Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward
Lowassa amekerwa na tabia ya baadhi ya watu wanaosambaza uzushi katika
mitandao ya kijamii kwa kutumia jina lake.
Lowassa alisema kuna watu
wanaoendeleza kusambasa picha ya noti ya Sh500 yenye picha yake huku
wakiongeza maneno mabaya juu yake.
Katika taarifa iliyotolewa na ofisi
yake, Lowassa alisema, "Kitendo hicho siyo utani, bali ni dhihaka na
dharau kwa alama za Taifa na mamlaka ya nchi."
"Hizi ni alama za Taifa ambazo
zinatakiwa kulindwa na kuheshimiwa na watu wote, si busara kwa hao
wanaozichezea kuendelea kufanya hivyo, kwani ni dharau kubwa kwa Taifa'
alisema.
Katika noti hiyo ya Sh500 inaonekana
upande wa kulia wa noti hiyo picha ya Edward Lowassa, huku ikikaribiana
na ngao ya Taifa huku ikionyesha kuwa ilitolewa na Benki Kuu ya
Tanzania..
Alisema anaheshimu maoni ya watu na
nguvu ya mitandao ya kijamii, lakini anasisitiza umuhimu kwa wananchi
hao kutumia nguvu hiyo ya mitandao kwa kujadili maendeleo ya nchi badala
ya kuzusha mambo yasiyo na tija. Kwa nyakati tofauti, picha hiyo
imekuwa ikisambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii ikiwamo ya
Facebook, Instagram, Whatsapp, na Twitter huku kukiwa na maneno kama
"timu Lowassa" na mengineyo.
Ikumbukwe kuwa Lowassa yupo katika
adhabu ya kutoshiriki katika masuala yoyote yahusianayo na kampeni za
chinichini za urais, baada ya kamati ya maadili ya CCM)kutoa hukumu yake
mwezi uliopita.
Adhabu hiyo pia iliwakumba wengine
watano wakiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira, Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na aliyewahi kuwa
Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Moja ya sababu ya adhabu hiyo ya miezi
12 ilikuwa ni kuanzisha kampeni za chinichini za kugombea urais mwaka
ujao nje ya muda uliopangwa, ambapo baadhi ya wanachama akiwamo Lowassa
walituhumiwa kuhusika kuandaa makundi na fulana za kujinadi.
Chanzo:Gazeti la Mwananchi Mtandaoni