Kibaha. Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema serikali
inafanyia kazi mkakati mpya wa utoaji mikopo kwa wanafunzi wa kada ya
afya wanaosoma katika ngazi ya cheti na astashahada.
Waziri Ummy ameyasema hayo jana wakati akizindua jengo la
Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania lililopo Halmashauri ya mji Kibaha,
mkoani Pwani.
Alisema kundi hilo ni muhimu linalopaswa kuangaliwa kwa jicho
la pili, kwani ndilo linalotoa huduma kwa ukubwa wake katika sekta ya
afya.
“Nipo katika mazungumzo ya awali na Waziri wa Elimu, Sayansi
na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako kuangalia ni namna gani
tutaiwezesha tasnia hii ikue ili tupate watumishi wengi zaidi wenye
viwango, maana mzazi ataweza kulipa ada litakapofikia suala la chakula
na mengineyo inakuwa shida,” alisema.
Alisema watumishi wa ngazi za uuguzi na ukunga wenye ujuzi na
weledi wa kutosha pekee wanachukia takribani asilimia afya 60 ya
watumishi wote wa afya nchini.
“Shirika la Afya duniani (WHO) linasema kuwa, zaidi ya
asilimia 80 ya huduma zote za afya hutolewa na wauguzi na wakunga, hivyo
mimi binafsi, Wizara yangu na Serikali kwa ujumla tunaendelea kutoa
kipaumbele katika kuhakikisha huduma za uuguzi na ukunga nchini
zinaimarika vya kutosha,” alisema.