CHUO CHA UONGOZI WA FEDHA KUANZISHA MASOMO YA NGAZI YA CHETI -PEMBA

August 08, 2015

wat1 
NA RAMADHANI ALI/MAELEZO  
………………………………….. 
CHUO cha Uongozi wa Fedha Zanzibar (ZIFA) kitaanzisha Tawi lake Kisiwani Pemba kuanzia mwaka huu  wa masomo na kitaanza kufundisha  masomo ya   uongozi wa fedha ngazi ya cheti.
Akizungumza na waandishi wa Habari Makao Makauu ya ZIFA Chwaka, Kaimu Mkuu wa Taaluma Dkt. Iddi Salum Haji amesema wameamua kufungua Tawi  Pemba ili kuzipunguzia gharama  familia zenye  kipato cha chini.
Amesema utafiti uliofanywa na Chuo  umegundua  kuna vijana wengi Kisiwani Pemba waliomaliza kidato cha nne na wanazo  sifa za kujiunga na chuo kwa masomo ya cheti  lakini wanashindwa kutokana na familia zao kukosa uwezo wa kuwasomesha.
Ameongeza kuwa chuo kimejipanga  na kukamilisha taratibu zote za kutoa mafunzo hayo  katika Mji wa Wete na wanafikiria kuanzisha Tawi  Mjini Dar es salaam hapo baadae.
Dkt. Iddi  amesema lengo la Chuo hicho ni kujipanua zaidi hasa kufuatia matokeo mazuri ya mitihani ambapo mwaka huu asilimia 98.3 ya wanafunzi   870 waliofanya mitihani kuanzia  ngazi ya cheti mpaka shahada ya kwanza wamefaulu vizuri.
“Wanafunzi waliohitimu fani ya Uhasibu wamepasi asilimia mia,  IT asilimia 97 na  fani ya Ugavi na Ununuzi wamefaulu kwa asilimia 98,” amesema Kaimu Mkuu wa Taaluma.
Amesema mafanikio hayo yamepatikana  kutokana  na wanafunzi kujituma zaidi na walimu  kujitolea  kwa uwezo wao wote na  kuwa  wabunifu  katika kufundisha.
Ameeleza kuwa baadhi ya fani   zinzofundishwa na chuo cha Uongozi wa Fedha  yanaelekeza zaidi  kwa vitendo na yanawasaidia  wahitimu kuweza  kujiajiri wenyewe.
Dkt.  Iddi amewashauri  wazazi kuwa waangalifu  wakati vijana wao wanapotafuta  nafasi za kujiunga na Taasisi za elimu ya juu  na kuwataka wahakikishe wanawapeleka kwenye vyuo vyenye sifa na vilivyosajiliwa na  kutambuliwa na Bodi za elimu ya juu NACTE na  TCU.
“Hivi sasa kumeibuka  msururu wa vyuo vinavyojitangaza vinatoa mafunzo ya Elimu ya juu lakini wanafunzi wanapomaliza na kutafuta ajira ama masomo ya juu inakuwa vigumu kupata kutokana na kuwa havitambuliki,” alisema Dkt. Iddi
Kaimu Mkuu wa Idara ya Masomo ya jumla  ZIFA Maalim Said Mohd amesema chuo hivi sasa kimejipanga kuteremka ndani ya jamii kwa kutoa elimu kwa wajasiriamali  ili waweze  kujiendesha  wenyewe.
“Kwa kuanzia chuo tayari kimeendesha mafunzo ya ujasiriamali  kwa vikundi vya   Wilaya ya Kaskazini A, Wilaya ya Kati  na Wilaya Kusini kwa Unguja na Chake chake na Micheweni  Pemba na lengo ni kumaliza Wilaya zote za Zanzibar,” alisisitiza Maalim Said.
Mmoja wa wanafunzi waliomaliza masomo  mwaka huu Bakar Omar Hamad  ameishauri Wizara ya elimu kufanya mapitio ya Taasisi zinazotoa elimu ya juu nchini ili kuhakikisha  uhalali wa usajili wao,  mitaala inayotumika  inalingana  na masomo na  kuhakikisha walimu  wanazo sifa zinazokubalika.
Amesema wazazi wamekuwa wakiwekeza   fedha nyingi kuwasomesha watoto  wao lakini baadhi  ambao mwamko wa kielimu ni mdogo wanawapeleka vijana wao katika vyuo ambavyo  pamoja  na kupata usajili lakini masomo  yanayotolewa yanakosa ithibati ya kufundishwa.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »