Rais
Jakaya Mrisho Kikwete akiweka saini Hati za Ahadi ya Uadilifu kwa
Viongozi, Watumishi wa Umma na Sekta binafsi akishuhudiwa na viongozi wa
taasisi na sekta hizo leo Agosti 14, 2015 Ikulu jijini Dar es salaam.
…………………………………………………………………..
Na Lilian Lundo, MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Jakaya Kikwete amezipongeza sekta binafsi kwa kukubali
kusaini hati ya ahadi ya uadilifu katika harakati za mapambano dhidi
ya rushwa na utovu wa nidhamu.
Rais alisema hayo katika wakati
akihutubia wakati wa hafla ya uzinduzi wa hati hizo zinazojumuisha
sekta ya Umma na Binafsi katika ukumbi wa Ikulu jijini Dar es Salaam.
Katika hafla hiyo, Mhe. Rais
alisaini hati tatu ambazo ni Hati ya ahadi ya uadilifu ya Viongozi wa
Umma, hati ya ahadi ya uadilifu ya Utumishi wa Umma na hati ya uadilifu
ya Sekta Binafsi.
“Ushiriki wa sekta binafsi
katika hati hii utasaidia kuleta mabadiliko ya kuwa na mwenendo wa
kimaadili ya mapambano dhidi ya rushwa” alisema Mhe. Kikwete.
Rais Kikwete alisema kuwa badala
ya wananchi na sekta binafsi kulalamika pembeni ni vyema kuwasilisha
malalamiko yao katika sehemu husika ili hatua za kisheria ziweze
kuchukuliwa.
Aidha, Rais aliongeza kuwa
baadhi ya sekta binafsi zimekuwa zikiombwa na kutoa rushwa ili kupewa
upendeleo wa kupata tenda serikalini, hivyo kwa kusaini hati hiyo ya
ahadi ya uadilifu kutaondoa mianya ya upokeaji na utoaji rushwa katika
sekta hiyo.
Hati ya ahadi ya uadilifu
inakumbusha Makampuni, Viongozi na Watumishi wa Umma juu ya wajibu wao
wa kuzingatia kanuni za maadili na mapambano dhidi ya rushwa nchini.
Wazo la kuwa na ahadi ya
uadilifu liliibuliwa katika maabara ya Mpango wa Tekeleza kwa Matokeo
Makubwa Sasa (BRN) ambapo ilionekanakuwa rushwa bado ni tatizo katika
uendeshaji wa shughuli za Umma na Binafsi hususani utoaji huduma kwa
umma na biashara.