Pichani kushoto Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Bw. Jowika
Kasunga akitoa ufafanuzi kwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Raisi Mazingira
na Muungano Mh. Luhaga Mpina (kushoto) wa namna ambavyo wilaya imeelekeza
Kiwanda cha Mbao cha Sao Hill na Green Resources Limited cha Mufindi
kutunza Mazingira, (katikati) ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda hicho
Bi Roselyne Mariki.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira
Mh. Luhaga Mpina akiangalia kipande cha gogo ambacho ni moja ya waste product
(taka) inayotoka katika kiwanda cha Sao Hill and Green Resources Limited
baada ya uzalishaji wa mbao na nguzo ambayo taka hiyo ya gogo pia hutumika
kutengenezea gundi. (Kushoto) Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Raisi Muungano na Mazingira akitoa maelekezo kwa uongozi wa kiwanda cha Sao Hill and Green Resources Limited, wa namna ya kuondosha taka za nguzo (hazipo pichani) zilizozagaaa katika eneo la kiwanda hicho..alipofanya ziara ya viwanda, ukaguzi wa usafi wa mazingira na kupanda miti Mkoani Iringa leo.
EVELYN MKOKOI
MUFINDI
10/4/2016
Kiwanda cha kuzalisha karatasi cha Mufindi Paper Mills kilichopo wilayani Mufindi
Mkoani Iringa, kimetozwa faini ya shilingi milioni ishirini kwa kukiuka
sheria ya usimamizi wa mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake.
Faini hiyo inayotakiwa kulipwa katika kipindi kisichozidi wala kupungua
wiki mbili imetokana na ukiukwaji wa sheria ya mazingira kwa utiririshaji
wa kemikali hatarishi kwa viumbe hai na mazingira katika mto kigogo,
na maeneo ya jirani na vijiji vinavyo uzunguka mto huo.
Akimfafanulia Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Raisi Muungano na Mazingira
Mh. Luhaga Mpina alipofanya ziara kiwandani hapo, Mratibu wa Baraza
la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kanda ya Nyanda
za Juu kusini. Bw. Godlove Mwaisojo, ameeleza kuwa moshi, vumbi na majitaka
yanayotoka katika mitambo ya kiwanda hicho baada ya uzalishaji wa karatasi,
yamezidi viwango vya sheria kwa kuwa na kemikali hatarishi kwa baiyonuwahi
na mazingira na hivyo Baraza limekuwa likielekza mara kadhaa uongozi
wa kiwnda hicho kurebisha mfumo wa utoaji taka bila utekelezaji wa aina
yoyote.
Bw. Mwamsojo alimueleza Mh Naibu Waziri Mpina Kuwa, kiwanda hicho
kimeshauriwa na baraza kuhakiki ubora wa hali wa hewa, na mitambo yao
ya uzalishaji lakini kilikaidi.
Kwa Upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Bw. Jowika Kasunga, amemueleza
Mh. Naibu Waziri Mpina kuwa, pamoja na ukiukwaji wa utekelezaji wa sheria
ya mazingira unaofanywa na kiwanda hicho, pia menejimenti ya kiwanda
hicho imekuwa na mgogoro mkubwa wa ardhi na mahusiano mabaya
na wanakijiji wanaozunguka kiwanda hicho, na kuwa karibia hekta elfu
kumi na nne za misitu zilizopo katika eneo hilo, zipo katika mgogoro
wa muda mrefu baina ya wanakijiji na muwekezaji huyo, ambapo mgogoro
huo umepelekea eneo hilo kutotumika na wanakijiji wala muwekezaji huyo.
Mh. Naibu Waziri Mpina, ameutaka uongozi wa mkoa wa Iringa kwa kushirikiana
na wizara husika kutatua mgogoro huo wa ardhi, ili uzalishaji wa rasilimali
ya misitu uendelee kwa manufaa ya taifa.
Kwa upande wake Mkuregenzi Mtendaji wa kiwanda hicho Bw. CHOUDARY kutoka barani Asia, alikubaliana
na adhabu hiyo na kuhaidi kurekebisha mitambo ya uzalishaji katika kiwanda
hicho kwa kipindi kisichozidi wiki mbili.
Ziara ya Naibu Waziri Mpina, pia ilihusisha ukaguzi wa mazingira katika
kiwanda cha uzalishaji mbao,nguzo na nishati cha Sao Hill and Green
Resources Limited, cha Mjini Mufindi na kujionea namna ambavyo kiwanda
hicho kinavyokabiliana na athari zitokanazo na mabadiliko ya tabia nchi
kwa kumiliki mashamba makubwa ya misitu katika vijiji vya Mapanda na
Achimbile, na kufanya biashara ya hewa ukaa.