TANZANITE YAREJEA KUJIPANGA DAR

September 19, 2017
Timu ya Taifa ya wasichana wenye umri wa chini ya miaka 20 (Tanzanite), imewasili salama nchini ikitokea Nigeria ambako ilicheza mechi ya awali dhidi ya wenyeji Nigeria katika mchezo wa kuwania kucheza Fainali za Kombe la Dunia 2018 huko Ufaransa.
Timu hiyo iliwasili saa 9.00 usiku wa kuamkia Jumanne Septemba 19, 2017 na kulakiwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Bw. Kidao Wilfred; Bw. Kaimu Mkurugenzi wa Mashindano, Bw. Jonas Kiwia na Ofisa Habari wa TFF, Bw. Alfred Lucas.

Mara baada ya kurejea, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Sebastian Nkoma, amesema walipoteza mchezo wa awali kwa kufungwa mabao 3-0 kwa sababu Nigeria ni timu bora na Tanzanite kwa sasa wanajipanga kwa ajili ya mchezo wa marudiano.

“Kwa kuwa tulionesha kiwango bora, ni matumaini yangu kwamba tutafanya vema kwenye mchezo wa marudiano hapa nyumbani na tutasonga mbele,” amesema Nkoma ambaye ndoto zake ni kuipeleka Tanzanite Ufaransa mwakani.

Mchezo wa marudiano utafanyika Oktoba mosi, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam, ulioko Chamazi, Dar es Salaam.

Wakati timu ikionekana ina ari ya kufanya vema kwenye mchezo wa marudiano, Kaimu Katibu Mkuu, Bw. Kidao Wilfred aliwapa shime kufanya vema kwenye mchezo wa kirafiki na kusisitiza kambi kuendelea mpaka mchezo wa maruadiano.

Mkuu wa Msafara, Bi. Amina Karuma, alisema kuwa mapambano bado yanaendelea na anaamini kikosi chake kitashinda katika mechi ya marudiano itakayochezwa baada ya wiki mbili. Karuma pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake Tanzania (TWFA).


Aliongeza kuwa anashikuru wachezaji wote ni wazima na wataendelea na kambi ili kujiandaa na mchezo wa marudiano huku akiahidi kuwatafutia mechi ya kirafiki kabla ya kuwakaribisha Nigeria.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »