuwa kila timu imejiandaa vya kutosha hivyo tutahakikisha tunatumia uwezo watu tulionao ili kuhakikisha pointi tatu muhimu zinabakia hapa hapa nyumbani "Alisema Morroco.
Aidha aliwataka wapenzi na mashabiki wa soka mkoani hapa kuendelea kuisapoti timu hiyo kwa kujitokeza kwa wingi hasa wanapocheza mechi zao ili kuipa hamasa ya kuweza kufanya vizuri kwenye michezo yao iliyosalia katika mzunguko wa kwanza wa ligi kuu.
EmoticonEmoticon