RAIS SAMIA AMEWAJENGEA HESHIMA WANAWAKE KATIKA MAENDELEO NA KUSISITIZA MATUMIZI YA NISHATI SAFI

August 29, 2024

 








Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
JUMUIYA ya Wanawake (UWT)Kibaha Mjini, Mkoani Pwani, imetoa wito kwa wanawake kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika kuleta maendeleo na kuboresha huduma za kijamii, huku ikisifu juhudi zake za kuleta mapinduzi kwenye sekta za usafirishaji, uwekezaji, nishati safi na uwezeshaji kwa wanawake.

Mbaraza kutoka UWT Mkoani Pwani, Mariam Ulega akiwa mgeni rasmi katika Kongamano la kumpongeza Rais Samia wilayani Kibaha alieleza ,Rais kawajengea heshima kubwa wanawake ,kwa kuwa miongoni mwa maRais nchini walioacha alama kwenye utendaji kazi wake.

Aliziomba Jumuiya ya wanawake,vijana na chama ziendelee kusema makubwa yaliyotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita ili jamii ifahamu.

Akielezea kuhusu Uwekezaji katika Miundombinu, anasema Rais ameweza kusimamia na kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo SGR ambao umeleta Mapinduzi kwenye sekta ya usafirishaji.

"Serikali pia imeendelea na ujenzi wa bwawa la umeme Stigo Rufiji ambalo litapunguza changamoto ya kukosa umeme wa uhakika na ukarabati wa barabara za wilaya na mkoa ili kuboresha usafiri na usafirishaji wa bidhaa, hususan kwa wakulima na wafanyabiashara"

Mariam alieleza mkoa umeendelea kuwa kitovu cha viwanda nchini Tanzania, na kusisitiza serikali imehimiza uwekezaji wa viwanda vidogo na vikubwa hali itakayochangia kuongeza ajira na kukuza uchumi wa mkoa.

Kadhalika Mariam Ulega aliwataka jamii kutumia nishati safi kwa kuachana na matumizi ya mkaa na kuni,na kuwataka wanawake,wanaume, wafanyabiashara, wakulima,vijana, shule ,vyuo, taasisi mbalimbali kuondokana na matumizi ya nishati chafu.

"Rais Samia Suluhu Hassan ni champion wa nishati safi, kwani amekuwa akisisitiza umuhimu wa kufikisha nishati safi kwa jamii , matumizi ya majiko sanifu ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa"

Mariam alifafanua kwamba, Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kushirikiana na Jumuiya za Kimataifa na wawekezaji wa nje katika kukuza matumizi ya nishati safi, ambayo ni sehemu ya mikakati ya kudhibiti mabadiliko ya tabianchi.

Akitoa taarifa ya Jumuiya, Mwenyekiti wa UWT Kibaha Mjini, Elina Mgonja alimpongeza Rais Samia kwa kazi kubwa anazozifanya na kupeleka mabilioni ya fedha kutekeleza miradi mbalimbali wilayani Kibaha.

Vilevile katika kuonyesha shukrani kwa Rais Samia, Mgonja aliwataka wanawake na vijana kuhakikisha wanajitokeza kwa wingi katika uchaguzi ujao ili kumpa Rais Samia Suluhu Hassan kura za kutosha kuendelea kuleta maendeleo nchini.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »