NA OSCAR ASSENGA,TANGA.
MKUU wa Mkoa wa Tanga,Luteni Mstaafu Chiku Gallawa
amesema kuwa upo umuhimu wa wasichana kusaidiwa,kutiwa moyo na kuhamasishwa
kupenda kupata maendeleo yao pamoja na
kuwalinda watoto hao na vitendo vyote vya ukatili likiwemo la kuwaozesha
mapema.
Gallawa ametoa kauli hiyo wakati akitoa hotuba yake
katika uzinduzi wa mradi wa kuwajengea uwezo wasichana wa mkoa wa Tanga
iliyoratibiwa na Tasasi ya Tawode na kufadhiliwa na Denmark kupitia shirika
lake Maendeleo la DANIDA.
Amesema jukumu la kuwalinda watoto wa kike ni la
kitu mtu na kuitaka jamii itambue kuwa hakuna mtu mmoja au taasisi yenye
ujuzi,maarifa na rasilimali za kutosha kukidhi mahitaji yote ya kuwalinda watoto
hao.
Mkuu huyo wa mkoa ametoa wito kwa wadau wote wa
maendeleo ya mtoto wa mkoa wa Tanga kuunga mkono jitihada zilizoanzishwa na
taasisi hiyo katika kuwawezesha watoto hao kujitambua ikiwemo kujithamini.
Aidha ameitaka jamii kutambua umuhimu wa kuzingatia
haki za watoto wa kike na kuzipatia ufumbuzi changamoto mbalimbali
zinazowakabili.
Ameongeza kuwa serikali ya mkoa wa Tanga itatoa
ushirikiano wa kutosha wakati wa utekelezaji wa mradi huo ambao kwa kiasi
kikubwa matokeo yake yatawezesha kukuza uchumi na kuondoa umaskini katika mkoa.
Gallawa ameipongeza taasisi hiyo kwa kuandaa mpango
maalumu wa kufadhili wasichana wanafunzi waishio katika mazingira
magumu, wasichana wazazi wadogo na wanawake wenye uhitaji zaidi wapatao 1000 ili
kujiunga na mfuko wa bima ya Afya (NHIF) kuanzia mwaka 2014.
Mwisho.
EmoticonEmoticon