Waziri
wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ameeleza kuridhishwa kwake na kazi ya
ujenzi wa miundombinu ya kusafirisha Umeme wa msongo wa kV 33
inayojengwa kuelekea eneo litakalotumika kuzalisha Umeme kwa kutumia
maporomoko ya maji ya Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge).
Dkt.
Kalemani aliyasema hayo mkoani Morogoro wakati alipofanya ziara ya
kukagua utekelezaji wa kazi ya maandalizi ya ujenzi wa mradi wa
Stiegler’s Gorge utakaozalisha umeme wa kiasi cha megawati 2100 pamoja
na kuzungumza na wananchi katika vijiji vinavyopitiwa na miundombinu
hiyo ya kusafirisha Umeme.
Dkt.
Kalemani alisema kuwa, maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa Umeme wa
Stiegler’s yanajumuisha ujenzi wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ya
Barabara na usafirishaji Umeme kuelekea eneo la Mradi ili mradi huo
mkubwa utekelezwe kwa ufanisi.
Alieleza
kuwa, ujenzi wa miundombinu hiyo ya usafirishaji umeme unatekelezwa na
kampuni ya ETDCO ambayo ni kampuni tanzu ya TANESCO na kwamba
miundombinu hiyo inajengwa kutoka katika kituo cha kituo cha kupoza
umeme cha Msavu hadi Mto Rufiji ambapo ni takriban kilometa 170.
“Kwa
Vijiji ambavyo vinapitiwa na mradi huu wa njia ya kusafirisha umeme,
wananchi watafungiwa umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 kama ilivyo
katika vijiji vingine vinavyopitiwa na miradi ya usambazaji umeme
vijijini na hakuna fidia kwa wananchi watakaopisha miundombinu hii,”
alisema Dkt Kalemani.
Alisema
kuwa, mradi wa Umeme wa Stiegler’s Gorge unatarajiwa kuanza kutekelezwa
mwezi Februari mwaka huu mara baada ya Mkandarasi kupatikana na kwamba
ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji umeme kuelekea eneo hilo la mradi
umetekelezwa kwa zaidi ya asilimia 80 na utakamilika mwezi Aprili mwaka
huu.
Meneja
Mradi wa Stiegler’s Gorge kutoka TANESCO, Florence Gwang’ombe, alisema
kuwa mradi huo wa ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme utaboresha
upatikanaji wa umeme katika maeneo ambayo hayakuwa na Umeme ikiwemo
baadhi ya maeneo ya Manispaa ya Morogoro, vijiji vya Matombo, Dakawa,
Kisaki pamoja na kambi ya Maafisa wa Wanyamapori ya Matambwe.
Alisema
kuwa, mradi unatarajiwa kutumia kiasi cha shilingi bilioni 6.1 hadi
kukamilika kwake na kwamba nguzo zinazotumika katika mradi huo ni za
miti na zege na katika sehemu nyingine umeme utasafirishwa kwa kutumia
nyaya zitakazopitishwa ardhini.
Kwa
upande wake, Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo alimpongeza
Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kufanya uamuzi wa kuanza kutekeleza
mradi huo wa Stieglers Gorge ambao alisema kuwa utaimarisha hali ya
upatikanaji wa umeme nchini, utainua uchumi wa nchi kutokana na
kuchochea uanzishwaji wa viwanda pamoja na maendeleo ya mtu mmoja mmoja
kupitia shughuli mbalimbali zinazotegemea nishati ya umeme.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ( wa Nne kushoto) akikagua maeneo ambayo miundombinu ya usafirishaji umeme inajengwa kuelekea katika eneo la Mto Rufiji utakapotekelezwa mradi wa uzalishaji umeme wa megawati 2100. Wa Tatu kulia ni Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo na wengine ni watendaji kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kampuni ya ETDCO ambayo ni kampuni tanzu ya TANESCO.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) akizungumza na watendaji kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na kampuni ya ETDCO ambayo ni kampuni tanzu ya TANESCO wakati alipokuwa katika kijiji cha Dakawa mkoani Morogoro kukagua miundombinu ya usafirishaji umeme inayojengwa kuelekea katika eneo la Mto Rufiji utakapotekelezwa mradi wa uzalishaji umeme wa megawati 2100.
Kazi ya ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji umeme kuelekea katika eneo la Mto Rufiji utakapotekelezwa mradi wa uzalishaji umeme wa megawati 2100 ikiendelea. Kazi hiyo inatekelezwa na kampuni ya ETDCO ambayo ni kampuni tanzu ya TANESCO.