Na: Veronica Kazimoto, 04 Januari, 2018,
Dar es Salaam.
Mwaka
huu wa fedha wa 2017/18, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imedhamiria
kuongeza idadi ya walipakodi kwa ajili ya kuisaidia nchi yetu kupunguza
kutegemea misaada kutoka kwa wahisani.
Lengo
kuu la kuongeza walipakodi ni kupanua wigo na kuongeza makusanyo ambayo
hutumika katika kuleta maendeleo na kujenga uchumi wa nchi.
TRA
ina mikakati mbalimbali ambayo imechukuliwa na inaendelea kutekelezwa
ili kuhakikisha kuwa, walipakodi wanaongezeka na hatimaye kuongeza
mapato ya Serikali.
Mikakati
hiyo ni pamoja na kusajili walipakodi ambapo Mamlaka imezindua kampeni
ya usajili wa walipakodi nchi nzima ili kuhakikisha kwamba kila
mfanyabiashara anasajiliwa na kupata Namba ya Utambulisho ya Mlipakodi
(TIN) kwa urahisi na haraka.
Akizungumza
na waandishi wa habari hivi karibuni, Kamishna wa Kodi za Ndani Elijah
Mwandumbya wa Mamlaka ya Mapato Tanzania alisema, usajili wa walipakodi
ni chanzo cha kuongeza idadi ya walipakodi na mapato kwa ujumla.
"Moja
ya majukumu ya msingi ya TRA ni Usajili wa Walipakodi ambao huongeza
idadi ya walipakodi, wigo wa ulipaji kodi, makusanyo pamoja na kutoa
taarifa sahihi za walipakodi wanaostahili kukadiriwa na kutozwa kodi ili
kuchangia Pato la Taifa", Alisema Mwandumbya.
Mwandumbya
alisisitiza kuwa, walipakodi wadogo wanaostahili kulipa kodi kwa njia
ya makadirio, watalipa robo ya kwanza ndani ya siku tisini (90) kuanzia
waliposajiliwa tofauti na utaratibu uliokuwepo kwa kulipa kodi hiyo hata
kabla mfanyabishara hajaanza kufanya biashara husika.
"Wananchi
wanaostahili kusajiliwa kama walipakodi ni watu wote wanaotarajia
kuanzisha biashara, kumiliki vyombo vya usafiri kama vile gari na
pikipiki, wanaostahili kulipa kodi ya majengo, wanaoingiza bidhaa kutoka
nje ya nchi na wanaotarajia kupata leseni za udereva", alifafanua
Mwandumbya.
Aidha,
Mwandumbya aliyataja mahitaji ya usajili kuwa ni Mkataba wa pango au
uthibitisho wa umiliki wa mahali pa biashara, barua ya mwenyekiti wa
Serikali ya Mtaa ikiwa na muhuri na namba ya simu ya mwenyekiti wa mtaa
husika, kitambulisho cha mhusika kama vile hati ya kusafiria, leseni ya
udereva, kitambulisho cha uraia au cha mpiga kura na mhusika ni lazima
aende mwenyewe kwenye ofisi za TRA kwa ajili ya kupigwa picha na
kuchukuliwa alama za vidole.
Kamishna
Mwandumbya, amewatahadharisha wananchi kuwa makini na vishoka kwa kuwa
usajili huo hufanyika bila malipo na hufanyika katika ofisi za TRA na
katika vituo maalum ambapo wananchi watatangaziwa kupitia vyombo vya
habari na kwenye maeneo husika.
"Napenda
kuchukua fursa hii kuwatahadharisha wananchi wote wanaostahili kupata
namba ya utambulisho wa mlipakodi kuwa makini na vishoka wanaoweza
kutumia mwanya huo na kuharibu nia njema ya kampeni hii kwasababu hakuna
wakala yeyote aliyepewa jukumu la kusajili au hata kutoa fomu ya
usajili", ametahadharisha Mwandumbya.
Elijah
Mwandumbya amesema endapo mtu atapata changamoto yoyote katika kusajili
na kupata namba ya mlipakodi anashauriwa kuwasiliana na Ofisi ya TRA
iliyopo karibu au kupiga simu bure katika Kituo cha Huduma kwa namba
0800 750075 au 0800 780078 au kutuma barua pepe huduma@tra.go.tz au
services@tra.go.tz.
Hatua
nyingine ni uwepo wa mifumo mbalimbali ya kielektroniki ya kusajili
walipakodi ambayo imerahisisha ulipaji kodi na hivyo kuongeza ulipaji
kodi kwa hiari.
Mifumo
hii imepunguza muda wa usajili ambapo kabla ya kutumia mifumo hii ya
kielektroniki kazi ya kusajili walipakodi mpaka kukamilika ilikuwa
inachukua takribani siku 7 lakini baada ya kuanza kutumia mifumo hii,
usajili hufanyika ndani ya dakika 30 tu.
Mkurugenzi
wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania ndugu
Richard Kayombo akizungumza ofisini kwake alisema TRA imejiwekea lengo
la kusajili walipakodi wakubwa, wa kati na wadogo wapatao milioni moja
(1,000,000) kwa mwaka huu wa fedha 2017/18. Hii itasaidia kwa kiasi
kikubwa kuongeza idadi ya walipakodi na hatimaye kuongeza mapato ya
Serikali.
Kayombo
alisema kuwa, mamlaka ina mpango wa kuhakikisha kuwa wafanyabiashara
wote wanakuwa na Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) na kuongeza
ufanisi wa zoezi la usajili kwa kutumia Mfumo wa Vitalu - Block
Management System ambao utawezesha kutambua walipakodi wanaostahili
kusajiliwa na kulipa kodi.
Aidha,
ameongeza kwamba, mamlaka ina mkakati wa kuongeza idadi ya walipakodi
ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Halmashauri au Manispaa mbalimbali
ili kuhakikisha kila mfanyabiashara katika maeneo hayo anakuwa na namba
ya TIN. Namba hii husaidia kumtambua kila mfanyabiashara mahali
anapofanyia biashara yake na kiasi cha kodi anachotakiwa kulipa.
"Kama
mamlaka, tuna mpango wa kuwarahisishia wafanyabiashara muda wa kufanya
usajili kwa kupeleka vifaa vya usajili karibu na mahali wanapofanyia
biashara kwa ajili ya kuokoa muda wanaoutumia kwenda kwenye ofisi zetu
kufanya usajili", amesema Kayombo.
Kupitia
mkakati huu, Mamlaka ya Mapato ya Tanzania itaweza kuwatambua na
kuwasajili wafanyabiashara waliopo kwenye sekta isiyo rasmi kwa
kuwapatia Kadi ya Utambulisho. Wafanyabiashara hao ni kama vile wenye
maduka ya reja reja hasa wenye ma fremu, wamachinga, washereheshaji,
wachimbaji wadogo wa madini n.k.
Uwepo
wa idara cha Huduma na Elimu kwa Walipakodi kilichopo ndani ya Mamlaka,
ni hatua nyingine ya kuongeza idadi ya walipakodi ambapo idara hi
inajishughulisha na kutoa elimu kwa Umma juu ya umuhimu wa kulipa kodi,
kujibu hoja mbalimbali pamoja na kuwakumbusha walipakodi kulipa kodi kwa
hiari na kwa wakati muafaka kupitia ujumbe mfupi wa maneno.
Mikakati
na hatua zote zilizobainishwa hapo juu zitaongeza idadi ya walipakodi,
uhiari wa kulipa kodi na mapato ya Serikali kwa ujumla.