WANAWAKE UWT KIBAHA MJI WAMPA HEKO RAIS SAMIA KWA KUCHAPA KAZI

August 29, 2024


NA VICTOR MASANGU, KIBAHA

Umoja wa wanawake Wilaya ya Kibaha mjini (UWT) katika kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kutekeleza ilani ya chama kwa vitendo imeamua kufanya kongamano kubwa la kumpongeza kwa dhati kutokana na kutenga fedha ambazo zimekwenda kuwasaidia kwa kiasi kikubwa kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo kwa wananchi.

Akizungumza katika kongamano hilo ambalo limehudhuliwa na viongozi mbali mbali wa chama na serikali pamoja na jumuiya zake Mwenyekiti wa UW T Wilaya ya Kibaha mjini Elina Mgonja amebainisha kwamba lengo lubwa ni kumpongeza Rais kwa kazi nzuri ambazo amekuwa akizifanya za kuwasaidia wananchi hususan kumtua mama ndoo kichwani.

"Sisi kama umoja wa wanawake UWT Kibaha mjini tumeungana kwa pamoja na kuandaa kongamano hili kwa lengo kubwa la kumpongeza Rais wetu Mama Samia kwani ameweza kufanya mambo makubwa katika nyanja mbali mbali ikiwemo kuboresha huduma ya afya, ujenzi wa miundombinu ya barabara, elimu sambamba na kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama ambayo imepelekea kumtua mama ndoo kichwani,"alisema Mgonja.

Mgonja alisema kwamba Rais Samia kwa kipindi chake cha miaka mitatu na nusu tangu alipoingia madarakani ameweza kuendelea kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo katika Jimbo la Kibaha pamoja na Mkoa mzima wa Pwani ambayo baadhi yake imeanza kufanya kazi na kuwasaidia wananchi katika maeneo tofauti sambamba na kuongeza kasi ya kuleta uchumi.

Katika hatua nyingine hakusita kumshukuru kwa dhati Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini Silvestry Koka , Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mkurugenzi wa Kibaha mjini, Mlezi wa UWT Selina Koka,Mke wa mbunge wa Jimbo la Mkuranga Mariam Ulega , pamoja na madiwani wote kwa kushirikiana bega kwa bega katika kuhakikisha kongamano hilo linafanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Kwa upande wake Mlezi wa UWT Wilaya ya Kibaha mjini Selina Koka ambaye pia mke wa Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini amesema kwamba amemshukuru Rais Samia kwa kuweza kutekeleza miradi mbali mbali ya maendeleo kwa vitendo katika Jimbo la Kibaha mjini ambayo imeweza kuleta chachu ya kuwasaidia wananchi katika nyanja tofauti tofauti.

Mama Koka amesema kwamba katika Jimbo la Kibaha mjini Rais Samia ameweza kuleta mageuzi makubwa katika nyanja mbali mbali kwenye kata zipatazo 14 ikiwemo sekta afya, katika kuboresha miundombinu ya zahanati, vituo vya afya, Hospitali, elimu, huduma ya maji safi na salama,nishati ya umeme pamoja na miundombinu ya barabara.

Naye mgeni rasmi katika Kongamano hilo Mariamu Ulega ambaye pia ni mke wa Mbunge wa Jimbo la Mkuranga amewapongeza wanawake wa UWT kwa kuweza kuandaa kongamano hilo kwa lengo la kumpongeza Rais wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kuwasaidia wananchi katika mambo mbali mbali ikiwemo kuwasogezea huduma za kijamii ikiwemo vituo vya afya, elimu, maji pamoja na mahitaji mengine.

Aliongeza kwamba wanawake wa UWT wameweza kufanya kitendo cha kiugwana kutokana na kutambua umuhimu na mchango mkubwa ambao ameufanya na Rais Samia katika kutekeleza ilani ya chama kwa vitendo kwa kushirikiana bega kwa bega na Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini ikiwemo kutenga fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

Umoja wa wanawake wa UWT Kibaha mjini katika kongamano hilo limeweza kugusia mambo muhimu ambayo yamefanywa na Rais ikiwemo utoaji wa vifaa vya Tehama,utoaji wa elimu bila malipo,kuboresha fursa za watoto wa kike katika elimu,stahiki za walimu,uboreshaji wa afya, huduma ya maji, pamoja na miundombinu ya barabara.













Share this

Related Posts

Previous
Next Post »