Mkuu wa Wilaya ya Chato Shabani
Ntarambe (aliyesimama) akimweleza jambo Waziri
wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina(mwenye kofia) wakati wa mkutano wa
hadhara kwenye soko la kimataifa la samaki la Kasenda wilayani Chato leo,
ambapo Waziri ameamuru kufanyika ukaguzi mpya wa hesabu za fedha kwenye masoko
yote ya kimataifa ya samaki na mazao yake yaliyoko katika Ziwa Victoria ili
kuhakiki uhalali wa mapato ya Serikali yaliyokusanywa katika kipindi cha
miaka mitano iliyopita.Kulia ni Diwani
wa kata ya Kasenda Muganza Mwita. (Picha
na John Mapepele)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina(mwenye kofia
katikati) akiwa kwenye moja ya boti inayotumika kwa Uvuvi wa samaki kwenye soko
la kimataifa la samaki la Kasenda wilayani Chato leo, Kulia ni Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Chato Bathromeo Christiani, Kushoto ni Diwani wa kata ya Kasenda Muganza Mwita. (Picha na John Mapepele)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina(mwenye kofia) akiwahutubia
wananchi kwenye soko la kimataifa la samaki la Kasenda wilayani Chato leo, ameamuru
kufanyika ukaguzi mpya wa hesabu za fedha kwenye masoko yote ya kimataifa ya
samaki na mazao yake yaliyoko katika Ziwa Victoria ili kuhakiki uhalali
wa mapato ya Serikali yaliyokusanywa katika kipindi cha miaka mitano
iliyopita. (Picha na John Mapepele)
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina(mwenye kofia) akikagua
ofisi za soko la kimataifa la samaki la Kasenda wilayani Chato leo, Kulia ni
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Uvuvi bi Mwanaidi Mlolwa. Nyumba
niYohana Mikumbe Mtekinolojia wa samaki katika soko la Kasenda. . (Picha na John Mapepele)
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina ameamuru
kufanyika ukaguzi mpya wa hesabu za fedha kwenye masoko yote ya kimataifa ya
samaki na mazao yake yaliyoko katika Ziwa Victoria ili kuhakiki uhalali
wa mapato ya Serikali yaliyokusanywa katika kipindi cha miaka mitano
iliyopita.
Masoko hayo yatakayohusika na ukaguzi huo ni pamoja na
Kirumba Mwanza, Nyakalilo Buchosa Mwanza ,Kasenda Chato Geita, Magalini
Muleba Kagera, Kemondo Bukoba Kagera na Mwigobero Musoma Mara ambapo
wafanyabiashara watakaobainika walihusika kufanya udanganyifu wa mapato
watatakiwa kurejesha fedha hizo walizoiibia Serikali kwa kipindi hicho ambapo
Watumishi wa Umma nao waliohusika kuhujumu mapato hayo watasakwa popote walipo
na kufikishwa kwenye vyombo vya dola kukabiliana na mashtaka ya kuhujumu wa
rasimali za nchi .
Hatua hiyo ya Waziri Mpina imekuja kufuatia kubaini kuwepo
udanganyifu mkubwa katika biashara ya samaki, dagaa,mabondo, na mapanki akibainisha
kuwepo tabia ya kupunguza uzito na idadi ya magunia,kubadilisha matumizi ya
vibali,kuchanganya mizigo ya ndani na nje ya nchi kwenye malori, kuanzishwa kwa
masoko ya kimataifa yasiyo rasmi na wafanyabiashara wakubwa wa mazao ya uvuvi
kutolipa kodi za mapato kutoka TRA.
Pia Waziri Mpina ameamuru kufutwa kwa masoko yote yasiyo
rasmi yaliyopewa hadhi ya kimataifa ikiwemo soko la Nyakalilo na Magalini
ambapo amemuagiza Katibu Mkuu Uvuvi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Yohana
Budeba kuwaondoa na kuwapangia vituo vingine vya kazi watumishi waliokuwepo
kwenye masoko hayo.
