Na Mwamvua Mwinyi,Bagamoyo.
Wakazi
wa kijiji cha Yombo kata ya Yombo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani
wamelalamikia mradi wa maji uliofadhiliwa na Bank ya Dunia na kugharimu
milioni 297, ambao haufanyikazi huku wakiwa hawanufaiki nao tangu
ukamilike.
Aidha
wamelalamikia kukwama kwa mradi wa jengo la uzazi, katika zahanati ya
Yombo,ambalo limetumia kiasi cha sh.mil.55 na kuwekwa jiwe la msingi na
katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Taifa,Abdulrahman Kinana tangu
mwaka 2014.
Kilio
hicho kimetolewa na baadhi ya wakazi wa kijiji hicho ,wakati wa mkutano
wa wananchi uliomwita diwani wa kata ya Yombo ,Mohammed Usinga kwenda
kuwaeleza hatua zinazochukuliwa ili kukamilisha miradi hiyo .
Mkazi
wa Yombo,Jabir Omary ,alisema inasikitisha kuona serikali na wafadhili
wanatumia mamilioni ya fedha kwenye miradi ya maendeleo lakini
haiendelezwi na haifanyikazi.
Alieleza mradi huo wa maji umetumia fedha nyingi ,hivyo ni jukumu la serikali kuisimamia ili ilete tija ndani ya jamii.Mkazi
mwingine ,Abubakar Harubu alimtaka diwani wa kata hiyo pamoja na bodi
ya maji ya kata kufuatilia na kusimamia kero hizo kwa maslahi ya wakazi
hao.
"Mradi
huu ni donda ,hauna manufaa ,;"Sisi hatutaki kusikia sijui mradi
umerithishwa kutoka kwa diwani aliyepita ,tunachotaka kuona ni
muendelezo wa miradi iliyoanzishwa kipindi cha nyuma iendelezwe na sio
vinginevyo"
"Mradi
huu umetumia mamilioni ya fedha ,jamani hata hamsikii uchungu wa fedha
hizi ,yaani tanki la maji hadi linaweka uchafu ndani kutokana na kukosa
maji,tunaomba viongozi wetu kutatua kero hizi za maji na afya" alisema
Harubu.Kuhusu kukwama kwa jengo la uzazi kwenye zahanati ya Yombo,Jabir alisema akinamama wanadhalilika na kukosa huduma hiyo muhimu .
Alielezea
kuwa ,zahanati hiyo pia ilikuwa kwenye mpango wa kupandishwa hadhi na
kuwa kituo cha afya lakini wanashangaa ujenzi hauendelezwi na kuelezwa
kuna muongozo uliotolewa kuwa kunatakiwa hekari sita ndipo kujengwe
kituo hicho.
Nae
afisa tatibu wa zahanati ya Yombo,Donald Malamsha ,alisema makisio ya
ujenzi ya jengo la uzazi ilikuwa ni sh.milioni 87 na hadi kufikia ujenzi
ulipokomea imeshatumika milioni 55.
Malamsha
alielezea fedha iliyokwisha tumika ni nyingi hivyo halmashauri na
serikali iangalie changamoto zinazokwamisha mradi na kuzitafutia
ufumbuzi wa haraka.Akielezea juu ya kero hizo,diwani wa kata ya Yombo,Usinga aliitaka bodi ya maji kusimama kidete ili watu wapate huduma ya maji.
Alisema
atasimamia tatizo la transformer liweze kufanya kazi na kuagiza vituo
vichache vyenye tija vifunguliwe na visivyofaa viache kwa sasa.Usinga
,aliwaasa wananchi kuacha kuhujumu mradi huo kwa kukata mabomba ,kuiba
baadhi ya vifaa na kuharibu miundombinu na badala yake walinde
miundombinu ya mradi ili udumu kwa muda mrefu.
Akizungumzia
kuhusu jengo la uzazi ,Usinga alisema halmashauri imeshatenga
sh.milioni 20 ili kukamilisha ujenzi huo wakati ikisubiri kupatikane
eneo lenye hekari 4-6 la kujengwa kituo cha afya cha Yombo kwani eneo la
sasa halikidhi mahitaji.
Mwenyekiti
wa bodi ya maji ,Yombo ,Yahaya Omary alisema mradi huo umetekelezwa kwa
fedha kutoka bank ya dunia ,ulianza ujenzi July 2013 na kukamilishwa
Octoba 2015 lakini haufanyi kazi iliyotarajiwa .
Alikiri
mradi huo kukumbwa na changamoto nyingi ikiwemo transformer kutokuwa
imara,pump kuwa na shoti za mara kwa mara ,mabomba kupasuka na kuibwa
kwa baadhi ya vifaa.Yahaya
aliongeza, bomba zilizotumika ni ndogo kulingana na mradi wenyewe na
endapo mradi huo ungekamilika ungeweza kulisha watu zaidi ya 2,000.
Alifafanua
kuwa ,mradi wa maji bado haujakabidhiwa rasmi kwa wananchi ila
ulikabidhiwa kwa majaribio kwa miezi sita ambayo imepita huku kukiwa na
changamoto lukuki ambazo zinapaswa kutatuliwa kabla ya kukabidhi .
Mwandishi
wa habari hii,alimtafuta kwa mara kadhaa kwa njia ya simu mkurugenzi wa
halmashauri ya Bagamoyo, Fatuma Latu,kutolea ufafanuzi zaidi juu ya
miradi hiyo ,hakupokea wala kujibu sms.
Mkutano
huo uliazimia kuunda timu ya watu kumi ,ambayo itakwenda kufuatilia
suala hilo katika ngazi na idara husika ili kupata ufumbuzi.
Diwani
wa kata ya Yombo wilayani Bagamoyo, Mohammed Usinga akizungumza na
wakazi wa kijiji cha Yombo kuhusiana na baadhi ya miradi ya maendeleo
isiyofanyakazi na mengine kushindwa kuendelezwa.(picha na Mwamvua
Mwinyi)
Jengo
la wodi ya uzazi katika zahanati ya Yombo, Bagamoyo likiwa limekwama
kwenye ujenzi na kuwekwa jiwe la msingi na katibu mkuu wa CCM Taifa
,Abdurahman Kinana mwaka 2014 .
Mradi
wa maji uliofadhiliwa na bank ya dunia na kugharimu mamilioni ya fedha
huko kata ya Yombo Bagamoyo, ambao haufanyi kazi iliyotarajiwa na
wananchi hawanufaiki nao tangu ukamilike 2015.