PROF. MAGHEMBE ATOA SIKU 40 KWA WALIOLIMA NDANI YA HIFADHI YA TAIFA YA ARUSHA WAONDOKE KWA HIARI

September 19, 2017
Na HAMZA TEMBA - WMU
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe ameliagiza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kupitia Hifadhi ya Taifa ya Arusha kuhakikisha kuwa wananchi wote waliolima ndani ya eneo la hifadhi hiyo kinyume cha sheria wanaondoa mazao yao pamoja na kusitisha kabisa shughuli zozote za kibinadamu ndani ya hifadhi hiyo.  

Prof. Maghembe ametoa agizo hilo jana wakati akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya siku moja katika hifadhi hiyo iliyopo wilaya ya Arumeru mkoani Arusha kwa ajili ya kukagua shughuli mbalimbali zinazofanywa na hifadhi hiyo ikiwemo maeneo yenye mgogoro kwa ajili ya kuyatafutia ufumbuzi.

"Naagiza, kuanzia leo ni marufuku mtu yeyote kuonekana akilima katika eneo hili, wekeni askari hapa, atakayeonekana piga pingu, hatuwezi kushuhudia watu wanalima ndani ya hifadhi tukae kimya, ni lazima tuchukue hatua. Watangaziwe na wapewe muda wa kuondoa mazao yao, ndani ya siku 30 au 40 wawe wameshaondoka", alisisitiza Prof. Maghembe baada ya kukagua eneo hilo.

Awali akiwasilisha taarifa ya hifadhi hiyo kwa Waziri Maghembe, Mhifadhi Mkuu wa hifadhi hiyo, Steria Ndaga alisema eneo hilo ambalo pia linajulikana kama shamba namba 40 na 41 limekuwa na mgogoro tangu mwaka 1990 baada wananchi wa Kijiji cha Olkung'wado kuvamia eneo hilo huku wakitoa hoja kadhaa ikiwemo madai kuwa shamba hilo ni maeneo yao ya asili waliyokuwa wakimiliki tangu zamani.

Alisema hoja nyingine wanazozitoa ni kuwa walipewa mashamba hayo na Serikali wakati wa operesheni ya uanzishwaji wa vijiji mwaka 1975 na 1976, Aidha, hoja nyingine ni kuwa hawakushirikishwa kwenye mchakato wakati wa ugawaji wa mashamba hayo na kwamba TANAPA pia haina hati miliki ya mashamba hayo.

Ngada alisema hoja zote hizo zilikinzana na ukweli ya kwamba shamba hilo lilimilikishwa kwa TANAPA tangu mwaka 1980 baada ya kutolewa tangazo kwa wadau wanaoweza kuliendeleza kufuatia muwekezaji wa awali, James Preston Mallory kushindwa kuliendeleza na hivyo kufutiwa hati miliki na Mhe. Rais mnamo mwaka 1979.

“Wadau mbalimbali waliomba umiliki wake ikiwemo Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro na Halmashauri ya Kijiji cha Olkung'wado, lakini Kamati ya Ushauri ya Ardhi ya Mkoa wa Arusha ikaishauri Serikali mashamba hayo yamilikiwe na TANAPA na hivyo tukaandikiwa barua rasmi ya kukubaliwa kupewa shamba na Idara ya Ardhi Mkoa” alisema Ndaga.

Alisema TANAPA ilinunua eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 966 kwa lengo la kupanua hifadhi ya Taifa ya Arusha ambapo baada kupewa shamba hilo, iliagizwa kulipa fidia ya mali zilizokuwepo, mwaka 1983 tathmini ikafanyika na malipo yakalipwa Serikalini hatimaye TANAPA ikapewa barua ya kumiliki ardhi mwaka 1988. Alisema kwa upande wa Kijiji hicho cha Olkung'wado hakuna nyaraka yeyote inayoonesha shamba hilo kupewa kijiji hicho. 

Mhifadhi huyo alisema baada ya mgogoro wa muda mrefu, wataalam wa TANAPA walifanya survey katika shamba hilo ili kubaini maeneo yaliyo na shughuli nyingi za kibinadamu na yale yenye umuhimu zaidi kiikolojia, mapendekezo yalitolewa kuwa maeneo yenye shughuli nyingi za kibinadamu yaachwe kwa wananchi na yale yenye umuhimu kiikolojia yaendelee kuhifadhiwa, Bodi ya TANAPA iliridhia ekari 366 zipewe wananchi na ekari 600 ziendelee kuhifadhiwa.

