TANAPA KUZINDUA KAMPENI YA USAFI MLIMA KILIMANJARO

April 20, 2016

PAS
Meneja Mawasiliano wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) Pascal Shelutete (kati) akiongea na wanahabari jijini Arusha jana kuhusiana na Kampeni ya siku Kumi ya Usafi wa Mlima Kilimanjaro inayotarajiwa kuanza leo. Wengine pichani ni Katibu Mtendaji wa Chama cha Mawakala wa Utalii  Tanzania Bw. Cyril Ako (kulia) na Mwakilishi kutoka Hoteli ya Kibo Palace BI. Jenipher Swai.
…………………………………………………………………………………………………..
Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kesho tarehe 21.04.2016 litazindua Kampeni Maalum ya siku 10 ya usafi wa Mlima Kilimanjaro. Uzinduzi huo Utafanywa na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Said Mecky Sadik.
Kazi hii ya kusafisha Mlima Kilimanjaro itafanywa na watumishi wa hifadhi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa utalii zaidi ya 200, wakiwemo mawakala wa utalii  (tour operators), waongoza wageni (guides), wapagazi (porters) na wapishi (cooks) wanaowahudumia watalii katika Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro.
Usafi huu utahusisha maeneo mbalimbali ya hifadhi kama vile njia za kupandia mlimani, maeneo ya kupiga kambi, maeneo ya mabanda, na maeneo ya kupumzikia wageni (picnic sites).
Kampeni hii ni muendelezo wa utaratibu wa kawaida wa hifadhi unaofanyika kila wakati kuhakikisha maeneo ya hifadhi hasa yanayotumika na wageni yanakuwa katika viwango vya kimataifa vya utoaji huduma kwa wageni. Huu ni utaratibu wenye lengo la kuwahamasisha wadau mbalimbali kuhakikisha kuwa wanauweka Mlima Kilimanjaro katika hali ya usafi muda wote.
Mlima Kilimanjaro unachangia zaidi ya Shilingi Bilioni 60 ambazo ni sawa na asilimia 34 kwa mwaka katika mapato ya TANAPA. Aidha, Mlima Kilimanjaro hutoa ajira zaidi ya laki tatu(300,000) kwa mwaka kwa Watanzania wanaofanya shughuli za utalii mlimani.
Imetolewa na Idara ya Mawasiliano
Hifadhi za Taifa Tanzania
20.04.2016

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »