TANZANIA YAJIPANGA KUTUMIA NISHATI YA NYUKLIA KUZALISHA UMEME

August 29, 2024

 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati akiwasilisha Mpango wa Tanzania katika Mkutano wa Pili wa Masuala ya Nishati ya Nyuklia kati ya Marekani na nchi za Afrika (US-Africa Nuclear Energy Summit) unaoendelea Jijini Nairobi, Nchini Kenya.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko akiwa katika Mkutano wa Pili wa Masuala ya Nishati ya Nyuklia kati ya Marekani na nchi za Afrika (US-Africa Nuclear Energy Summit) unaoendelea Jijini Nairobi, Nchini Kenya.

Dkt. Biteko atangaza msimamo katika Mkutano wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia;

Asema mashapo 58,500 ya urani kutumika kama chanzo cha uzalishaji

Marekani kuendeleza ushirikiano na Afrika matumizi Nishati ya Nyuklia

Na Mwandishi wetu, Nairobi

Tanzania imeeleza mpango na utayari wake katika uendelezaji wa nishati ya nyuklia ikiwa ni moja ya vyanzo mbadala vya nishati safi ya umeme kwa maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa jamii.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati akiwasilisha Mpango wa Tanzania katika Mkutano wa Pili wa Masuala ya Nishati ya Nyuklia kati ya Marekani na nchi za Afrika (US-Africa Nuclear Energy Summit) unaoendelea Jijini Nairobi, Nchini Kenya.

Katika mkutano huo unaojumuisha viongozi katika Sekta ya Nishati, Watunga Sera na Wataalam kutoka nchi mbalimbali barani Afrika, Dkt. Biteko amesema Tanzania iko tayari kuendeleza nishati ya nyuklia ikiwa ni moja ya vyanzo vitakavyoiwezesha nchi kuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika na ambayo inakidhi viwango vya kimataifa katika uhifadhi wa mazingira.

“Utayari wa Tanzania katika kuendeleza na kutumia nishati ya nyuklia unatiliwa mkazo katika Sera ya Nishati ya mwaka 2015, Sera ya Madini ya mwaka 2009, Mpango Kabambe wa Kuendeleza Sekta ya Umeme na Mkakati wa Nishati Jadidifu ambapo nyaraka zote hizi zinatambua umuhimu wa nyuklia kukidhi mahitaji ya nishati nchini.” Ameeleza Dkt. Biteko

Amesema chini ya uongozi wa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Serikali inaendelea kuchukua hatua muhimu zitakazowezesha matumizi ya nishati nyuklia kama moja ya vyanzo vya nishati safi ambapo hadi sasa Tanzania ina mashapo ya madini ya urani takriban tani 58,500 ambayo yanaweza kutumika kama chanzo cha uzalishaji wa nishati ya nyuklia.

Amefafanua kuwa, uwepo wa vyanzo mbadala wa vya umeme utawezesha nchi kuboresha mashirikiano yake ya kibiashara na nchi nyingine ndani na nje ya bara la Afrika na hivyo kuboresha uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

“Mpango huu wa kuwa na umeme wa kutosha utawezesha hatua ya kuunganisha gridi za umeme miongoni mwa nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika na baadaye katika maeneo mengine ya Bara hili.” Amesema Dkt.Biteko

Ametumia mkutano huo kueleza nia ya Tanzania kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo nchi ya Marekani na Bara la Afrika ili kuendeleza nishati ya nyuklia hasa ikizingatiwa kuwa takriban watu milioni 600 barani Afrika na biashara ndogondogo zipatazo milioni 10 bado zinakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa umeme wa uhakika.

Amesema mahitaji ya umeme nchini Tanzania yanakua kwa asilimia 10 hadi 15 kwa mwaka na ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu, Tanzania imepanga kuzalisha megawati 10,000 za umeme ifikapo mwaka 2030.

Kwa upande wake, Msaidizi Maalum wa Rais wa Marekani wa Masuala ya Uhifadhi wa Mazingira, Fedha na Uvumbuzi, Bw. Nana Ayensu amesema kuwa mkutano huo ni muhimu kwa nchi washiriki katika kufungua milango ya uendelezaji wa nishati ya nyuklia ambayo ni rafiki kwa matumizi ya binadamu na hifadhi ya mazingira na pia kuimarisha ushirikiano miongoni mwa nchi husika.

Ameongeza kuwa nishati ya nyuklia itafanikisha ajenda za kimataifa za nishati safi zinazoendelea ikiwemo nishati safi ya kupikia inayopigiwa chapuo kimataifa huku kinara wake akiwa ni Rais, Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Akizungujmzia utayari wa nchi yake, amesema Marekani ipo tayari kushirikiana na nchi za Afrika ili kuendeleza matumizi ya nishati ya nyuklia ambayo inatoa uhakika wa upatikanaji nishati na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »