Viwavijeshi vyavamia mashamba Kilindi

March 11, 2014
Wadudu  waharibifu wa mazao aina ya viwavijeshi wamevamia mashamba ya wakulima wa vijiji mbalimbali vilivyopo Kata nane za wilayani ya Kilindi na kuharibu mahindi.
Uharibifu wa wadudu hao umezua hofu ya kuibuka kwa baa la njaa wilayani hapa.

Wakizungumza katika mahojiano na NIPASHE kwenye Kijiji cha Msente, kilicho Kata ya Mswaki, wilayani Kilindi wakati walipokuwa wakikabidhiwa vyeti vya kuzaliwa vilivyoratibiwa na shirika la World Vision Tanzania, baadhi ya wakulima walisema hatua hiyo imewaathiri kwa kuwa wanakabiliwa na uhaba wa chakula.

“Yaani viwavijeshi vimevamia mazao shambani kwa kiasi kwamba tumebaki na njaa...tunaomba sana serikali itusaidie kuondokana na uharibifu huu," alisema Daud Ramadhani, mkazi wa Msente.

Awali, kabla ya kukabidhi vyeti vya kuzaliwa, Mratibu wa World Vision, Philipo Kibona, alisema kutokana na baadhi ya wakazi kukabiliwa na uhaba wa chakula na wameathiriwa na tatizo hilo hawatatozwa fedha za vyeti hivyo na badala yake fedha hizo ziwasaidie kununua chakula.

“Kutokana na uhaba wa chakula uliowakabili wananchi hawa tumeamua kutoa bure vyeti hivyo ili ziwasaidie kununua chakula," alisema Kibona.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Seleman Liwowa, akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu, alikiri kuwa wadudu hao wameathiri mazao wilayani humo na kwamba  idara ya kilimo imeomba lita 1,000 za dawa za kuulia wadudu hao kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ingawa wamefanikiwa kupata lita 200 tu ambazo wamezisambaza kwa baadhi ya vijiji ili kupunguza tatizo hilo.

CHANZO: NIPASHE

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »