TADB YAADHIMISHA MWEZI WA SARATANI YA MATITI KWA ELIMU NA VIPIMO KWA WANAFANYAKAZI WAKE

November 01, 2023

 Na Mwandishi Wetu


Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeendesha semina ya mafunzo ya uelewa wa saratani ya matiti , saratani ya mlango wa shingo ya kizazi, saratani ya tezi dume na maambukizi ya virusi vya UKIMWI kwa wafanyakazi wake.

Semina hiyo iliyoambatana na upimaji kwa wafanyakazi hao, iliendeshwa kama sehemu ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kukabiliana na Saratani nchini.

Akiongea wakati wa semina hiyo, Mkuu wa rasilimali watu na utawala wa TADB Bi. Noela Ntunkamazina alisema kuwa kwa kushirikiana na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, (ORCI) TADB wameungana na mataifa mengine kuwaongezea uelewa wa saratani mbalimbali wafanyakazi wake mwezi Oktoba ambao unatambulika kama mwezi wa kuongeza uelewa wa Saratani ya matiti.

“Kwa kutambua kuwa saratani ni ugonjwa unaoathiri jinsia zote na kwa kuelewa kuwa kupitia upimaji wa afya mara kwa mara saratani hugundulika mapema na hivyo kwa kupata tiba sahihi muathirika huweza kupona, kama TADB tumeona vyema kuwapa wafanyakazi wetu fursa ya kupata elimu na kupima ilikufahamu hali zao za kiafya,” alisema.

Daktari Bingwa magonjwa ya Saratani kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dkt. Sadiq Siu alibainisha kuwa saratani ya matiti ni saratani ya pili inayoongoza kwa vifo vya wanawake nchini ikitanguliwa na saratani ya shingo ya uzazi. Pia alibainisha kuwa saratani ya matiti inaathiri siyo tu wanawake bali hata wanaume.

“Naipongeza TADB kwa kuona umuhimu wa kuwaletea wafanyakazi wake fursa hii muhimu ya kupata uelewa wa saratani mbalimbali na pia kupata nafasi ya kupima saratani ya matiti, saratani ya shingo ya kizazi na saratani ya tezi dume. Ni jambo muhimu kwa taasisi nyingine kuiga na kuwaelimisha wafanyakazi wake. Kwa pamoja tunajukumu la kuchangia kupunguza vifo vitokanavyo na saratani. Ugonjwa huu unakua kwa kasi. Ikumbukwe kuwa kwa kugundulika mapema na kuzingatia matibabu sahihi, saratani inaweza kutibika.

Bi. Felister Rutta mmoja wa wafanyakazi wa TADB aliishukuru menejimenti ya benki hiyo kwa kuwaletea semina hiyo ambayo alisema itawasadia wanyakazi kuufahamu ugonjwa huo na hivyo kuchukua tahadhari ikiwa ni pamoja na kuwaelekeza ndugu jamaa na marafiki.
Daktari Bingwa wa magonjwa ya Saratani kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dkt. Sadiq Siu (wa kwanza kushoto aliyesimama)akitoa mada juu ya saratani ya matiti, saratani ya mlango wa shingo ya kizazi na saratani ya tezi dume kwa wafanyakazi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) ikiwa ni sehemu ya benki hiyo kuadhimisha mwezi wa saratani ya matiti kwa kutoa elimu kwa wafanyakazi wake pamoja na kuwafanyia vipimo.

Baadhi ya wafanyakazi wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) wakifuatilia kwa makini mada juu ya saratani ya matiti, saratani ya mlango wa shingo ya kizazi, saratani ya tezi dume iliyokuwa ikitolewa na Daktari Bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka Taasisi ya Saratani ya Ocean Road Dkt. Sadiq Siu ikiwa ni sehemu sehemu ya benki hiyo kuadhimisha mwezi wa saratani ya matiti kwa kutoa elimu kwa wafanyakazi wake pamoja na kuwafanyia vipimo.






Share this

Related Posts

Previous
Next Post »