“Baada ya kikao cha wadau wa uhifadhi kilichoitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru tarehe 11 Mei, 2017 ambacho kilijumuisha Madiwani, mwakilishi wa Mbunge, katibu tarafa, watendaji wa kata, wenyeviti na watendaji wa vijiji, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na wataalam wa halmashauri, ilifikiwa maazimio ambapo wajumbe waliridhia maamuzi ya Bodi ya Wadhamini ya TANAPA kuwapa wananchi ekari 366 ya shamba hilo na kubakiwa na ekari 600” alisema Ndaga.

Aliongeza “Kikao hicho pia kiliridhia TANAPA kuweka vigingi vya mpaka katika shamba hilo ambapo tarehe 14 Mei, mwaka huu, 2017 zoezi hilo lilianza na jumla ya vigingi 26 viliwekwa”.

Alisema hata hivyo kumekuwepo na taarifa kuwa baadhi ya wanakijiji wa Kitongoji cha Momella walifungua kesi mahakamani wakidai wakidai kuwa kijiji cha Olkung'wado kimenyang'anywa ardhi yao na TANAPA, hata hivyo Serikali hiyo ya Kijiji imekana kwa maandishi kuhisika na ufunguzi wa kesi hiyo wakidai imefunguliwa na mtu binafsi na sio Serikali ya Kijiji hicho.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Dkt. Alan Kijazi alimuhakikishia Waziri Maghembe kuwa maagizo yote aliyoyatoa ya kusitisha shughuli za kibinadamu ndani ya eneo hilo yatafanyiwa kazi na atapewa mrejesho wa utekelezaji wake.

Hifadhi ya Taifa ya Arusha ilianzishwa mwaka 1960 wakati huo ikiitwa Ngurdoto na ina ukubwa wa kilomita za mraba 322. Hifadhi hiyo ni maarufu kwa utalii wa magari, kutembea kwa miguu, kupanda milima (mlima Meru), utalii wa farasi, mitumbwi ya kuogelea, baiskeli na wa utalii wa kutumia farasi. Katika mwaka wa fedha uliopita 2016/2017 hifadhi hiyo ilivunja rekodi ya ukusanyaji wa mapato kwa asilimia 12 ambapo ilikusanya Shilingi bil. 5.4.
Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akiingia kwenye ofisi kuu ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha jana Mkoani Arusha katika ziara yake ya kikazi ya siku moja katika hifadhi hiyo iliyolenga kukagua shughuli za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuitafutia ufumbuzi. Kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Dkt. Alan Kijazi.
 Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akisalimiana na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Arusha, Steria Ndaga alipowasili katika ofisi kuu ya hifadhi hiyo jana Mkoani Arusha kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku moja iliyolenga kukagua shughuli za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuitafutia ufumbuzi. 
 Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Arusha, Steria Ndaga (wa pili kulia) akiwasilisha taarifa ya hifadhi hiyo kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja katika hifadhi hiyo jana ambayo ililenga kukagua shughuli za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuitafutia ufumbuzi.
Prof. Maghembe akizungumza kwenye kikao hicho.
Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Dkt. Alan Kijazi (kushoto) akizungumza kutambulisha viongozi wa Hifadhi ya Taifa ya Arusha kwa Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe (kulia) wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja katika hifadhi hiyo jana Mkoani Arusha ambapo ililenga kukagua shughuli za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuitafutia ufumbuzi. 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) na wajumbe wa kikao hicho wakifuatilia taarifa kuhusu Hifadhi ya Taifa ya Arusha ambayo iliwasilishwa na Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi hiyo, Steria Ndaga.
 Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe (kushoto) akiongea na viongozi wa TANAPA kuhusu eneo lililolimwa na wananchi ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha kinyume cha sheria wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja katika hifadhi hiyo iliyolenga kukagua shughuli za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuitafutia ufumbuzi, aliagiza wananchi hao waondolewe ndani ya siku 40. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Dkt. Alan Kijazi na Mhifadhi Mkuu wa hifadhi hiyo, Steria Ndaga (kulia). 
Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe (wa pili kulia) akisikiliza ufafanuzi wa jambo kutoka kwa Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Arusha, Steria Ndaga (kushoto) wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku moja katika hifadhi hiyo jana ambayo ililenga kukagua shughuli za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuitafutia ufumbuzi. 
 Baadhi ya wanyamapori (Twiga na Pundamilia) wakionekana wakijivinjari ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Arusha wakati wa ziara ya kikazi ya siku moja ya Waziri wa Maliasili, Prof. Jumanne Maghembe katika hifadhi hiyo jana ambayo ililenga kukagua shughuli za uhifadhi hususan maeneo yenye migogoro kwa ajili ya kuitafutia ufumbuzi. 

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »