WAZIRI MAKAMBA ASEMA HADI KUFIKIA DESEMBA VIJIJI 3000 KATI YA 12,600 NCHINI VITAUNGANISHWA NA UMEME WA REA

August 14, 2023


 NA MASHAKA MHANDO, Bumbuli


WAZIRI wa Nishati January Makamba, amesema hadi kufikia Desemba mwaka huu, vijiji 3,000 kati ya vijiji 12,600 vilivyopo hapa nchini ambavyo havina umeme wa REA, vitaunganishwa na huduma hiyo.


Sanjari na suala la umeme, Makamba ambaye ni mbunge wa jimbo la Bumbuli, amewataka wana-CCM mkoani Tanga kumuunga mkono Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Rajabu Abdallah MNEC, kutokana na kazi anazozifanya tangu achaguliwe mwaka jana.


Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika mji wa Bumbuli, Waziri Makamba alisema Mwenyekiti huyo amekuwa wa kipekee kutokana na kwamba tangu achaguliwe umoja miongoni mwa wana-CCM umeimarika.


"Tumuunge mkono Mwenyekiti wetu kazi anazozifanya hazina kifani tangu achaguliwe amesukuma maendeleo ya mkoa wetu, lakini pia ameleta umoja kwa wana-CCM, fitina na majungu yamepungua," alisema Makamba.


Akizungumza changamoto mbalimbali zilizopo katika jimbo hilo, Makamba alisema halmashauri ya Bumbuli sasa angalau imekuwa na mzunguko wa fedha tofauti na awali ilipoanzishwa.


Alisema halmashauri inataka kujenga stendi mpya ya kisasa lakini changamoto iliyokuwepo ni ukosefu wa eneo la kujenga mradi huo mkubwa kutokana na kukosa eneo la kujengea stendi hiyo.


Akijibu swali kutoka kwa mpiga kura wake ambaye alisema katika kitongoji chake hakina umeme na hajui mbunge huyo ni lini atawapatia nishati hiyo, Waziri Makamba alisema kwa Tanzania kuna vijiji 3,000 na vitongoji 36,000 bado havijapata nishati ya umeme.


Alisema katika jimbo lake vijiji vyote vimepata umeme tofauti na maeneo mengine ambayo hata hivyo alisema kwamba wakandarasi wapo katika maeneo hayo wakiendelea na kazi za kuweka umme huo.


"Tunawaomba wananchi muwe na subira tunatarajia hadi kufika Desemba vijiji vyote vitakuwa vimewekewa umeme, mnajua mikoa kama Katavi na Rukwa bado hawajaunganishwa na  umeme wa gridi ya Taifa.


Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Tanga, Abdallah akizungumza na wananchi wa jimbo la Bumbuli alisisitiza kutaka wananchi wamuunge mkono Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutokana na kuutendea haki mkoa huo kwa kuleta fedha nyingi katika miradi mbalimbali.

Share this

Related Posts

Previous
Next Post »