HANDENI WASHAURIWA KUHIFADHI CHAKULA.

August 12, 2013

Na Oscar Assenga,Handeni
WANANCHI wa wilaya ya Handeni mkoani Tanga wameshauriwa kuhifadhi chakula cha kutosha ili kujihadhari na upungufu wa chakula unaoweza kujitokeza kutokana na wilaya hiyo kutopata mavuno ya kutosha.

Ushauri huo ilitolewa na Kaimu Ofisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wa wilaya hiyo, Yibarila Kamele wakati akizungumza na mwandishi wa blog hii kuhusiana na maendeleo ya kilimo wilayani humo.

Kamele amesema kukosekana kwa mvua ya kutosha mwishoni mwa msimu huu kume sababisha wakulima kukosa mavuno ya kutosha kama walivyotegemea hali ambayo inaweza kuleta ukosefu wa chakula kama wananchi hawatakuwa makini na kuuza chakula hicho kidogo walichopata.

Amesema kuwa ni muhimu kila mwananchi ahifadhi chakula cha kutosha kwa msimu wote ujao ambapo kila kaya ya watu sita inatakiwa kujiwekea jumla ya magunia 18 ambayo ndio kadili la chakula kwa kaya.

Aidha pia Kamele amesema kuwa wananchi wote ambao watauza mahindi wauze kwa wakala wa taifa wa kuhifadhi chakula (NFRA) ambao kwa sasa wameshaingia Handeni na wananunua kilo moja ya mahindi kwa shilingi 530 na sio kama wanavyonunua wachuuzi wengine ambao wao wananunua kilo 350 ambayo inamuumiza mwananchi.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »