Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Anastazia
Wambura jana Jumatatu Septemba 18, 2017 ametembelea Ofisi za Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) zilizoko Uwanja wa Kumbukumbu ya
Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.
Mhe. Naibu Waziri Anastazia Wambura ambaye aliongozana na Katibu Mkuu
wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Bw. Mohammed Kiganja alilakiwa na
Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Bw. Kidao Wilfred.
Mhe. Naibu Waziri Anastazia Wambura alifanya mazungumzo na Kidao kwa
muda ambako alijifunza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupata ripoti
ya utendaji katika mwezi mmoja tangu uongozi mpya wa TFF uingie
madarakani.
Mhe. Naibu Waziri baada ya kupata maelezo ya Utendaji kwa Uongozi
mpya amepongeza Uongozi mpya kwa kuanza vizuri na ameridhishwa na
mipango ya Uongozi mpya katika program za Vijana na Soka la Wanawake.
Pia amepongeza zoezi la Ugawaji wa mipira 100 kwa mikoa yote ya
Tanzania na kusema muhimu ni kutumika ilivyokusudiwa. Anaamini mwanzo
mzuri wa Rais Wallace Karia ni dalili njema za kuleta maendeleo makubwa
katika soka.
Mbali ya kuzungumza na Kaimu Katibu Mkuu, Naibu Waziri Wambura
alikuwa shuhuda wa mazoezi ya jioni ya Timu ya Taifa ya vijana wenye
umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ kwenye Uwanja wa Karume, Dar
es Salaam.
Mara baada ya mazoezi hayo, Naibu Waziri Anastazia alikaribishwa
kuzungumza na vijana wa Serengeti Boys, ambako awali kabisa alitaka
vijana hao ambao wengi wao wana umri wa chini ya miaka 15 kwa sasa kuwa
ni wenye thamani.
“Mtakumbuka kamba kwee Umitashumta mlikuwa wengi, ila mmebaki ninyi.
Nataka mjue kuwa Serikali iko hapa na tunafuatilia. Tunataka matunda
kutoka kwenu,” amesema Naibu Waziri, huku akiwapa salamu za Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dk. Harrison Mwakyembe.
Akaongeza: “Nawapongeza sana kwa kuonesha mnaweza. Ila fanyeni
mazoezi kwa juhudi, chezeni mpira kwa uhodari, ila msisahau kuzingatia
pia masoma. msifanye masihara hata kidogo. Mkizingatia masomo na kucheza
mpira, mtafanya makubwa zaidi.
“Naamini baada ya kambi hii mtakuwa vizuri. Je, kwenye mashindano
yajayo mtashika namba gani?” alihoji Naibu Waziri Wambura kabla ya
vijana kwa pamoja kujibu: “Namba moja.”
Shirikisho
la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), liliiteua Tanzania kuandaa Fainali za
Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 mwaka 2019. Tayari Tanzania imeanza kuandaa timu.
EmoticonEmoticon