MWANDISHI WA HABARI APIGWA RISASI

October 14, 2013
Mwandishi wa Habari na mtangazaji wa ITV, Ufoo Saro
MWANDISHI wa Habari ambaye pia ni Mtangazaji wa ITV, Ufoo Saro, amepigwa risasi na mchumba wake aitwaye Antel Mushi. Baada ya kufanya unyama huo, Mushi ambaye alikuwa Mfanyakazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa nchini Sudan, alimuua kwa risasi mama yake Ufoo, Anastazia Saro (58) kisha naye akajiua.

Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema tukio hilo lilitokea jana alfajiri, eneo la Kibamba, Dar es Salaam. “Tukio hilo limetokea leo (jana), asubuhi saa 12 alfajiri eneo la Kibamba CCM, baada ya Mushi ambaye ni mzazi mwenzake na Ufoo, kurejea nchini juzi akitokea Sudan na kufikia nyumbani kwa Ufoo.

“Kabla ya tukio, inaonekana kulikuwa na mazungumzo kati ya wawili hao na mama yake Ufoo, ambapo walishindwa kuelewana na Mushi akampiga risasi kifuani mama yake Ufoo na kumuua kisha akampiga Ufoo tumboni na mguuni na yeye akajiua,” alisema Kamanda Kova.

Alisema kwamba, Ufoo baada ya kujeruhiwa, alikimbizwa katika Hospitali ya Tumbi Kibaha na baadaye akahamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo alifanyiwa upasuaji katika maeneo aliyojeruhiwa.

Hata hivyo, Kamanda Kova alisema jitihada za kupata maelezo ya Ufoo zilishindikana baada ya kuwaambia polisi kwamba atazungumza baada ya kupona.

Ufoo ana mtoto mmoja aitwaye Alven Mushi mwenye umri wa miaka 10 ambaye alimzaa na marehemu Mushi.


Source:Rai Jumatatu

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »