DC BUNDA: UWEPO WA TAWA WILAYANI BUNDA UNA MANUFAA MAKUBWA KWA WANANCHI

February 05, 2024

 Na. Beatus Maganja


Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mhe. Dkt. Vicent Anney amesema wananchi wa wilaya yake wananufaika sana na uwepo wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA kutokana na ufadhili wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotokana na shughuli za uwindaji wa kitalii unaofanyika katika Pori la Akiba Grumeti.

Dkt. Vicent ameyasema hayo Februari 02, 2024 wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo iliyofadhiliwa na TAWA wilayani humo.

"Nichukue nafasi hii kuishukuru TAWA kwa uwepo wake katika wilaya ya Bunda, pia tunaishukuru Serikali kwa mipango yake kwasababu imetusaidia sisi wananchi wa Bunda kupata huduma mbalimbali za kijamii ambazo zimetokana na gawio linalotokana na shughuli za uwindaji zinazofanywa katika maeneo ya Bunda " amesema

Mkuu huyo wa wilaya amesema TAWA imefadhili miradi miwili katika Kata ya Hunyari Kijiji cha Sarakwa ambayo ni darasa moja (1) na Ofisi moja (1) ya Mwalimu Mkuu, samani za shule ambazo ni jumla ya madawati 100, vitu vya walimu 12, meza 5 za walimu na mantenki matatu yenye ujazo wa Lita 2000 kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi kuhifadhi maji pamoja na nyumba mbili (2) za walimu ambazo zimesaidia kuboresha ufundishaji kwa kuwa walimu wanakuwa na utulivu wa mawazo

Wananchi wa kijiji cha Sarakwa wameishukuru Serikali na kukiri kuwa TAWA ndiyo taasisi pekee iliyojitokeza kufadhili miradi mikubwa katika Kijiji hicho tangu kuanzisha kwake, baada ya wananchi kuhangaika kwa muda mrefu kukamilisha miradi hiyo kwa nguvu zao bila mafanikio na hivyo kukibatiza Kijiji chao kwa jina la "Kijiji cha TAWA".

"Tangu kuanzishwa kwa Kijiji hiki Mwaka 2014, Kijiji hiki na shule hii (Shule ya Msingi Steven Wasira) haikuwahi kupata mradi wowote, TAWA pekee ndiyo imekuwa ya kwanza kutoa mradi mkubwa wa madawati 100, kumalizia chumba cha darasa moja (1), meza 5 na viti 12 vya walimu na ofisi 1 ya walimu kwahiyo Kijiji hiki tunakipa jina TAWA" amesema Mwenyekiti wa Kijiji Kijiji cha Sarakwa Giragu Gisunu Nyarumuga

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Msingi Steven Wasira Paulo Kisumda amesema miradi hiyo iliyofadhiliwa na TAWA katika Kijiji cha Sarakwa imesaidia kupunguza migongano kati ya wananchi na wanyamapori ambapo amekiri kuwa awali walikuwa wanawachukia Wanyamapori lakini tangu waanze kupata miradi hii wamegundua wanyamapori wana faida kubwa, na wao kama wananchi ni sehemu ya wamiliki wa rasilimali hiyo hivyo wataongeza ushirikiano katika kuwalinda na kuwahifadhi.

Kwa upande wake Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ikifanya mambo makubwa kwa wananchi kupitia taasisi hiyo, hivyo TAWA imejidhatiti kuuhabarisha umma wa watanzania kwa kufanya ziara wilaya kwa wilaya, vijiji kwa vijiji kuhakikisha wanaelewa umuhimu na faida za shughuli za uwindaji wa kitalii Nchini.







Share this

Related Posts

Previous
Next Post »