Waziri Mpina ametolea mfano udanganyifu mkubwa uliofanywa na
wafanyabiashara na watumishi wa umma wasio waaminifu likiwemo tukio la Disemba
16 mwaka jana ambapo mfanyabiashara mmoja (jina tunalo)huku akitumia gari lenye
usajili ya nchi ya Rwanda lenye namba za usajili RB 9591 alipewa kibali cha
kusafirisha magunia 258 kwenda Ngara mkoani Kagera na badala yake aliyapeleka
nchini Rwanda na kuisababishia Serikali hasara ya sh. Milioni 3.
Pia kupunguza uzito na idadi ya magunia ili kulipia kidogo
mapato ya Serikali akitolea mfano mfanyabiashara mwingine (jina tunalo) ambapo
Disemba 2 , 2017 kutoka soko la Kasenda alisafirisha magunia 300 ya dagaa
lakini yaliyolipiwa mrabaha wa Serikali ni magunia 200 tu huku Serikali
ikipoteza mapato ya magunia 100 .
Waziri Mpina amesema matukio hayo ya udanganyifu aliyotolea
mfano ni ya siku moja tu huku wafanyabiashara hao wakiwa na utamaduni wa
kusafirisha zaidi ya safari nane kwa mwezi ambapo Serikali hupoteza mabilioni
ya fedha za mapato kwa mwaka ambapo Samaki, dagaa, kayabo, mabondo,
mapanki,furu wamekuwa wakiroroshwa kupitia mipakani na njia ya panya kwenda
nchi za Rwanda, Burundi, DRC, Zambia, Malawi, Uganda na Kenya.
Amesema wafanyabiashara waliopewa leseni za kusafirisha
mazao ya uvuvi nje ya nchi wamekuwa mawakala wa raia wa kigeni ambapo kazi ya
kununua, kukusanya na kusafirisha hufanywa na wageni jambo ambalo ni kinyume
cha Sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 na kanuni zake za mwaka 2009 kifungu
cha 13 (14).
Kuhusu kasi ya Uvuvi haramu katika Wilaya ya Chato Waziri
Mpina amesema taarifa zinaonesha kwa kipindi cha Januari hadi Disemba
mwaka 2017 zana haramu zikiwemo Timba, Kokoro,Katuri,Mitumbwi, yenye thamani ya
sh milioni 525,207,000 vilikamatwa, kutaifishwa na kuteketezwa.
Ametumia nafasi hiyo kuwasihi wananchi kuacha uvuvi haramu
huku akieleza kusikitishwa na namna watanzania hao wazawa walivyopoteza mitaji
yao lakini akatangaza msimamo mzito.
“Nimesononeshwa sana na taarifa ya kuteketezwa kwa mitaji ya
wafanyabiashara hao wazawa kwa sababu ya kujihusisha na uvuvi haramu lakini
nataka kuwakikishia kuwa vita dhidi ya uvuvi haramu haina suluhu na kwamba
sitamuonea haya wala huruma mtu yoyote atakayejihusisha na uvuvi haramu
tutawashughulikia wote bila huruma kwani Serikali ya awamu ya tano imejidhatiti
kukabiliana na uvuvi haramu kwa nguvu zote na bila kuchoka”alisema.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya
Uvuvi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Mwanaidi Mlolwa alisema jukumu la
kulinda rasilimali za nchi liko kikatiba hivyo kila mwananchi ana wajibu
wa kusaidia kulinda rasilimali hizo zisitoroshwe kwa manufaa ya nchi ya
nyingine.
Amesema Sheria ya Uvuvi namba 22 ya mwaka 2003 kifungu
cha 37(a) (ii) na (iii) na kanuni zake za mwaka 2009 zinawapa mamlaka
wasimamizi wa Sheria hiyo kumkamata mtu yeyote anayekutwa na samaki na mazao
yake waliovuliwa kwa njia haramu na kutaifisha mali zote ikiwemo samaki, boti,
mitumbwi na magari yaliyobeba samaki hao.
Mkuu wa Wilaya ya Chato, Shabani Ntarambe amesema katika
kukabiliana na uvuvi haramu wilaya kwa kipindi cha Januari hadi
Disemba mwaka 2017 imefanikiwa kukamata ,kutaifisha na kuteketeza zana haramu
za uvuvi zikiwemo Timba, Kokoro,Katuri,Mitumbwi, yenye thamani ya sh. milioni
525.2 na kumhakikishia Waziri Mpina kuwa mapambano bado yanaendelea kukomesha
kabisa uvuvi haramu