Waziri wa Mifugo na Uvuvi,
Mhe. Luhaga Mpina(mwenye kofia), akimpima urefu samaki aina ya Sangara kwenye
rula maalum ili kubaini kama ana urefu unaotakiwa kisheria kwenye kiwanda cha Nile
Perch Limited jijini Mwanza, kushoto Dkt. Yohana Budeba Katibu Mkuu Uvuvi na
kulia ni Bwana Gabriel Mageni Afisa Mvuvi Mkuu. Samaki chini ya sentimita 50 na
mwenye zaidi ya sentimita 85 hawaruhusiwi kisheria kuvuliwa.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi,
Mhe. Luhaga Mpina akimbeba samaki aina ya sangara aliyevuliwa kinyume na
taratibu alipokuwa katika ukaguzi wa mazao ya uvuvi katika Kiwanda cha Nature
Fisheries Limited Jijini Mwanza, kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt
Yohana Budeba na kulia ni Afisa Uvuvi Mkuu Bw. Boniface Shatila.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi,
Mhe. Luhaga Mpina (Mwenye Kofia) akitoa tamko la Serikali la kuwataka wenye
viwanda vya samaki kutofadhili uvuvi haramu alipotembelea katika gati la Kiwanda
cha samaki cha Tanzania Fish Processing
(TFP) jijini Mwanza leo, kulia ni Katibu Mkuu wa Mifugo na Uvuvi Dkt. Yohana Budeba.
Samaki mzazi aina ya
Sangara aliyevuliwa kinyume na taratibu(alikuwa na urefu wa sentimita 120), samaki
ambaye akiachwa ziwani kwa muda wa miezi
mitatu ana uwezo wa kuzaa samaki milioni tatu, na kuongeza idadi kubwa ya jamii
hiyo ya samaki katika ziwa Victoria.
Na Mwandishi Maalum, Mwanza
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amewaamuru
wamiliki wa viwanda vitano vya kuchakata minofu ya samaki vilivyoko jijini
Mwanza kulipa faini ya shilingi milioni 180 ndani ya saa 24 baada ya kubainika kupokea
na kuchakata samaki wasioruhusiwa kwa kukiuka
Sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2009 sambamba na Sheria ya usimamizi wa Mazingira
namba 20 ya mwaka 2004
Pia Waziri Mpina amechukizwa na kitendo cha
viwanda hivyo kufadhili uvuvi haramu na kueleza kuwa ni bora kutokuwa na
kiwanda hata kimoja cha samaki kuliko kuendelea kuwa na viwanda vinavyofadhili
uvuvi haramu na kutishia kuvifunga viwanda vyote sambamba na kutaifisha samaki,
magari na boti zinazobeba samaki wasioruhusiwa.
Waziri Mpina amesema hayo leo kwa nyakati
tofauti wakati alipofanya ziara kutembelea viwanda vinavyochakata samaki jijini
Mwanza ambapo pia amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Yohana Budeba kuwasimamisha kazi maofisa watatu
wa Kitengo cha Udhibiti wa Usalama na Ubora wa Mazao ya Uvuvi Kituo cha Mwanza kutoka
Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa
sheria na kulisababishia Taifa hasara kubwa.
Maofisa hao ambao Waziri Mpina ameagiza
wasimamishwe kazi na kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu ni pamoja na Philemon
Mugabo,Dorina Mlenge na John Bosco Rubajuna
Waziri Mpina ametaja viwanda vilivyokutwa vikichakata samaki wasioruhusiwa
wakiwemo samaki wazazi na samaki wachanga na idadi ya kilo zilizokamatwa kwenye mabano kuwa
ni pamoja na Nile Perch Fish (920), Victoria Fish (131), Nature Fish (150),
Omega Fish (580), Tanzania Fish Processing (842) huku magari 41, boti 15, Nyavu
haramu 294 wakiwa na samaki wachanga na wazazi ambapo sheria inakataza kuvuliwa
samaki chini sentimita 50 na juu ya sentimita
85 .
Majina ya viwanda hivyo na faini zao
walizotozwa Nile Perch sh milioni 25, Tanzania Fish Processing sh. milioni 50, Victoria Perch Milioni 30,
Nature Fish milioni 25, Omega Fish Ltd milioni 50 ambapo amesisitiza kuwa
adhabu hiyo ni ya kwanza na ya mwisho na kwamba ikithibika tena wenye viwanda waendelea
kufadhili uvuvi haramu hatua za kuvifunga viwanda na kutaifisha mali ikiwemo
mitumbwi, boti na magari yatakayokuwa yanabeba samaki hao itafuata.
Waziri Mpina amesema ukanda wa Ziwa Victoria
ulikuwa na Viwanda 13 vya kuchakata samaki vilivyokuwa na uwezo wa kuchakata tani
1,065 kwa siku lakini kutokana na kushamiri kwa uvuvi usiongatia sheria
kumesababisha viwanda 5 kufa kutokana na kukosekana malighafi na kwamba viwanda
8 vilivyobaki sasa vinachakata tani 171 tu kwa siku huku ajira zikiwa
zimeporomoka kutoka ajira 4, 088 na kufikia 2,179 tu.
Mpina amesema tayari Rais Dk John Magufuli
ameshatoa maagizo kwa wavuvi kuachana na uvuvi haramu sambamba na wenye viwanda
kutofadhili uvuvi huo huku pia Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan naye
akisisitiza jambo hilo na Wizara ya Mifugo na Uvuvi ikikemea vikali huku Sheria
za nchi nazo zikikataza jambo hilo
lakini wenye viwanda kwa makusudi wameamua kudharau maagizo ya viongozi wakuu wa
nchi jambo ambalo Wizara ya Mifugo na Uvuvi chini ya uongozi wake Waziri Mpina
haliwezi kukubalika kamwe.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi)
Dk. Yohana Budeba amesema kama watumishi wa wizara yake wangesimamia majukumu
yao kikamilifu mambo hayo aliyobaini Waziri Mpina yasingejitokeza huku akikiri
kupokea maagizo yake yote na atayasimamia kwa haraka kuona yanatekelezwa.
Afisa Mazingira kutoka Baraza la Taifa la
Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira(NEMC), Mhandisi Boniphace Guni amesema wenye
viwanda hivyo wamekutwa na makosa ya kupatikana na samaki waliochini wa ukubwa,
kukutwa na samaki wachanga kinyume cha Sheria ya Usimamizi Mazingira namba 20 ya
mwaka 2004 pamoja na Sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 ambapo wamekiuka
kifungu namba 58(I)(a) hivyo wamestahili adhabu hiyo ya kulipa faini ya
milioni 180 ndani ya saa 24.